Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango,
Bw. Benny Mwaipaja (kulia), akiwaongoza Waziri wa Viwanda na Biashara,
Mhe. Innocent Bashungwa (katikati), Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet
Hasunga (wa pili kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Anthony Mtaka,
kutembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya
Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani
Simiyu.





(Picha na Peter Haule, WFM).
***********************************
Na. Peter Haule na Farida Ramadhani, WFM, Simiyu
Waziri wa Viwanda
na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa, amewataka Watanzania kutambua
umuhimu wa mifumo ya fedha iliyoanzishwa na Serikali kwa lengo la
kupunguza vitendo vya rushwa na kuweka mazingira mazuri ya utawala bora.
Waziri Bashungwa
amesema hayo alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango katika
maonesho ya Nanenane yanayoendelea Kitaifa katika Viwanja vya
Nyakabindi, Mkoani Simiyu.
Alisema kuwa rushwa itapungua endapo kiwango cha kukutana kati ya mtu na mtu kitapunguzwa hasa katika masuala yanayohusu fedha.
“Mifumo ya fedha
inayofanya kazi katika Serikali ya Awamu ya Tano ni ya Kielektroniki
hivyo mtu anaweza kufanya malipo kwa njia ya simu ya mkononi katika
ofisi yeyote ya Serikali bila kukutana na mtu, na hatua hii itapunguza
mazingira ya ushawishi wa rushwa”, alieleza Mhe. Bashungwa.
Aidha, Mhe.
Bashungwa, ameipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuweka Sera nzuri
za Fedha ambazo zimesaidia kuifikisha nchi katika uchumi wa kati miaka
mitano kabla ya wakati uliokuwa unatarajiwa awali mwaka 2025.
Aliongeza kuwa
Wizara yake itaishirikisha Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Taasisi ya
Uhasibu Nchini (TIA) kutoa elimu kwa wafanyabiashara wadogo na wenye
viwanda kuhusu elimu ya biashara na utunzaji wa hesabu ili kuimarisha
ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Akizungumzia
Kilimo Mhe. Bashungwa ameeleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2014-2019,
Sh. trilioni 1.3 zilitumika kila mwaka kuagiza nje yan chi chakula
ikiwemo ngano na Mafuta ya kupikia, bidhaa zinazoweza kupatikana nchini
endapo vijana wasomi wataangalia namna ya kuchochea mnyororo wa thamani
wakati wa kuandaa Sera.
Kwa upande wake
Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga, ameshauri suala la kodi ya
ongezeko la thamani (VAT) katika vifungashio vya mazao ya ndani kama
Pamba, Korosho na Kahawa liangaliwe upya ili kujenga ushindani dhidi ya
mazao kutoka nje ambayo yamesemehewa kodi hiyo jambo litakalochochea
ushindani na kulinda viwanda vya ndani.
Akieleza kuhusu
biashara ya mazao ya kilimo wakati wa changamoto ya Covid 19, Mhe.
Hasunga alisema kuwa baadhi ya nchi zimechukua hatua ya kufunga mipaka
na kuzuia mizigo na wasafirishaji kuingia katika nchi mbalimbali
zikiwemo nchi jirani.
“Sisi kama Wizara
ya Kilimo pamoja na wadau wengine tumeathirika kwa kiwango kikubwa,
tunakusudia kuwa na kikao cha pamoja katika maonesho haya ya Nanenane
kati ya Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda na Biashara Pamoja na
taasisi zake ili tuzungumze namna tutakavyo kabiliana na changamoto ya
ugonjwa huo”, alieleza Mhe. Hasunga.
Alisema kuwa
kikao hicho kitaangalia namna bidhaa zinazoharibika haraka kama
maparachichi na mbogamboga zinaweza kusafirishwa kupitia Bandari za
Tanga na Tanga badala ya kuzipeleka Mombasa.
Kwa upande wake
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango,
Bw. Benny Mwaipaja, aliwashukuru Mawaziri hao kwa kutembelea Banda la
Wizara, Nyakabindi, Simiyu na kueleza kuwa Wizara inafanya kila
linalowezekana kuhakikisha kuwa sekta ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na
Viwanda vinachangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Alisema kuwa
Wizara imeondoa kodi zipatazo 114 zilizokuwa kero katika sekta hizo na
hatua hiyo itaongeza tija ya uzalishaji na pia kuifanya nchi iendelee
kuwa na usalama wa chakula na kuahidi kuzifanyiakazi changamoto
zilizotolewa na Viongozi hao kwenye masuala ya kodi kwenye Sekta zao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...