NA
INNOCENT KANSHA - Mahakama
Mahakama ya Tanzania
imefanya Maboresho na inaendelea kufanya maboresho katika maeneo yote muhimu ya
utendaji kazi kupita nguzo tatu za Mpango Mkakati wa Miaka Mitano ulioanza
kutekelezwa mwaka 2015/16 hadi mwaka 2019/20.
Nguzo hizo ni Utawala,
Uwajibikaji na Matumizi ya Bora ya Rasilimali, Upatikanaji wa haki sawa kwa wote na kwa wakati na Kujenga taswira
chanya na Kurejesha imani ya wananchi kwa Mahakama.
Hivyo maboresho ya
sheria na kanuni mbalimbali yaliyofanywa na Mahakama ya Tanzania katika
kurahisisha utoaji wa haki maana yake ni kuhakikisha sheria zile ambazo
hazikuwa rafiki zilikuwa na muonekano wa
utaratibu wa zamani basi kuwekewa utaratibu mpya unaoendana na hali ya sasa.
Kwa upande wa kanuni
kama zilikuwa na utaratibu ambao sasa umepitwa na wakati basi kupitia Maktaba Kuu
ya Mahakama ya Tanzania, hupokea majuzuu
ya sheria hizo kwa kushirikiana na Katibu wa Kamati ya Sheria/Kanuni, ambayo huweza kushauri sheria zipi na kanuni
zipi ambazo ni za zamani zinazohitaji kuboreshwa.
Maboresho yanafanyika pale
ambapo kamati hiyo inaona kwamba sheria za sasa, katika muda huu hazifai kutumika na ni vitu gani vinafaa kutumika.
Akizungumzia
kuhusu maboresho
hayo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maktaba Mahakama ya Tanzania Mhe.
Kifungo Mrisho , ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo alisema ‘‘Katibu
wa Kamati ya Sheria na Kanuni huchukua kile ambacho huonekana ni bora
na kuhakikisha kwamba kanuni/sheria hizo zinafika kwa Mwenyekiti wa
Kamati ya
Kanuni/Sheria. Mwenyekiti huyo huchaguliwa na Jaji Mkuu akipata mawazo
yoyote
kuhusu maboresho ya sheria/kanuni huwasiliana na Jaji Mkuu ili kuitisha
kamati kupitia sheria hizo na kuweka maboresho hayo
kama ni ya sheria au kanuni”.
Kamati hiyo inakuwa na
utaratibu wa kuchukua maoni hayo ambayo yamekamilika na sheria hizo ambazo
zimefanyiwa mabadiliko na kuwasilisha kwa Jaji Mkuu, ambaye ana uwezo wa kuhakikisha
kwamba sheria na kanuni hizo ambazo zimefanyiwa marekebisho zinapelekwa kwa
wadau, ambao ni wahe. Majaji, Wasajili, Mahakimu na Mawakili wa kujitegemea kwa
ajili ya kuleta maoni yao.
Mrisho aliongeza maoni
hayo yakishaletwa kamati hiyo hukaa vikao kwa ajili ya kuyaangalia na kuweza
kutunga sheria/kanuni iliyokamili ili kuja na sheria/kanuni iliyokamili kwa
ajili ya kuhakikisha kwamba maboresho yamefanyika kuendana na wakati.
‘‘Kwa kifupi tu, ni kwamba Mhe. Jaji Mkuu kupitia Sheria Sura Namba
354 Judicature and Application of laws Act (JALA) sheria hii humpa mamlaka ya kutengeneza
kanuni za Mahakama Kuu, lakini pia katika sheria yoyote ile inayotungwa na Bunge,
hata hivyo kuna zinazompa mamlaka Waziri
kutengeneza kanuni au taratibu za kimuongozo wa namna gani sheria husika
itumike lakini kuna sheria zingine zinazompa mamlaka Jaji Mkuu kutengeneza
kanuni au taratibu .
