Na
Mwandishi Wetu,MAELEZO-DAR
ES SALAAM
OFISI
ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini imesema ruzuku sio kigezo cha Chama Cha
Siasa kuwa na nguvu ya kushika dola na vijenge
hoja na ushawishi itikadi yake
kwa wananchi katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na
Madiwani Oktoba mwaka huu.
Rai
hiyo imetolewa leo (Jumanne Juni 30, 2020) Jijini Dar es Salaam na Naibu
Msajili wa Vyama Vya Siasa Nchini, Mohamed Ahmed wakati wa kufunga kikao kazi
cha kuwajenga uwezo Viongozi wa Vyama vya Siasa na kusema vyama vyote vipo sawa kwa mujibu wa sheria.
Ahmed
alisema katika kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu,
Vyama vya Siasa nchini havina budi kujitazama na kujikosoa kwa hoja zilizo
imara zenye uwezo wa kuwashawishi wanachama wake katika msingi wa kushika dola
baada ya kutazama ruzuku, kwani wakati wa kuanzisha mfumo wa vyama vingi nchini
mwaka 1992, vyama hivyo havikuwa na uwezo wa kifedha.
‘Ukitazama
Vyama vya siasa vya mwaka 1992 sio vya leo, tulianza tukiwa wachanga kabisa na
kushiriki katika chaguzi mbalimbali na leo hii vimeanza kujijenga siku hadi
siku, tuvijenge vyama vyetu kwa ajili ya ushindani wa hoja katika uchaguzi na
kushika hatamu ya uongozi’’ alisema Ahmed.
Aliongeza
vyama voyte vyenye usajili wa kudumu vina haki sawa kwa mujibu wa sheria na
kuwa hata vyama vyenye uwezo wa ruzuku vimejikuta vikiingia katika migogoro ya
mara kwa mara baina yao na kuathiri dhana ya msingi mkuu wa vyama vya siasa,
ambayo ni kushika hatamu ya uongozi na kuongoza dola.
Akifafanua
zaidi alisema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itaendelea kushikiana na
vyama vyote vya siasa katika kuwajengea uwezo katika kipindi hiki cha kuelekea
katika Uchaguzi Mkuu kwa kupokea maoni, changamoto na kuendesha mikutano ya
mara kwa mara na wadau wa siasa.
Aidha
Ahmed alivikumbusha vyama vya siasa kuendeleza dhana ya uvumilivu, mshikamano
na ushirikiano baina yao na kushindana kwa hoja na kuepuka tofauti za itikadi
za siasa, upinzani, kwa kuwa nchi ndiyo kipaumbele cha kwanza katika jamii
yenye amani na utulivu.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Chama Cha Mapinduzi (CCM) Anna
Abdallah aliipongeza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kuitisha mkutano
huo kwa kuwa umetoa fursa kwa vyama hivyo kufahamu wajibu wa msingi wa vyama
vya siasa katika kushiriki katika maendeleo ya nchi.
Anna
alisema mkutano huo umetoa taswira halisi ya mtazamo wa vyama vya siasa na
nafasi ya wananchi katika kufanya uamuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu
wajibu na haki yao ushiriki wao katika maendeleo ya nchi na kuvikumbusha vyama
hivyo kuwa siasa sio uhasama.
Naye
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Nchini, John Shibuda alisema suala la
amani na utulivu ni jambo muhimu linalopaswa kupewa kipaumbele na mamlaka na
taasisi mbalimbali za dola katika kipindi hiki cha kuelekea katika Uchaguzi
Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
‘Mwezi
Julai tunatarajia kuwa na kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa, ambapo tutakutana
na mamlaka za dola ikiwemo Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa ili kuweza kuwekana sawa na kujitafakari sote kwa pamoja nafasi
tuliyonayo kuelekea katika Uchaguzi Mkuu’’ alisema Shibuda.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...