Charles James, Michuzi TV

WANAWAKE nchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi nchini na kuepuka kusubiri nafasi za maalum.

Pia wametakiwa kuwa mstari was mbele katika kuhamasisha amani na utulivu na wasikubali kutumika na vyama vyao au na wanasiasa kuvuruga amani kwa maslahi yao.

Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Jenista Mhagama wakati akizungumza na viongozi wanawake ww vyama vya siasa ambapo amewataka kusimama kidete kusimamia amani na kuwa chachu ya utulivu kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Viongozi hao wanawake wamekutana na Waziri Mhagama kwa lengo la kumpogeza kwa kusimamia vema vyama vya siasa ambapo wizara yake ndio inayohusika na usimamizi wa vyama vya siasa kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Waziri Mhagama amesema wanawake wana nguvu kubwa na uwezo wa kuwa viongozi na ndio maana Rais Dk John Magufuli amewaamini katika nafasi mbalimbali na hata wakati alipoteuliwa na chama chake kuwa mgombea Urais wa CCM alimchagua tena Mama Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza wake kwa mara nyingine.

" Nguvu yetu wanawake ni kubwa sana na kipindi hiki tunapoelekea kwenye uchaguzi nitoe rai kwenu kugombea nafasi za Uongozi kupitia vyama vyenu, chukueni fomu mkachuane kwenye majimbo na kata msiogope kwa sababu uwezo tunao.

Tusikubali kusubiri nafasi za upendeleo kama tuna lengo la kufikia 50/50 basi inatulazimu pia tuingie kwenye uwanja wa mapambano ili tupime nguvu zetu, na kwa sababu sisi tuna uwezo mkubwa basi naamini tutashinda," Amesema Mhagama.

Amewataka wanawake kuwa mstari wa mbele katika kuyasema maendeleo yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano kwani yanawahusu watanzania wote bila kubagua Itikadi zao za kisiasa, kiimani na kikabila.

" Tumefikia uchumi wa kati kwa sababu pia ya utulivu wa vyama vya siasa ambavyo nyie ni viongozi, niwasihi tukahubiri pia maendeleo yetu ambayo nafahamu nyie mnayajua kwa sababu mmefanya ziara kwenye miradi inayofanywa na mmejionea kazi kubwa ambayo inafanywa," Amesema Waziri Mhagama.

Kwa upande wake Mratibu wa tukio hilo ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha UDP, Saumu Rashid amemshukuru Waziri Mhagama kwa kukubali kupokea zawadi yao na kumpongeza kwa namna ambavyo amevilea vyama vya siasa kwa muda wote wa miaka mitano.

" Tunakupongeza sana Waziri kwa ushirikiano mkubwa ambao umetupatia, hakika umekua mwema kwetu na tunakuombea urudi bungeni, sisi kama viongozi wanawake tunakuahidi tutakua mstari wa mbele kuchochea amani na utulivu kwenye uchaguzi mkuu," Amesema Saumu.

Nae Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amewataka viongozi hao kutoruhusu kuwa sehemu ya machafuko yanayosababishwa na baadhi ya wanasiasa wasio na uzalendo wa Nchi yao.

" Niwapongeze kwa Umoja wenu huu kama viongozi wanawake, mmekuja hapa pamoja mkiwa mmevaliwa sare moja ambayo siyo ya vyama vyenu, niwasihi Umoja huu huu ndio muende nao kwenye uchaguzi mkiweka mbele maslahi ya Nchi yetu," Amesema Jaji Mutungi.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Ajira Kazi Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama akipokea tuzo kutoka kwa Mwenyekiti wa Viongozi Wanawake wa Vyama vya Siasa, Saumu Rashid ambapo wanawake hao Viongozi walimuandalia Waziri Mhagama zawadi ya kumpongeza kwa utendaji kazi wake.
 Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi akizungumza katika mkutano huo wa Waziri Mhagama na Viongozi Wanawake wa vyama vya Siasa nchini.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Ajira Kazi Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama akizungumza na viongozi wanawake wa vyama vya siasa ofisini kwake jijini Dodoma leo. Kulia ni Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.
 Viongozi Wanawake kutoka Vyama mbalimbali vya siasa nchini wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Ajira Kazi Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama katika mkutano wao wa pamoja ambapo viongozi hao wanawake walienda kumpongeza Waziri Mhagama.
 Kiongozi wa Viongozi Wanawake wa Vyama vya Siasa, Saumu Rashid akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake baada ya kumkabidhi Waziri Mhagama tuzo ya kutambua utendaji kazi wake
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Ajira Kazi Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama (katikati) na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wanawake wa vyama vya siasa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...