Na Sajini Taji, Shani Mhando, Morogoro
KAIMU Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jinsia katika Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto Bi.Mboni Mgaza amepongeza
kuanzishwa kwa mtandao wa wanawake katika Jeshi la Magereza nchini.
Akizungumza
katika ufunguzi wa mafunzo ya mtandao wa wanawake katika Jeshi la
Magereza jana Mkoani Morogoro, Bi Mboni amesema, hii ni hatua nzuri sana
yakupongezwa kwa Jeshi hilo kwani itahakikisha wanawake katika nyanja
zote wanatumia fursa mbalimbali zilizopo na zitakazojitokeza ndani ya
Jeshi hilo na nje ya Jeshi ili kujipatia mafanikio.
Ameongeza
kuwa msingi wa kuwepo kwa mitandao ya wanawake nchini ni kuwawezesha na
kuwajengea uwezo wanawake katika nyanja za kiuchumi, mafunzo, ajira,
uongozi na maamuzi ili kuweza kutimiza majukumu yao bila kubaguliwa
jinsia zao.
“Ni matarajio
yangu kuwa kuanzishwa kwa mtandao huu ndani ya Jeshi la magereza
utazingatia miongozo na kanuni mbalimbali zilizotolewa na serikali
kuhakikisha katika maeneo yote yenye changamoto za usawa wa kijinsia ili
mwanamke awezeshwe na aweze kukabiliana nazo,” alisema Bi. Mboni.
Aidha
Bi. Mboni amewaasa washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia mambo yote
watakayofundishwa katika mafunzo hayo ili wawe wawakilishi wazuri kwa
askari wote wa kike katika Jeshi la Magereza hivyo kuwajengea uwezo,
kukuza uelewa na kuwaunganisha ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi
zaidi.
“Jukumu mlilopewa
na Jeshi la Magereza la uelimishaji ni jukumu muhimu sana katika ustawi
wa mtandao wa wanawake ndani ya Jeshi la Magereza,
ninauhakika,
mafunzo mtakayoyapata hapa yatawaongezea uwezo wa kutekeleza jukumu
hili muhimu na kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya mtando
ndani ya Jeshi,” alisema Bi Mboni.
Kwa
upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia katika Jeshi la Magereza, Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Bertha Minde amesema kuwa kuanzishwa
kwa mtandao wa wanawake ndani ya Jeshi la Magereza kumewawezesha
wanawake kushika nafasi za juu za uongozi katika Jeshi hilo huku
akitolea mfano wa baadhi ya viongozi wanawake walioshika nafasi za juu
akiwemo Kamishna(01), Kamshna Msaidizi Mwandamizi(01) na Makamishna
Wasaidizi(06) ingawa bado kuna upungufu mkubwa wa kinamama katika nafasi
za juu za uongozi.
Naye
Msemaji wa Jeshi la Magereza, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Amina
Kavirondo amemuomba Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo Bi. Mboni Mgaza
kuendelea kuwaunga mkono katika mtandao wa wanawake katika Jeshi la
Magereza ili kuwezesha kufikia malengo waliyokusudia
Mtandao
wa wanawake katika Jeshi la Magereza ulianzishwa rasmi Desemba 7, 2018
baada ya Mkutano wa SADC uliofanyika Desemba, 2011 nchini Afrika ya
Kusini ambapo katika kikao hicho wazo la mtandao wa wanawake
lilirasimishwa na kuwekewa mikakati.
Kongamano la siku mbili la Mtandao wa wanawake katika Jeshi Magereza (TPS WOMEN NETWORK) limefanyika Mkoani Morogoro kuanzia Juni 22, 2020. #Pichani ni Wana Mtandao wanawake wa Jeshi hilo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...