Na Agnes Gerlad
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inaendelea na shughuli za Usajili na Utambuzi wa Watu nchini kote ambapo wananchi wanaendelea kupatiwa huduma katika ofisi za Usajili za NIDA zilizoko katika kila wilaya nchini.
Kwa mujibu wa Msemaji wa NIDA, Bw. Geofrey Tengeneza amesema, NIDA kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji, Uongozi wa Wilaya/Mkoa, Serikali za Mitaa na Wadau wengine inaendelea kutoa huduma zote zinazohusiana na Usajili na Utambuzi wa watu kama ilivyokuwa awali.
Ameongeza kusema kwamba, Usajili wa awali kwa maana ya Mwombaji kujaza fomu ya Maombi ya Utambulisho wa Taifa, kuchukuliwa alama za Kibaiolojia inayohusisha mwombaji kupigwa picha, kuchukuliwa alama za vidole na kuweka saini ya kielektroniki unaendelea kufanyika katika ofisi zote za Usajili za NIDA zilizoko katika wilaya zote nchini kwa kuzingatia tahadhari na maelekezo yaliyotolewa na Wizara ya Afya juu ya kujikinga na changamoto ya janga la Corona (COVID 19).
Aidha ametoa rai kwa wateja waliokamilisha Usajili kuangalia Namba zao za Utambulisho wa Taifa kupitia Kituo cha Huduma kwa Mteja, kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwenda namba 15096 ama kupitia tovuti yetu www.nida.go.tz (https://services.nida.go.tz/nidportal/get nin.aspx) bila kulazimika kufika kwenye ofisi za Usajili za wilaya jambo linalowaokolea wananchi muda wao na kupunguza msongamano kwenye ofisi za Usajili.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...