Leandra Gabriel, Michuzi TV
NOVEMBA Mwaka huu Marekani itafanya uchaguzi mkuu ambao wagombea wao wamevuta macho ya watu wengi zaidi, na hiyo ni kufuatia wagombea wa nafasi ya juu ya urais kutoka chama cha Democratic kinachowakilishwa na Joseph Robinette Biden Jr (Joe Biden) na chama cha Republican kinachowakilishwa na Donald Trump kurushiana maneno na vijembe ikiwa ni sehemu ya utetezi wa kiti hicho.
Joe Biden alikua makamu wa Rais wa 44 nchini Marekani, aliyehudumu nafasi hiyo na Rais wa awamu ya arobaini na nne wa nchi hiyo Barack Obama.
Joe alizaliwa Novemba 20,1942 huko Scranton, Pennsylvania alisoma katika chuo kikuu cha Delaware kabla ya kutunukiwa shahada ya sheria kutoka chuo cha Syracuse mwaka 1968.
Mwaka 2008 Biden alitangaza nia ya kugombea nafasi ya urais, haikuwa bahati kwake, chama cha Democratic kilimchagua Barack Obama kupeperusha bendera ya chama hicho na akamchagua Biden kuwa mgombea mweza.
Kabla ya kuingia kwenye siasa Biden alihudumu kama wakili na baadaye kuwa mwakilishi mdogo zaidi kuwahi kutokea nchini Marekani pia amekuwa seneta aliyehudumu kwa muda mrefu wa miaka 44 katika jimbo la Delaware.
Licha ya kushindwa katika mbio za urais mwaka 1988 na mwaka 2008, Aprili 25, 2019 Biden alitangaza nia ya kugombea urais wa Marekani kwa mwaka 2020 na baadaye Agosti 1, 2020 alimchagua Seneta wa Colifornia Bi. Kamala Harris (55) kuwa mgombea mweza katika uchaguzi mkuu utakofanyika Novemba mwaka huu.
Kamala Devi Harris alizaliwa Oktoba 20, 1964, amesomea uchumi na kuhitimu shahada ya uzamivu katika sheria mwaka 1989, alikuwa mwanasheria mkuu wa 32 wa Colifornia kuanzia mwaka 2011 hadi 2017 na Seneta anayewakilisha jimbo la Colifornia tangu mwaka 2017.
Kamala anaandika historia ya kuwa mwanamke mweusi mwenye mchanganyiko wa Marekani na Asia kugombea nafasi hiyo ya juu kabisa.
Katika sera zao Biden na mgombea mwenza Kamala Harris wamekuwa wakimwelezea Donald Trump kuwa ni mtu anayependa kulalamika na asiyefaa kuiongoza Marekani na hiyo ni pamoja kwa kuiacha Marekani katika hali mbaya kiuchumi, ajira, haki pamoja na kuiacha vibaya nchi hiyo wakati huu ambao dunia inapambana na janga la virusi vya Corona.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...