RAIS Dkt. John
Magufuli ametoa siku 30 kwa Viongozi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano kumsimamia usiku na mchana mkandarasi wa kampuni ya Padiel JV
kuhakikisha anakamilisha kwa haraka kazi
ya ujenzi wa barabara ya Kilosa- Dumila yenye urefu wa Kilometa 24.
Akizungumza katika
hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa barabara hiyo leo (Jumatatu Juni
29, 2020), Rais Magufuli alisema hajaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi
huo inayofanywa kasi ya mkandarasi huyo kutokana ujenzi wa barabara hiyo kuchukua
muda mrefu kukamilika.
Alisema kumekuwepo na
malalamiko ya makampuni mengi ya kizalendo yakilalamika kutopewa kazi za miradi
ya serikali, lakini pindi yanapopewa kazi hiyo yameshindwa kutekeleza ujenzi wa
miradi hiyo, hatua inayosababisha kuchelewesha maendeleo ya wananchi.
Aidha Rais Magufuli
alimtaka Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe
pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROAD) kuhakikisha
kuwa iwapo kuna vikwazo vinavyokwamiza utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo
ikiwemo malipo yanashughulikiwa kwa haraka.
‘’Sifurahishwi na
kazi ya mkandarasi ningekuwa mimi ni Kamwelwe (Waziri) basi leo asingekuwepo
huyu mkandarasi, haiwezekani tuwape kazi halafu ifanyike ya hovyo hivi, natoa
rai kwa makandasi wote wanaotekeleza miradi ya ndani wabadilike’’ alisema Rais
Magufuli.
Aliongeza kuwa katika
kipindi cha uongozi wake, Serikali ya Awamu ya Tano kamwe haitowatetea
wakandarasi wazembe na kuitaka kampuni ya Padiel JV kuhakikisha ujenzi wa
barabara hiyo inakamilika haraka kwa kuwa kwa kipindi kirefu wananchi wa Wilaya
ya Kilosa wamekuwa wakiishi katika mateso makubwa ya barabara hiyo.
Aidha Rais Magufuli
aliiagiza Wakala wa Barabara Nchini Mkoa wa Morogoro kuanza kufanya usanifu na
upembuzi yakinifu wa kipande cha barabara iliyosalia ya Kilosa-Mikumi yenye
urefu wa Kilometa 70 ili kipande hicho kiweze kukamilika kwa haraka.
Naye Afisa Mtendaji
Mkuu wa TANROAD, Mhandisi Patrick Mfugale alisema ujenzi wa barabara hiyo inayounganisha
Wilaya ya Handeni (Tanga)-Turiani-Dumira-Kilosa- Mikumi, una gharama ya kiasi
cha Tsh. Bilioni 32 na kukamilika kwake kunatarajia kupunguza changamoto ya
wasafiri kusafiri umbali mrefu pasipo na barabara ta mchepuko.
Alisema kuwa ujenzi
wa barabara hiyo ulianza februari 2019 na unatarajia kukamilika mwezi Januari
2020 ambapo ujenzi huo unatarajia kuwanufaisha makandarasi wazalendo kupata
ujuzi katika ujenzi wa barabara.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...