Katibu Tawala wa Wilaya ya Kondoa akitoa rai kwa wananchi wa Kondoa kuitumia Mahakama ili kusuluhisha migogoro yao.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi
wa Mahakama ya Wilaya Kondoa akitoa ufafanuzi juu ya maboresho ya
miundombinu ya Mahakama yalivyorahisisha utoaji haki kwa wakati.
Jengo Jipya la Mahakama ya Wilaya ya Kondoa linalotumika kutoa huduma za kimahakama.Picha na MAHAKAMA na Idara ya Habari-MAELEZO

**********************************
Na Innocent Kansha – Mahakama Kondoa
Mahakama ya wilaya ya Kondoa
imesikiliza na kumaliza mashauri ya jinai na madai 184 kati ya mashauri
262 yaliyokuwepo katika Mahakama za wilaya za Kondoa na Chemba.
Akizungumza na Maafisa Habari wa
Mahakama ya Tanzania, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya
Wilaya ya Kondoa Mhe. Francis Robert Mhina alisema mashauri hayo
yamesikilizwa na kumalizika kati ya mwezi Januari na Julai, mwaka huu.
“Mashauri yaliyobaki mwezi Desemba
2019 yalikuwa ni 152, yaliyosajiliwa kati ya Januari na Julai mwaka huu
ni mashauri 110, tumesikiliza na kumaliza jumla ya mashauri 184 na
kubakiwa na mashauri 78”, alifafanua Mhe. Mhina.
Kwa mujibu wa Hakimu Mfawidhi
huyo, asilimia kubwa ya mashauri yanayofunguliwa kwenye Mahakama hizo ni
yale yanayohusu ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji, pamoja na mauaji,
kujeruhi na mashauri ya kukutwa na nyara za wanyama pori.Alisema mashauri yanayohusu nyara
za taifa hasa wanyama pori yanatokana na uwepo wa mapori tengefu ya
hifadhi za Swaga swaga na Mkungunero.
“Wananchi wengi wanaoishi kando
kando ya hifadhi hizi wamekuwa wakiendesha shughuli zao mbalimbali za
kiuchumi bila kuzingatia mipaka na kujikuta wanakinzana na sheria za
hifadhi kama kulima ndani ya hifadhi, kuvua samaki, kuchoma mkaa,
kukutwa na nyara za Taifa na kuwinda wanyama pasipo kuwa na vibali
halali”, alisema Mhe. Mhina.
Mhe. Mhina alisema asilimia kubwa
ya mashauri ya mauaji yanatokea Wilaya ya Chemba. Mahakama ya Wilaya ya
Kondoa pia inahudumia Wilaya Chemba kwa sasa.
Kuhusu matumizi ya Tehama katika
Mahakama ya wilaya ya Kondoa, Mhe. Mhina amesema yamesaidia kwa kikubwa
kurahisisha suala la upatikanaji wa haki kwa wakati. Aliongeza kuwa
mfumo wa kusajili mashauri (JSDS II) unatumiwa vizuri na watumishi
katika kutunza kumbukumbu za kila siku za mashauri baada ya kufungiwa
mkongo wa Taifa wa mawasiliano.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya
Kondoa Bw. Andrea Ng’hwani alisema Serikali Wilayani humo imeyapokea
maboresho ya miundombinu ya Mahakama kwa furaha kwani yametatua
changamoto na kero za wananchi wa Kondoa kwa kiasi kikubwa.
“Nawakumbusha wananchi kuwa nchi
hii inaongozwa kwa misingi ya kisheria na hakuna mazingira yoyote
yanayoruhusu mtu kujichukulia sheria mikononi ndiyo maana kuna Jeshi la
Polisi na Mahakama ili kutatua kero zao” alisisitiza Katibu Tawala.
“Kero za wananchi zimepungua sana
na sasa hatupokei malalamiko yanayohusu Mahakama kiutendanji na mambo
mengine yanayohusu uelewa wa taratibu za kimahakama tumekuwa mstari wa
mbele kuyatolea ufafanuzi wa kuwaelekeza sehemu sahihi ya kutatua na
kupata ufafanuzi”, alisema Katibu Tawala.
Bw. Ng’hwani alisema wananchi
wanapaswa kupeleka migogoro yao mahakamani ili iweze kutatuliwa kisheria
na pale wanapoona hawajaridhika na maamuzi, wakate rufaa Mahakama ya
juu zaidi kupata haki ili Amani na utulivu vizidi kuimarika.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...