Akitolea ufafanuzi wa
taratibu za maboresho alisema pale
ambapo Jaji Mkuu amepewa mamlaka ya kutengeneza sheria fulani au kanuni kupitia
kamati yake ikishaona hilo, kwa mfano, Sheria ya Vyombo vya Habari iliyotungwa
mwaka 2017 (Media Service Act of 2017) Mhe. Jaji Mkuu alipaswa kutengeneza kanuni.
‘‘Hivyo kamati hiI hungalia zile sheria zinazotakiwa kutungiwa kanuni na kumshauri
, Jaji Mkuu ambaye hutoa agizo kwa kamati sasa kanuni zitengenezwe”.alisisitiza.
Alisema hata kama kuna sheria yoyote ya mabadiliko
inayohitaji maboresho yanayofanyika bungeni au labda inataka kwenda bungeni
bado kamati hiyo hushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
kuhakikisha kwamba ile sheria ambayo inakuja basi iwe na ahuweni katika ubora
kwa ajili ya kuendeshwa katika Mahakama na misingi mizuri ya upatikanaji wa
haki.
“Hata mwaka 2016 kamati ya kanuni iliweza
kupendekeza mabadiliko ya Sheria Sura Namba 141 ambayo ni Sheria ya Rufani
inayotoa mamlaka ya kusajili rufaa katika Mahakama ya Rufani Tanzania haikuwa
na kipengele cha mapitio (review) lakini kamati ya kanuni iliweza kushauri
kufanyika maboresho hayo” alisema Mrisho.
Mabadiliko ya
Kanuni za Mahakama ya Rufani Tanzania ya 2019
(The Tanzania Court of Appeal Rules) yameleta kanuni za utendaji haki,
bila kuzingatia taratibu za kiufundi zilizopitiliza (overriding objectives).
Kanuni
hizi zinajulikana Kama “oxygen principle” Kama zinavyoainishwa chini ya kifungu
cha 3A na 3B cha Sheria ya Mamlaka ya Mahakama ya Rufani Tanzania (The
Appellate Jurisdiction Act). Kanuni hizi zinaitaka Mahakama kuepuka taratibu za
kiufundi katika kufikia utoaji wa haki.
Kuanzia mwaka 2016,
2017, 2018 na 2019 kuna mabadiliko ya maboresho ya kanuni mengi yamekwishafanyika
na yapo kwenye matumizi lakini ni mabadiliko yanayoletwa na maboresho ya sheria
zinazotumika mahakamani kwa kupitia kamati hiyo.
Alifafanua kuwa hadi sasa sheria na kanuni , ambazo zimekwisha
pitishwa na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali ni kanuni 41, lakini mapendekezo mengi yamekwisha fanyiwa kazi
na kamati ya maboresho, pia takribani sheria 38 zimefanyiwa kazi ingawa
hazitangazwa katika gazeti hilo.
Lengo likiwa ni
kurahisiha utaratibu mzima wa uendeshaji wa mashauri kuanzia hatua ya awali ya
upokelewaji wa shauri hadi hatua ya mwisho kabisa ya utekelezaji wa tuzo
uliotokana na hukumu au uamuzi ama amri ya Mahakama.
Mrisho alisema kuwa ikumbukwe kamati hiyo ilianzishwa Julai, mwaka 2014 wakati wa
utawala wa Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Othuman Chande na Mwenyekiti wake wa
kwanza alikuwa Mhe. Jaji Edward Rutakangwa kamati inaundwa na Wahe. Majaji wa
Mahakama ya Rufani Tanzania wanne,
Wahe. Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wanne na pia sekretarieti ya wataalamu
watatu ambao wote ni wanasheria wabobezi.
