*Atumia nafasi hiyo kuelezea utaratibu wa vitambulisho vya wajasiriamali kuendelea, agusia upanuzi wa uwanja wa ndege Mbeya



Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Mbeya


NI maelfu ya wananchi Mbeya!Ndivyo unavyoweza kuelezea kutokana na idadi kubwa ya watu ambao wamejitokeza kwenye mkutano wa kampeni za mgombea urais wa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.John Magufuli ambaye ametumia nafasi hiyo kuwaambia anataka kuibadilisha Mbeya kwani anaipenda kutoka moyoni.


Akiwa mbele ya wananchi hao Dk.Magufuli ameeleza kwa kina mipango na mikakati iliyopo katika kuhakikisha mkoa huo unakuwa kitovu cha uchumi kwa mikoa ya nyanda za juu kusinini na katika kufanikisha hilo katika miaka mitano ijayo Serikali itaendelea kuujenga mkoa huo katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo na kiuchumi.


Dk.Magufuli amefafanua katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2020, imeeleza mambo ya maendeleo ambayo yatafanyika katika Mkoa huo lengo ikiwa ni kuhakikisha Mbeya inapiga hatua ya kimaendeleo na kusisitiza katika anataka Mbeya iwe yenye maendeleo.


"Ninasema haya kwasababu maendeelo hayana Chama na leo tumekuja tena na kwa maelekezo ya Chama changu kupitia Ilani ya kurasa 303, ninaelekezwa tunataka Mbeya liwe lango la uchumi kwa ukanda huu wa nyanda za juu kusini na kufanikiwa kwa hayo itatokana na wana Mbeya.


"Tuliyotekeleza kwa kipindi cha miaka mitano, ndugu zangu wa Mbeya na Watanzania mnaonisikiliza tumefanya mambo mengi makubwa, mojawapo kuimarisha huduma za jamii hasa elimu, afya na umeme na wagombea wenzangu wameeleza yale ambayo yamefanyika katika maeneo yao.Kwa Mbeya tumeimarisha huduma na kufanya upanuzi hospotali ya Kanda Mbeya kwa kujenga wodi ya wazazi, kununua vifaa tiba vya kisasa,"amesema Dk.Magufuli.


Amefafanua katika mkoa wa Mbeya katika kipindi cha miaka mitano wamejenga na kufanya ukarabati wa hospitali sita na kwamba Sh.bilioni 13.9 zimetumika kujenga vituo vya afya na zahanati wakati Sh.bilioni 3.53 zimetumika katika ununuzi wa dawa na vifaa tiba huku akisisitiza mafanikio makubwa yamepatikana, hivyo kupunguza vifo vya akina mama na watoto.Pia wamepunguza idadi ya watu wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi.


Dk.Magufuli amesema katika elimu nako kuna mambo makubwa yamefanyika nchini na kwa Mkoa wa Mbeya kwa ujumla. Amesema katika kipindi cha miaka mitano kuna shule za msingi zimejengwa, nyumba za walimu,madarasa, mabweni,upanuzi wa vyuo vikuu, ujenzi wa maktaba.Pia tumejenga jengo la utawala na taaluma katika Chuo kikuu Mzumbe kwa gharama ya zaidi ya Sh.bilioni tatu.Pia wamekiboresha Chuo cha Ualimu Tukuyu kwa Sh.milioni 628.2 na Chuo cha Ualimu wa awali Mpugusa wamekiboresha kwa Sh.bilioni 9.6


Kuhusu maji amesema katika kipindi cha miaka mitano kuna miradi ya maji imetekelezwa Mbeya ambapo kuna miradi mikubwa 52 ambayo imegharimu Sh. bilioni 22.5 ikiwemo mradi wa maji Shongo,Mbalizi,Makongorosi, Luduga hadi Mawindi.Kwa upande wa umeme amesema katika Mkoa wa Mbeya wamefikisha umeme katika vijiji 385 ambavyo vina umeme.


Dk.Magufuli amesema kuwa ukiachilia mbali uboreshaji huduma za jamii ambapo wamejitahidi kuimarisha miundimbinu na kwa msingi huo miaka mitano wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa miundombinu ya barabara na kwa Mbeya barabara za Sh.bilioni 252.36 zimetumika.


"Tumejenga kwa lami barabara zenye urefu wa kilometa 11.85 hapa Mbeya Mjini kupitia mradi wa kuendeleza miji kimkakati katika miji 28 ambapo jumla ya Sh.bilioni 799.52 zinatumika katika mradi huo. Sambamba nayo tumeimarisha bandari ya Itungi.


"Tumeimarisha usafiri katika Ziwa Nyasa, tumejenga meli mbili katika ziwa hilo.Tumenunua vichwa vipya vinne vya treni katika reli ya Tazara.Tumeleta Sh.bilioni 14.7 kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa Songwe Mbeya ambapo tutajenga jengo la abiria, kununua rada kubwa ili ndege ziwe zinatua wakat wote,"amesema Dk.Magufuli.


