WAZALISHAJI 141 wakubwa, wakati na wadogo nchini wamekabidhiwa vyeti na leseni za kutumia alama ya ubora ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) baada ya bidhaa wanazozalisha kuthibitishwa kukidhi viwango vya ubora.

Kati ya wazalishaji hao 58 ni wazalishaji wadogo ambao wanazalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo vitakasa mikono, vyakula, vilainishi, vifaa vya umeme na vya ujenzi.

Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa hafla ya kukabidhi leseni hizo kwa wazalishaji hao, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt Yusuf Ngeya, alisema imekuwa ni kawaida shirika kuwakabidhi vyeti na leseni za kutumia alama ya ubora wazalishaji ambao wanakidhi vigezo ili waendelee na uzalishaji wa bidhaa zenye ubora.

Alisema hatua ya bidhaa hizo kupatiwa vyeti na leseni ya lutumia alama ya ubora ya shirika hilo kutawafanya wazalishaji hao kuwa na uwezo wa kushindana na bidhaa nyingine sokoni, kuuza nchi za Afrika Mashariki bila bidhaa zao kulazimika kupimwa tena kwa ajili ya kuzithibitisha ubora na watapanua wigo wa biashara zao kwa kuyafikia masoko mengi zaidi.

"Ni wakati muafaka wa kuwapongeza na kuwapa moyo wajasiriamali wadogo ili nao waweze kuwa wakubwa kama wengine, tunakabidhi vyeti na leseni za ubora kwa wajasiriamali na kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu na hii ni kawaida yetu kila baada ya miezi mitatu kuwapongeza baada ya kupata vyeti vyao vya Ubora na leseni,"alisema na Dlt. Ngenya na kuongeza;

"Namshukuru Rais John Magufuli kwa kutoa fursa kwa ajili ya kuhudumia wajasiriamali wadogo bure pale wanapoomba bidhaa wanazozalisha wenyewe kuthibitishwe ubora na TBS."

Dkt.Ngeya aliwataka wajasiriamali hao kuwa mabalozi wazuri wa TBS
kwa kuhamasisha wananchi wanaojihusisha na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kwenda kuthibitisha ubora wa bidhaa zao wanazozalisha.

"Hakikisheni mnaendelea kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokubalika kila siku na sio leo mnapata leseni na cheti na badala yake mnaanza  kutengeneza bidhaa zisizokuwa na ubora tutakuwa tunapita na kuwafanyia ukaguzi wa mara kwa mara, kwani sheria inaturuhusu kufanya hivyo,"alisema.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ihnemeter, ambayo inazalisha na kuuza vifaa vya umeme ikiwemo Meter, Abraham Rajakili, aliishukuru TBS kwa kuwapatia vyeti na leseni za ubora kwani huo ni mwaga mzuri wa kuingia sokoni kwa kukubalika zaidi na kujiamini.

"Kwa kweli tunawashukuru TBS kwa hatua hii tunaamini kuwa bidhaa zetu zitaweza kufanya vizuri zaidi sokoni kutokana na kuwa na nembo za ubora ya TBS,"alisema

Wakati huo huo, Dkt, Ngenya alisema kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu,TBS imesajili takribani majengo 513 ambayo yanashughulikia chakula na vipondozi na kusajili bidhaa ya chakula na vipodozi 596 kwa kipindi hicho.

"Tangu mabadiliko ya sheria yafanyike na majukumu ya kusimamia sekta ya vyakula na vipodozi kuhamia kwetu (TBS),ni marufuku mfanyabiashara kuingiza chakula au vipodozi visivyosajiliwa sokoni na hata majengo yanayofanya shughuli hizi lazima nayo yaangaliwe ikiwemo migahawa, magari yanayobebea vyakula, maduka ya vyakula na vipodozi,"alisema. 

Kabla ya mabadiliko hayo usimamizi wa chakula na vipodozi ulikuwa chini ya iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Yusuf Ngenya, (aliyevaa suti) akiangalia bidhaa mbalimbali za wazalishaji ambazo shirika hilo limezipatia vyeti na leseni ya kutumia alama ya ubora baada kuthibitishwa na kukidhi matakwa ya viwango. Hafla hiyo ilifanyika makao makuu ya shirika hilo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...