Na Said Mwishehe, Michuzi TV

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania(JET)kimeendele kuwakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali nchini kwa ajili ya kuweka mikakati na kujengeana uwezo utakaosaidia katika uhifadhi wa wanyamapori na mazingira pamoja na kukabiliana na ujangiri nchini.

JET iliwakutanisha wadau hao katika mafunzo maalumu yaliyofanyika kwa njia ya mtandao ambapo wengi wao wameelezea jitihada wanazofanya kwenye taasisi zao kukabiliana na ujangiri pamoja na kuweka mazingira mazuri ya kulinda uhifadhi wa wanyamapori.

Mafunzo yamefadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Marekani(USAID) kupitia mradi wake wa Protect uliojikita kwenye kutoa elimu ya kutokomeza ukatili kwa wanyamapori na uhifadhi wa mazingira

Hata hivyo wakati wa mafunzo ambayo waandishi wa habari za mazingira nchini ambao ni sehemu ya wanachama wa JET nao walipata fursa ya kuwasikia wadau hao na mikakati yao kwa kila mmoja katika eneo lake na mwisho wa siku kutimiza lengo kusudiwa kuhusu ufahifadhi wa wanyamapori.

Mwakilishi kutoka Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania(TPSF) Victoria Michael anasema sekta binafsi kwa sasa zinatambua kuwa zinawajibu wa kushirikiana na sekta nyingine katika uhifadhi wa wanyamapori nchini.

"Sekta binafsi tunamchango mkubwa lakini tunawajibu wa kushiriki kikamilifu katika kukabiliana na ujangiri.Kwanza unapoacha wanyama wakauliwa na uharibifu wa mazingira ukafanyika maana yake hata mazingira ya kufanya biashara yanaharibika kabisa.

"Hivyo tunaendelea kuwapa elimu wanachama wetu wa sekta binafsi ikiwa kuwawezesha na wao wenyenyewe kutambua umuhimu wa wao kushiriki. Tumekuwa tukitoa mafunzo ya kutambua mbinu zinazotumiwa na majangari kutorosha wanyama.Hata kutambua namna wanavyohifadhi, lazima kuwepo na mbinu za kutambua na hiyo inalenga kuondoa na kupunguza utoroshwaji wa wanyama.

"Hata hivyo ombi letu tunashauri kuwepo na ushirikishaji kwenye sera ili kuhakikisha sekta binafsi nayo inapata nafasi ya kutosha ya kushiriki kwenye kulinda uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na ujangiri na biashara ya wanyamapori,"amesema.

Ameogeza kuwa sekta binafsi imeamua kuanzisha kamati ambayo itafanya kazi kwa miaka mitano na kazi kubwa ya kamati hiyo ni kwa ajili ya kusaidia kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye sekta ya uhifadhi wa mazingira na wanyama pori.

"Tumeona sekta binafsi nayo tayari imeanza kujiunga kwenye harakati za kuhakikisha wanyamapori wanahifadhiwa .Hapo awali sekta binafsi haikuwa na ushiriki mzuri lakini sasa tumeona namna ambavyo tunashiriki,"amesisitiza.

Kwa upande wake Salimu Msemo kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka yeye alijikita katika kuzungumzia mada ya masuala ya kisheria zinazohusu ujangiri na uwindaji haramu.

Amefafanua kuna sheria mbalimbali ambazo zinahusika katika eneo eneo hilo na baadhi ya sheria hizo ni sheria ya uhifadhi wa nyamapori, shera ya misitu, sheria ya hifadhi za Taifa, sheria ya makosa ya uhujumu uchumi na makosa ya kupangwa ambako hapo ndipo unaweza kukutana na ujangiri.

"Kuna sheria ambayo inayosaidia pale unapohitaji msaada wa kisheria katika kushughulikia makosa ya ujangiri kwa zaidi ya nchi mmoja kwa maana ya mtu anapofanya ujangiri na kukimbilia nchi nyingine.Pia kuna sheria inayohusu silaha hasa kwa kuzingatia ujangiri umekuwa ukihusishwa zaidi na matumizi ya silaha, hivyo kuna sheria ya kubana matumizi ya silaha zinazotumika kwenye ujangiri.

"Tunayo sheria ya utakatishaji fedha, tunafahamu makosa ya ungajiri ni makosa tangulizi ambayo yanachangia kutakatisha fedha.Katika kipindi hiki kuna sheria inayohusika kupambana na rushwa kwani tunafahamu biashara haramu ya ujangiri inakwenda sambamba na masuala ya rushwa,amesema Msemo.

Anafafanua kutokana na majukumu ambayo ofisi yao inafanya ya kuendesha mashtaka watenda makosa huwa wanachukuliwa adhabu pale itakapobainika kutenda makosa, hivyo miongoni mwa adhabu ni pamoja na kutaifishwa kwa vitendea kazi wanavyokutwa navyo.

