Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Emmanuel Tutuba (kulia) akipata maelezo ya Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka kwa Mtaalamu wa Huduma hizo wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Joseph Msumule (wa pili kushoto), alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa, Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu. Mtaalamu wa Mifumo ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Maendaenda (kulia) akitoa maelezo ya Mfumo wa Malipo ya Serikali (GePG) kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Emmanuel Tutuba, alipotembelea Banda la Wizara hiyo katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa, Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Benny Mwaipaja.

Watoto wakiwa wanasoma machapisho mbalimbali yanayohusu Mifumo ya Fedha, yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa, Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu. Furaha Alphad na Ilham Khalid (wa kanza na wa pili kulia) ambao ni wanafunzi wa Kidato cha Sita katika Shule ya Dutwa Mkoani Simiyu, wakisikiliza kwa makini maelezo kuhusu Sekta Fedha kutoka kwa Mtaalamu wa Huduma Ndogo za Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Joseph Msumule (wa pili kushoto) walipotembelea Banda la Wizara hiyo katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa, katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.

Wanafunzi wa Sekondari ya Kidinda Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu, wakisikiliza Maelezo Mtumishi wa Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA), Bi. Grace Masawe, kuhusu masuala mbalimbali ya Chuo zikiwemo sifa za kujiunga na Chuo hicho, katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa, katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu. Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Emmanuel Tutuba (kushoto), akizungumza jambo na watumishi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa, Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu. (Picha na Peter Haule, WFM)

*********************************

Na. Peter Haule, WFM, Simiyu

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Emmanuel Tutuba, ameishauri Wizara ya Fedha na Mipango na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuratibu kwa karibu vikundi vinavyotoa huduma ndogo za fedha vikiwemo VIKOBA ili kutoa elimu na ufahamu kabla ya mwananchi kujiunga au kukopeshwa fedha ili kuwa na uhakika na usalama wa fedha.

Rai hiyo imetolewa na Bw. Tutuba, alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango wakati wa Ufunguzi wa Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu.

“Kuna vikundi vinavyowaambia wananchi kuwa vinatoza riba ya asilimia tano, kumbe asilimia hiyo ni kwa mwezi na sio kwa mwaka ukifanya hesabu utagundua riba kwa mwaka ni asilimia 60 ilihali kuna benki zinazotoa mikopo kwa riba ya asilimia 18 kwa mwaka, hivyo lengo la huduma ndogo za fedha kumsaidia mwananchi kurahisisha shughuli za kiuchumi halifikiwi”, alieleza Bw. Tutuba.

Bw. Tutuba alisema kuwa, kuna vikundi wananchi wanaunganishwa bila kuwa na ufahamu wa kutosha hivyo kuchangishwa fedha lakini akienda kudai maslahi yake anaambiwa fedha hazipo, jambo ambalo taasisi zinazodhibiti vikundi hivyo zinabidi kufuatilia kwa karibu kwa kutoa elimu toshelevu ili mwananchi aweze kufanya maamuzi sahihi.

Pia alisema kuwa kwa ngazi ya Halmashauri anashauri fedha zinazotolewa kama mikopo kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Wlemavu, zitolewe kwa mfumo wa kibenki utakaosaidia ufuatiliaji na urejeshwaji wa mikopo hiyo kwa urahisi kwa kuwa na uelewa wa maana ya mikopo.

Alisema kuwa kuna vikundi ambavyo vinaanzishwa kwa mtazamo wa kutafuta fedha bila kuwa na wazo au biashara yenye tija kwa kikundi na eneo alipo hivyo dhana ya kuwakomboa wananchi kupitia mikopo hiyo kutofikiwa.

“Wale wanaokopeshwa wakipata fedha katika mifumo ya kibenki watapata elimu inayotakiwa, watarejesha fedha kwa uhakika, watafuatiliwa lakini hata dhamana sio lazima ziwe za ajabu zaidi ya muhtasari wa Kijiji kutambua biashara yake”, aliongeza Bw. Tutuba.

Alisema ikiwezekana ianzishwe Benki katika Serikali za Mitaa itakayosaidia kutoa fursa kwa watu kutoa wazo la mradia au biashara na litakapodhibitishwa lina tija katika uchumi wa Kijiji au Kata linaweza kudhaminiwa na Serikali ya Kijiji ili watu waweze kurejesha fedha.

Alifafanua kuwa Benki hiyo itawahudumia wananchi kwenye maeneo yao badala ya kuwaacha wananchi kwenda kurubuniwa kwenye vikundi vyenye dhamira ovu.

Kwa upande wake Mtaalamu wa Masuala ya Sekta Ndogo ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Joseph Msumule, alisema kuwa Sheria mpya ya huduma ndogo za fedha imeanzishwa ili kurahisisha utoaji wa huduma hiyo lakini kudhibiti wafanyabiashara wenye nia ovu kwa wananchi, pia sheria imeweka kiwango cha mtaji kwa wakopeshaji ili kusajiliwa, lengo likiwa ni kusaidia vikundi vya kuweka na kukopa kuwa na uwezo wa kutoa huduma wakati inahitajika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...