Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
UPELELEZI katika kesi ya kufanya biashara ya upatu na kutakatishaji fedha Sh.bilioni 17 inayomkabili Mfanyabiashara Tariq Machibya (29) maarufu kama Mr.Kuku anayeiishi Osterbay jijini Dar es Salaam, liyoko mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, bado haujakamilika.
Leo Agosti 24, 2020 Wakili wa Serikali Ester Martin alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Janeth Mtega kuwa kesi hiyo leo imekuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi bado haujakamilika.
Kutokana na taarifa hiyo, Hakimu Mtega ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 7, mwaka huu kwa kutajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande.
Katika kesi hiyo inadaiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, kati ya Januari 2018 na Mei 2020, maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, mshitakiwa alifanya na kusimamia biashara ya upatu kwa kukusanya fedha toka kwa umma kwa ahadi kwamba zimewekewa kwa biashara ya kuku na watu wangepata asilimia 70 ya mtaji wa awali waliowekeza kwa miezi minne na asilimia 90 kwa mtaji wa awali uliowekezwa kwa miezi sita kiasi ambacho ni kikubwa kuliko mtaji uliokusanywa.
Pia kati ya Januari 2018 na Mei 2020, maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, Machibya alikubali kupokea fedha kutoka kwa umma ambazo ni Sh bilioni 17 bila kuwa na leseni.
Katika shtaka jingine indaiwa kati ya Aprili 26,2019 na Januari 26,2020 maeneo ya jiji hilo, mshitakiwa alijihusisha na miamala ya Sh 6,477,297,614.83 kwa kutoa kutoka kwenye akaunti ya CRDB ya Mr Kuku Farmers Ltd huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kusimamia biashara ya upatu.
Pia kati ya Januari 17,2020 na Machi 30,2020 maeneo hayo, Machibya alijihusisha na miamala ya Sh 629,249,576.36 kwa kutoa fedha hizo katika akaunti ya CRDB wakati akijua fedha hizo ni zao la biashara ya upatu.Kati ya Machi 5,2020 na Aprili 17,2020 maeneo ya Dar es Salaam, mshitakiwa alijihusisha na miamala ya 1,366,718,048.46.
Katika shtaka la sita, Mr. Kuku anadaiwa kati ya Januari 17,2020 na Januari 30,2020 maeneo ya CRDB Viva tower iliyopo Kinondoni, Dar es Salaam alijihusisha na miamala ya USD 107,893.73 na kuingiza fedha hizo kwenye akaunti ya CRDB.
Inadaiwa kati ya Machi 3 na 30, mwaka huu maeneo ya CRDB Waterfront mshitakiwa alijihusisha na kuingiza USD 146,300 kwenye akaunti ya Mr Kuku Farmers Ltd.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...