VIJANA watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka saba yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu, kupanga mipango ya ugaidi pamoja na kukutwa sare za jeshi na kuzitumia isivyo halali.

Mengine ni, kukutwa na dawa za kulevya, kukutwa na silaha, kushiriki vikao vya kupanga mikakati ya ugaidi , kukutwa na vilipuzi.

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na jopo la mawakili wa serikali watatu wakiongozwa na wakili wa serikali Mkuu, Shadrack Kimaro, wakili wa serikali mwandamizi Wankyo Simon na wakili wa serikali Mwandamizi, Tulimanywa Majigo imewataja washtakiwa hao kuwa ni, Halfan Hassan, Adam Kasekwa maarufu kama Adamo na Mohamed  Lingwenya.

Akisoma hati ya mashtaka wakili Wankyo amedai, katika shtaka la kwanza la kuongoza genge la uhalifu, washtakiwa wote wanadaiwa kati ya Mei Mosi na Agosti Mosi 2020 katila hoteli ya Aishi iliyopo Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro na katika sehemu za Dar es Salaam,  Morogoro na Arusha washtakiwa pamoja na wengine ambao hawapo mahakamani kwa makusudi walitengeneza mpango wa kutengeneza mikakati ya kigaidi. 

Amedai kuwa walifanya hivyo kwa kutengeneza milipuko na kupanga kulipua vituo mbali mbali vya mafuta na mikutano ya madhara kwa lengo la kuharibu misingi ya kisiasa, katiba, uchumi na sifa ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania

Katika shtaka la pili inadaiwa kuwa siku na mahali hapo hapo washtakiwa wote kwa pamoja walishiriki vikao vya mikakati ya ugaidi huku wakijua kuwa kikao hicho ni muunganiko wa matukio ya ugaidi kwa kupanga kulipua vituo mbali mbali vya mafuta na mikutano ya madhara kwa lengo la kuharibu misingi ya kisiasa, katiba, uchumi na sifa ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika shtaka la tatu mshtakiwa Kasekwa anadaiwa Agosti 5, 2020 Katika eneo la Rau Madukani, wilayani Moshi mkoa wa Kilimanjaro alikutwa na dawa za kulevya aina ya Herione zenye uzito wa gramu 3.18.

Pia mshtakiwa Lingwenya anadaiwa siku na mahali hapo alikutwa na dawa za kulevya aina ya herione zenye uzito wa gramu 1.06.
Aidha mshtakiwa Kasekwa anadaiwa Agosti 5, 2020 huko huko katika eneo la Rau Madukani alikutwa na silaha aina ya pistol yenye namba A 5340 aina ya Luger bila ya kuwa na kibali.
Katika shtaka la sita mshtakiwa Kasekwa anadaiwa siku na mahali hapo alikutwa na vilipuzi ambavyo ni risasi tatu bila ya kuwa na leseni.

Katika shtaka la saba mshtakiwa Hassan anadaiwa Agosti 10, 2020 katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam,  kwa lengo la kuhatarisha usalama wa nchi alitumia sare za jeshi la wananchi JWTZ na Jeshi la kujenga Taifa  JKT ambazo ni suruali moja ya JKT, pamoja na suruali nne za JWTZ, fulana moja, Koti la mvua moja, jacket moja, kofia tano, overall tano, begi la kubebea vifaa vya JWTZ lijulikanalo kwa jina la ponjoo,  vyeo vinne vya koplo, mikanda minne, soksi pea moja,sweat, beji la mafunzo ya parachuti, kibuyu cha kunywea maji pamoja na kisu aina ya AK 47 CCCP. Vyote vya JWTZ.

Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ambazo kwa kawaida husikilizwa mahakama Kuu ama kwa kibali kutoka kwa DPP. 

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi hiyo itatajwa tena Septemba 2, mwaka huu washtakiwa wamerudishwa rumande. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...