"Kwa mfano gari iliyotumika kwenye ujangiri huwa tunashauri itaifishwe, pia kama kuna mali ambavyo tutajiridhisha imetokana na shughuli za ujangiri basi tumekuwa tukiiomba Mahakama kuitaifisha.

"Ofisi yetu kwa kushirikiana na taasisi nyingine zinazohusika na haki jinai kwa sasa angalau nyara za Serikali kwa sehemu kubwa sana ziko salama kutokana na ushirikiano kati ya taasisi moja na nyingine.Kutokana na utendaji kazi wa ofisi hii kwa kushirikiana na wadau wengine jamii nayo imeona umuhimu wa kulinda uhifahi wa mazingira na wanyamapori,"amesema.

Pia kumekuwepo na mchango mkubwa wa vyombo vya habari kuripoti hukumu za ujangiri na hiyo imeifanya jamii kutambua madhara ya ujangiri na hatua ambazo zitachukuliwa.

Wakati huo huo Mkurugenzi Msaidizi wa Kikosi cha Kupambana na Ujangiri Robert Mande amezungumzia uzuri wa mada zilizoandaliwa katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na JET na kufafanua unapozungumzia ujangiri watu wengi wanaona unazungumzia tembo tu, kumbe masuala ya ujangiri yanahusisha makosa mengine ya kupangwa.

Mande amesema ujangiri unapangwa na watu mbalimbali, wengine wanakuwa ndani ya nchi na wengine nje ya nchi.Hivyo vyombo vya ulinzi na usalama viliungana pamoja ili kufanya kazi hiyo, na sasa kunamafanikio sana na sasa vinaongozwa na ofisi ya NPC na kwamba uchunguzi wao unaongozwa na waendesha mashtaka.

"Utamaduni wa kila mtu kujifungia na kupambana na ujangiri imeshindwa kufanya kazi vizuri, hivyo kikubwa ambacho kinafanyika sasa ni kuunganisha wadau mbalimbali kutoka sekta tofauti na hivyo kumekuwa na mafanikio makubwa,"amesema.

Anaeleza huko nyuma kulikuwa na idadi kubwa ya tembo waliokuwa wanauliwa na ilipofika mwaka 2013 Tanzania ikawa kwenye orodha ya nchi ambazo zipo kwenye ujangiri mkubwa wa tembo.

Hivyo anasema kama nchi iliamua kufanya kitu kwa kuweka chombo maalum kwa ajili ya kushughulikia ujangiri nchini kwa kuunganisha vyombo vya ulinzi na ulalama, vyombo vya kisheria na wote ambao wanafanya kazi kwa pamoja.

"Kwa sasa kwa hiyo ujangili umepungua kwa asilimia 80 baada ya kuanza kushirikiana kwa vyombo vya ulinzi na usalama na taasisi nyingine,"amesema Mande huku akitoa takwimu katika maeneo mbalimbali yanayohusu ujangili, idadi ya kesi na kiasi cha fedha ambacho kimepatikana kutokana na jitihada zinazoendelea.

Anasisitiza idadi ya tembo kuanzia mwaka 2018 hadi sasa imeongezeka na inatia matumaini.Hivyo anashauri taasisi nyingine, taasisi za watu binafsi, mashirika ya umma wakishirikiana na Serikali kutakuwa na mafanikio makubwa zaidi yaliyopo sasa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya JET Dk.Ellen Utaru ametumia nafasi hiyo kueleza kikubwa ambacho washiriki wamejifunza ni kuendelea kuelimika katika mambo yanayohusu uhifadhi wa wanyamapori na mazingira na kwa waandishi wa habari ni vema wakajikita zaidi kwenye ufafanuzi na kutoa elimu kwa jamii

"Kupitia mafunzo haya waandishi wa habari za mazingira tumepata upande mwingine wa taarifa. Tunapaswa kuandika kwa usahihi kabisa ,tumepata kitu kizuri, pongezi kubwa kwa watoa mada, tunawashukuru na msiache kutupa msaada kadri tunavyohitaji.JETI na wanachama wetu tutaendelea kuhitaji ushirikiano wenu,"amesema.

Dk.Ellen anasema waandishi habari za mazingira wamepata wigo mpana wa kuandika zaidi."Wote tunayo majukumu na sio tu wale wanaosimamamia wanyamapori na wanyama bali ni jukumu letu wote.

Mkurugenzi Mtendaji wa JET John Chikomo ametumia nafasi hiyo kuelezea umuhimu wa mchango wa vyombo vya habari katika kuendelea kuihamasisha jamii ya Watanzania kutambua umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori na mazingira.

Pia wataendelea kuwajengea uwezo waandishi wa habari za mazingira kadri ya uwezo wao kwa kushirikiaa na wafadhili ambao wamekuwa wakiunga mkono juhudi za JET katika sekta hiyo .

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...