TAKUKURU MANYARA YAWASHIKILIA MAAFISA WATATU WA TRA KWA RUSHWA
Na mwandishi wetu, Babati
TAASISI
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara,
inawashikilia maafisa watatu wa Mamlaka ya mapato nchini (TRA) kwa
kuomba na kupokea rushwa ya shilingi milioni moja kwa mfanyabiashara wa
eneo hilo ili wasimuongezee makadirio ya kodi katika biashara yake ya
duka la rejareja.
Mkuu
wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu aliwataja maafisa hao
wa TRA wanaowashikilia ni Eva Joseph Mtandao, Jackline Leonard Manjira
na Ephrahim John Medard.
Makungu
alisema uchunguzi wa TAKUKURU Mkoani Manyara, ulibaini kuwa
mfanyabiashara huyo alikadiriwa kulipa kodi ya shilingi 250,000 kwa
mwaka na mtumishi wa TRA ambaye hakumdai rushwa.
Alisema
mfanyabiashara huyo akaomba kulipa kodi hiyo kwa awamu na akakubaliwa
ambapo hadi Juni 20 alikuwa amelipa awamu ya kwanza ya kodi
aliyokadiriwa.
"Wakati
akiendelea na biashara yake huku akisubiri kulipa awamu ya pili
alifuatwa tena na watuhumiwa hao watatu ambao walimwambia kuwa
amekadiriwa chini ya kiwango kwani kwa biashara yake alitakiwa kuwa na
mashine ya EFD hivyo ametenda makosa," alisema Makungu.
Alisema
baada ya maelezo hayo walimtaka aende ofisi za TRA zilizopo mjini
Babati kwa hatua zaidi jambo ambalo mfanyabiashara huyo alilitimiza kwa
kufika ofisini hapo.
Alisema
alipofika mjini Babati mfanyabiashara huyo alielezwa kuwa alikadiriwa
chini ya kiwango hivyo anatakiwa kulipa kodi ya shilingi 450,000 kwa
mwaka na faini ya shilingi milioni 3 kwa kutotumika mashine ya EFD.
"Mfanyabiashara
huyo aliwaeleza maafisa hao kuwa hawezi kulipa fedha hizo kutokana na
biashara aliyonayo, vinginevyo ni bora afunge tu biashara hiyo, baada ya
kutoa msimamo huo ndipo akafahamishwa na Afisa Jackline Manjira wa TRA
Babati ili asipigwe faini awape shilingi milioni moja," alisema
Makungu.
Alisema hata
hivyo, kutokana na mwamko walionao wananchi wa Manyara kwa sasa
mfanyabiashara huyo aliamua kutoa taarifa TAKUKURU na mtego wa shilingi
milioni moja uliandaliwa ambao uliwezesha kukamatwa kwa watumishi hao.
Alisema
uchunguzi unaonyesha kuwa baada ya watumishi hao kukabidhiwa fedha za
mtego wa hongo Jackline Manjira na Eva Mtandika waliandika kwenye faili
la mfanyabiashara huyo kuonyesha kuwa amesamehewa ongezeko la kodi na
ununuzi wa mashine ya EFD hadi mwaka 2021.
"Tunatarajia
kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao wakati wowote mara uchunguzi
utakapokamilika, tunawataka TRA Babati na watumishi wa umma kwa ujumla
wafahamu kuwa uadilifu siyo karama au kipaji ni uamuzi tu wa mtumishi wa
umma," alisema Makungu.
Makungu
alitoa wito kwa wana Manyara na watanzania kwa ujumla kuendelea kutoa
taarifa za rushwa kwa ofisi ya wilaya iliyopo karibu ambapo TAKUKURU
wamefungua ofisi za wilaya kote Tanzania bara au wawasiliane nao kwa
namba ya dharura 113.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...