Hadi mwaka 2019 wakati
kamati hiyo ilifanya kazi ya mwisho ya kupitisha
utaratibu wa kuweza kutoa hukumu au kutoa adhabu kwa mahakimu (Sentencing
Guideline Manual) ambao umepitishwa Desemba, mwaka 2019, na Kamati ya Maboresho
ya Kanuni na kuzinduliwa. Januari 31, mwaka 2020.
Hizi zote ni taratibu
ambazo zinazoboresha ufanisi wa kazi wa Mahakama, utaratibu huu umewekwa
kisheria ufuatwe ili kuongeza tija katika utendaji wa kazi.
“Kamati hii
inashughulikia mambo mengi kama vile kutoa mapendekezo juu ya utoaji wa vitabu mbalimbali
vya maelekezo au miongozo mfano kamati inatoa ushauri juu utoaji wa kitabu cha
maelekezo au mwongozo wa ukazaji wa hukumu (Execution Guideline Manual), pia
kuna mwongozo mwingine wa watumiaji wa Mahakama ili kuwapa uelewa mpana
watumiaji kujua taratibu za Mahakama.(Court users Guideline Manual)” alisema.
Kingine cha Mwongozo wa
Usimamizi wa Mashauri (Case Management Guideline) hii inasaidia taratibu za
uendeshaji wa kesi mahakamani, kitaelezea taratibu za uendeshaji wa kesi
mbalimbali kama vile madai, jinai, talaka, mirathi na kesi nyingine nyingi
zinazofunguliwa mahakamani.
Kwa
upande wake Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.Shamillah Sarwatt, alisema maboresho haya yametoa mwanga chanya
kwa Mahakama na wadau mfano; Kanuni za Kusajili kesi kwa njia ya Mtandao
(Electronic Filing Rules) za mwaka 2018.
‘‘Zinatoa
fursa kwa Wakili wa Serikali na wa kujitegemea ama mtu mwingine yeyote kusajili
shauri mahala popote pale alipo bila kulazimika kufika mahakamani kwa kutumia Teknologia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), vivyo hivyo kwa kutumia kanuni hizi mlolongo
wa taratibu nzima za usajili wa mashauri umerahisishwa na hivi sasa inachukua
siku moja tu badala ya hapo awali ilikuwa inachukua muda mrefu zaidi,”alisema.
Msajili huyo.
Sarwatt
aliongeza kuwa mabadiliko mengine yaliyofanyika
ni ya Sheria Anuai Namba 8 ya Mwaka
2018 ambayo imefanyiwa marekebisho, ikiwemo Sheria ya Mamlaka ya Mahakama ya
Rufani Tanzania, iliyoiwezesha Mahakama
hiyo, kutofungwa na sababu za kiufundi
wakati wa kusikiliza shauri.
Nyingine ni Sheria ya
Migogoro ya Ardhi Sura Namba 216 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002 (Land
Dispute Act Cap. 216 RE 2002) nayo imefanyiwa marekebisho na kuruhusu Wahe.
Mahakimu wenye mamlaka ya nyongeza kusikiliza mashauri ya migogoro ya ardhi
katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
Kupitia maboresho kuna
mabadiliko ya jedwali la sheria za madai na taratibu zake ya mwaka 2019,
yamepunguza hatua za usikilizwaji wa mashauri ya madai kutoka hatua 38 hadi
hatua 22 tu zitakazo tumika mahakamani.
Maboresho haya lengo
lake ni kusaidia uharakishwaji wa utoaji wa haki kwa wakati na kwa wote, urahisishaji
wa utaratibu mzima wa kuendesha mashauri unalenga katika kupunguza muda wa
shauri kukaa mahakamani hivyo kutoa fursa kwa mdaawa wa shauri kutumia muda huo
katika shughuli za uzalishaji mali kwa faida ya mtu mmoja mmoja na kwa Taifa
letu kwa ujumla. Msajili wa Mahakama Kuu
ya Tanzania.
Mhe.Shamillah Sarwatt, akifafanua jambo kuhusu
mabadiliko hayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...