MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa upelelezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mtendaji Mkuu wa Bohari ya Dawa nchini ( MSD) Laurian Bwanakunu na mwenzake umefikia katika hali nzuri.
Taarifa hiyo ya upelelezi imefanya upande wa mashtaka kutaka kujua hali halisi ya upelelezi umefikia katika hatua gani kwani ni mara kwa mara upande wa mashtaka wamekuwa wakidai upelelezi uko katika hali nzuri.
Mapema leo Agosti 24, 2020, Wakili wa Serikali, Fatma Waziri alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Janeth Mtega kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi unaendelea kwani upo katika hatua nzuri.
Baada ya kueleza hayo Wakili wa utetezi Oscar Magolosa aliuomba upande wa mashtaka kueleze upelelezi umefikia hatua gani kwa sababu kila siku wamekuwa wakitoa kauli hiyo..."tunaomba tarehe ijayo upande wa mashtaka uje utueleze upelelezi umefikia hatua gani," amedai Magolosa.
Akijibu hoja hiyo, Wakili Waziri alisisitiza kuwa upelelezi uko katika hatua nzuri hivyo, aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.Hakimu Mtega ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 7, mwaka huu kwa kutajwa.
Mbali na Bwanakunu mshitakiwa mwengine ni Kaimu Mkurugenzi wa Lojistiki Byekwaso Tabura ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka matano ikiwemo kuisababishia MSD hasara ya zaidi ya Sh bilioni tatu.
Katika kesi ya msingi inadaiwa kati ya Julai Mosi, 2016 hadi Juni 30, mwaka 2019, washitakiwa hao wakiwa watumishi wa umma walitumia vibaya madaraka yao kwa kuendesha genge la uhalifu ili kujipatia faida.
Inadaiwa katika tarehe hizo wakiwa ofisi za MSD zilizopo Keko ,Wilaya ya Temeke Dar es Salaam, washitakiwa hao kwa vitendo vyao viou waliisababishia MSD hasara ya Sh 3, 816,727,112.75 .
Katika mashitaka mengine , mshitakiwa Bwanakunu anadaiwa katika tarehe hizo, akiwa mtumishi wa umma alitumia vibaya madaraka yake kwa kukiuka sheria ya utumishi wa umma kwa kuwalipa wafanyakazi wa MSD Sh. 3,816,727,112.75 kama nyongeza ya mshahara na posho ya pango la nyuma, bila kibali kutoka kwa Katibu Mkuu wa Utumishi wa umma.
Washitakiwa hao kwa pamoja, wanadaiwa kuwa katika tarehe hizo, kwa uzembe wa kutohifadhi vyema vifaa tiba na dawa na kufanya viharibike visitumike, na hivyo kuisababishia MSD hasara ya Sh 85, 199, 879.65.
Washitakiwa hao pia wanakabiliwa na mashitaka ya utakatishaji fedha kwamba, katika tarehe hizo, wote kwa pamoja walijipatia Sh 1,603,991,095.37 wakati wakijua fedha hizo zimetokana na kosa la kushiriki genge la uhalifu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...