
Mkurugenzi
wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi
***********************************
Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma.
Serikali kupitia Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuwa, haina upungufu
wa chanjo wa aina yeyote hivyo kuwataka wazazi/walezi kuwapeleka watoto
wao kuwapatia chanjo katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi
wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi wakati alipotembelea
ghala ya kuhifadhia chanjo iliyopo hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma
kukagua hali ya chanjo katika mkoa huo.
Dkt. Subi amesema kuwa, chanjo
zote aina tisa ambazo zinakinga dhidi ya magonjwa kumi na tatu zipo
kwenye ghala hilo“tulikua na upungufu wa aina mbili za chanjo nchini
kati ya tisa ambazo tumekuwa tukizitoa lakini, sasa hivi chanjo zote
zipo, kwani zimeshawasili hapa nchini na usambazaji unaendelea”, amesema
Dtk. Subi.
Hata hivyo Dkt. Subi amesema kuwa,
upungufu huo wa chanjo ulitokea baada ya Dunia kukumbwa na janga la
mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 ambapo anga zote zilifungwa kwani chanjo
husafirishwa kwa mnyororo baridi, kwahiyo huitaji usafiri wa anga.
“Tunamshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kulifungua anga la
Tanzania ambapo, chanjo sasa zimeanza kuingia nchini na hadi sasa
mikoa kumi na tatu(13) chanjo hizi zimeshapokelewa kati ya mikoa 26, na
mikoa mingine kumi na tatu ya Tanzania Bara usambazaji unaendelea
kupitia Bohari ya Dawa (MSD)”.
Aidha, Dkt. Subi alisema kuwa,
usambazaji wa chanjo hizo mbili ambazo wananchi walikua wanazikosa,
umeshaanza na watazipata kwa uhakika, huku akielekeza bohari ya dawa
nchini (MSD) kuhakikisha chanjo zote zimefika katika mikoa iliyosalia
ya Tanzania Bara ifikapo mwishoni mwa wiki hii.
“Waganga Wakuu wa Mikoa na
Halmashauri wote nchini hakikisheni chanjo hizo mnazipeleka kwenye vituo
vyetu vya kutolea huduma za afya na muwajulishe wananchi kwamba chanjo
zipo na zinapatikana bila malipo yeyote, wazazi na walezi pelekeni
watoto wenu kupata chanjo katika mikoa yenu”Alisisitiza Dkt. Subi.
Kwa upande wa taarifa iliyotolewa
na moja ya chombo cha habari hapa nchini kwa kukosekana kwa chanjo ya
kuzuia kuhara (Rota) Dkt. Subi alifafanua kuwa, nchi ya Tanzania
haijawahi kukosa chanjo hiyo,huku akiweka bayana kuwa, chanjo
zilizopungua kwa mwezi mmoja na nusu ni chanjo ya Polio na Surua-Rubella
hali iliyosababishwa na mlipuko wa Covid-19 Duniani, huku akisisitiza
kuwa serikali imekua ikinunua chanjo hizo kutoka nchi za Ulaya na Asia.
Aliendelea kusema kuwa, Serikali
inaendelea kutoa fedha za chanjo, na kuweka wazi kuwa hadi sasa imetoa
zaidi ya shilingi bilioni 18 kwa ajili ya ununuzi wa chanjo na
kuifanya Tanzania kuendelea kuwa katika kiwango cha juu cha utoaji wa
chanjo kwa zaidi ya asilimia 98 kwa miaka sita mfululizo.
Hata hivyo, Dkt. Subi amesema
kuwa, Tanzania haijawahi kupata mgonjwa wa kupooza tangu mwaka 1996,
jambo linalotokana na uwepo wa hali nzuri ya upatikanaji wa chanjo,
huku akidai kuwa nchi ya Tanzania tayari imepata cheti cha utambuzi
kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2015.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...