Akifafanua zaidi amesema katika kipindi cha miaka mitano wameendelea kuimarisha ulinzi wa rasilimali za nchi. "Nchi yetu imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi, hata hivyo madini yalikuwa yahatunufaishi lakini sasa yanaleta faida. Tumeanzisha wizara mahusisi ya madini , masoko , sheria ya madini.Hivyo imesaidia kuongeza mapato yanayotokana na madini.Tumefanikiwa kuongeza uzalishaji na mapato yameongezeka.


"Kwa hapa Mbeya mapato yameongezeka kutoka Sh.bilioni 1.03 mwaka 2015 hadi kufikia Sh.bilioni 42.75 kwa mwaka 2020, haya ni mafanikio makubwa.Pia hapa Mbeya kutoka 2015 haya ni mafanikio. Hapa Mbeya kuna wachimbaji wagodo zaidi ya 1,332, mafanikio mengine katika madini yamefafanuliwa katika Ilani ya CCM ambayo yamejieleza vizuri,"amesema.


Pamoja na hayo amesema wamejitahidi kushughulikia baadhi ya kero, ikiwemo migogoro ya ardhi kati ya wananchi na hifadhi na kwa Mbeya kuna vijiji 56 eneo la Mbarali ambavyo mgogoro ulikuwepo umepatiwa ufumbuzi.


"Changamoto nyingine ni kero iliyokuwa inawakabili wafanyabiashara ndogondogo, hivyo tukaamua kuanzisha vitambulisha vya wajasiriamali, na hata Mbeye tuliamua kuanzisha vitambulisho, unalipa Sh.20,000 unatumia mwaka mzima, lakini katika kutafuta kura kuna watu wanapenyeza maneno kuhusu vitambulisho hivyo lakini wafanyabiashara wanaelewa manyanyaso waliyokuwa wanayapata.


"Kwa hiyo kimsingi vitambulisho ni ukombozi kwa wajasiriamali, hivyo wanaobeza vitambulisho hivyo ni kuwabeza wajasiriamali ambao siku moja nao wanatakia kuwa matajiri wa nchi hii.Nakumbuka kulikuwa na mama mjane aliyekuwa anauza uji na alikuwa na mtoto anayemlipia karo, siku moja uji wao ulimwaga na mwingine kunywewa na mgambo, huo ndio ulikuwa mtaji wa mama na hivyo ukawa mwisho wa maisha yao na kwa uchungu yule mama aliamua kwenda kujinyonga.


"Hapa Mbeya watu walikuwa wanaufukuzwa kila siku, ndio maana tukasema watu wapewe vitambulisho vya Rais ambavyo atavitumia mwaka wote na mahali popote, vitambulisho hivi sasa mtu anaweza kwenda kukopa, maeneo kama Kigamboni watu wanakopa kwa vitambulisho hivyo, vinathaminiwa hata na watu wa bima za afya,"amesema na kusisitiza wakichaguliwa suala la vitambulisho litaendelea ili kulinda wajasiamali na kulinda shughuli zao.


Amesisitiza katika kipindi cha miaka mitano wamepanga kuimarisha huduma za jamii, afya , elimu na maji ambapo katika afya wataendelea kuimarisha hospitali za kanda.Amefafanua katika eneo hilo la huduma za afya wanataka watu kutoka nchi jiani waje kutibiwa hapa Mbeya.


Kwa upande wa elimu wataendelea kujenga miundombinu, watajenga shule 26 kwa kila Mkoa shule moja na shule hizo zitakuwa kwa ajili ya masomo ya sayansi. Pia shule 1500 zitaunganishwa kwa inatenti ili ziwe zinafundisha kwa mtandao."Tutaendelea kuimarisha shule za ufundi".


Pia ameelezea kuhusu ununuzi wa vinjwa saba vya treni na mabehewa 21 kwa reli ya Tazara, tutaendelea kujenga barabara za mfano ili liwe Mbeya liwe Jiji la kimataifa na kwamba watapanua uwanja wa ndege ili kuwa lango kuu la uchumi.Watanunua ndege na moja itakuwa ya mizigo ili marachichi yawe yanakwenda Ulaya na ndio maana mipango inaonesha ndege itakuwa inatua hapo.


"Wakati Profesa Mark Mwandosya anajenga huu uwanja wa ndege walimsema kuwa anapendelea kwao, nampongeza sana Mwandosya, uwanja huu ndio umekuwa mkombozi kwa ukanda huu, uwanja huu utakuwa kama wa Dar es Salam, utakuwa kama wa Kilimanjaro au kama wa Mwanza , ndege itatoka hapa kwenda moja kwa moja Ulaya.


"Kwa hiyo Mbeya mkae mkao wa kutengeneza pesa, tunataka watalii wanaokwenda Arusha tunaka wazidi wanaokuja Mbeya.Ndio maana uwanja huu tumeujenga na tumeweka Sh.bilioni 20 kuanza kuukarabati ili ndege ziwe zinatua hapa,"amesema Dk.Magufuli.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...