Serikali kupitia Wizara ya
Afya – Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii imezindua miongozo saba yenye lengo la
kuimarisha huduma za Ustawi wa Jamii nchini.
Akizindua miongozo hiyo
jijini Dodoma Katibu Mkuu Wizara ya Afya – Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt.
John Jingu amesema moja ya jitihada za kuimarisha Huduma za Ustawi wa Jamii ni
kutengeneza miongozo hiyo ikiwa ni sehemu ya kuboresha huduma za ustawi nchini.
“Lengo letu kubwa ni huduma
za Ustawi wa Jamii ziendelee kuimarika siku hadi siku, utengenezaji wa miongozo
hii ni moja ya jitihada” amesema Jingu.
Ameongeza pia kuwa, Serikali
imefanya mambo mengi katika kuimarisha
huduma za Ustawi hususani kwa watoto, wazee, akina mama na wahanga wa ukatili
hivyo miongozo hiyo inaboresha zaidi huduma hizo kufanyika ikiwemo mwongozo wa kuwaelekeza
wanaotaka kuanzisha makazi salama, mwongozo wawakilishi wa watoto mahakamani
Pamoja na program za kijamii za marekebisho ya tabia kwa Watoto wanaokinzana na
sheria.
Miongozo mingine ni wa
kuwaunganisha Watoto na familia zao, mwongozo wa utambuzi wa huduma kwa Watoto
walio katika mazingira hatarishi, mwongozo wa uanzishaji wa makazi ya wazee na
wasiojiweza Pamoja na mwongozo wa majukumu ya Maafisa Ustawi wa Jamii katika
Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Awali akimkaribisha Katibu
Mkuu kuzindua miongozo hiyo, Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng’óndi
amesema kwa ujumla miongozo hiyo inalenga kuboresha, kuweka taratibu na vigezo
vya kutoa huduma za Ustawi kisayansi kwani katika utengenezaji wake umefanyika
utafiti mkubwa wa ndani na nje ya nchi.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Afya,
Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Rasheed Maftaha
amesema Halmashauri zinahitaji miongozo ili kuweza kutoa huduma kwa wananchi
kwa kuzingatia viwango.
“Tunaahidi miongozo hii
tutaisimamia ipasavyo inatekelezwa kama ilivyokusudiwa.” Alisema Maftaha.
Mwakilishi wa shirika la IOM
linalojihusisha na kuhifadhi wahanga wa ukatili na usafirishaji haramu Dkt. Qasim Sufi amesema miongozo hii ya Taifa inakwenda
sambamba na mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto
Pamoja na mpango wa kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu.
Inakusudia pia kusaidia
jitihada za Serikali katika kukuza uwezo wa kupanga, kutekeleza na kusimamia
mikakati na huduma katika kupambana na unyanyasaji wa wanawake na Watoto.
Wakati huo huo, Dkt. Jingu
amezindua muundo wa Utumishi wa kada ya Maafisa Ustawi wa Jamii wenye lengo la
kubainisha majukumu ya Maafisa Ustawi wa Jamii ili kuondoa mkanganyiko na kada
nyingine.
Muundo huo pia unalenga
kusaidia vyuo vinavyotoa taaluma ambazo ni muhimu katika fani za Ustawi wa
Jamii kuweza kuimarisha Mitaala yao ili kutambua ni watu gani wanahitajika
katika kada ya ustawi wa jamii, ikiwemo kuongeza sifa za watu wanaostahili
kuajiriwa kama Maafisa Ustawi wa Jamii.
Katibu
Mkuu Wizara ya Afya – Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu (wa tatu
kutoka kulia) akikata utepe katika moja ya miongozo saba kuashiria kuzindua
miongozo hiyo yenye lengo la kuimarisha huduma za Ustawi wa Jamii nchini.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya – Idara kuu ya
Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akionesha moja ya miongozo saba
iliyozinduliwa yenye lengo la kuimarisha huduma za ustawi wa Jamii nchini. Kulia
ni mwakilishi wa shirika la IOM Dkt. Qasim Sufi, Kushoto ni Kamishna wa Ustawi
wa Jamii Dkt. Naftali Ngóndi.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...