Charles James, Michuzi TV
TUMEANZA sasa! Ndiyo kauli iliyotolewa na mashabiki wa Soka mkoani Dodoma wakiongozwa na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde baada ya Timu ya Dodoma FC inayomilikiwa na Jiji la Dodoma kuanza kwa Ligi kwa ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Mwadui.
Mchezo huo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania bars umechezwa katika dimba la uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma huku goli la wenyeji likifungwa na kiungo mshambuliaji, Khamis Mcha 'Vialli'.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Mavunde ambaye ni mmoja wa mashabiki wakubwa wa timu hiyo amesema huo ni mwanzo mzuri kwao hasa ikizingatiwa kuwa kwa muda mrefu Dodoma ilikosa timu ya Ligi Kuu.
" Ni furaha kwetu kwa sababu wote tunafahamu Dodoma ilikua haina timu Ligi Kuu, sasa kitendo cha kupanda na kuanza Ligi kwa ushindi ni dalili kwamba timu yetu iko vizuri na tumedhamiria kufanya vizuri zaidi kwenye Michezo mingine ijayo.
Niwapongeze benchi la ufundi, wachezaji na zaidi mashabiki wetu ambao ni wananchi wa Dodoma kwa kujitokeza kwa wingi kuipa hamasa timu yao, niwaombe wazidi kujitokeza kwenye Michezo inayokuja kwa wingi huu huu," Amesema Mavunde.
Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Timu hiyo, Mbwana Makata amesema huu ni mwanzo mzuri kwa timu yake mapungufu yaliyopo atayafanyia kazi ili kufanya vizuri katika michezo inayokuja.
" Tunamshukuru Mungu kwa kuanza na ushindi, ni mchezo wetu wa kwanza wa Ligi kama Timu, bado kuna tension lakini naamini tutakaa sawa zaidi kwenye michezo inayokuja," Amesema Makata.
Mchezo huo pia umehudhuriwa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru na aliyekua Mkurugenzi wa Jiji hilo, Godwin Kunambi ambaye ameenda kugombea ubunge Jimbo la Mlimba mkoani Morogoro.
Wachezaji wa Timu ya Dodoma FC na Mwadui wakichuana kwenye mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu uliopigwa katika dimba la Jamhuri jijini Dodoma ambapo Dodoma FC imeibuka na ushindi wa goli 1-0.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia (wa pili kulia) akiwa ameongozana na mgombea Ubunge Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde (wa pili kushoto) wakiingia uwanja wa Jamhuri kuangalia mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu kati ya wenyeji Dodoma FC na Mwadui.
Mashabiki wa Soka mkoani Dodoma wakifuatilia mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu kati ya Dodoma FC na Mwadui katika uwanja wa Jamhuri.
Rais wa TFF, Wallace Karia akijadiliana jambo na Mgombea Ubunge Jimbo la Dodoma Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde (katikati) na Aliyekua Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi (kulia) walipokua wakifuatilia mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu kati ya Dodoma FC na Mwadui.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...