TAASISI
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilayani Kiteto Mkoani
Manyara, inamshikilia Daktari na mtaalamu wa dawa za usingizi kwa tuhuma
za kudaiwa kupokea rushwa ya shilingi 180,000 kutoka kwa mzee wa miaka
60 aliyekuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa tezi dume .
Mkuu
wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza mjini
Babati amesema watumishi hao wawili wa idara ya afya walitaka kiasi
hicho cha fedha kwa mzee huyo aliyekuwa anahitaji kufanyiwa upasuaji wa
tezi dume.
Makungu
amewataja watuhumiwa hao ni Dokta Martin John Kongora wa hospitali ya
wilaya ya Kiteto na mtaalamu wa dawa za usingizi wa hospitali hiyo
Fabiano Aweda.
Amesema
watuhumiwa hao walitenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha 15 cha
sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Amesema watuhumiwa hao waliomba rushwa hiyo licha ya mzee huyo kuwa na bima ya afya ya iCHF.
"TAKUKURU
Wilayani Kiteto ilipokea malalamiko hayo tukamueleza mlalamikaji
akawaombe wamfanyie upasuaji kwa kuwa ana bima ya afya lakini watuhumiwa
hao walikataa," amesema Makungu.
Amesema
watuhumiwa hao walimuambia mzee huyo endapo hatatoa fedha hizo
wataandika taarifa ili apelekwe hospitali ya rufaa ya Dodoma ambapo
gharama zitaongezeka za malazi na nauli.
Amesema
kwa kuzingatia Dokta Kongora alikuwa mtaalamu pekee na hali ya mgonjwa
ilikuwa mbaya walielekeza rushwa hiyo wapewe wataalamu hao wa afya
wakati ushahidi wa kuomba na kupokea rushwa ukiendelea kukusanywa.
"Tuliacha
wamfanyie upasuaji mgonjwa ambapo walifanya upasuaji huo kwa ufanisi na
vile vile tulisubiri pia mgonjwa apone na kuruhusiwa kutoka hospitali
ndipo tulimkamata," amesema Makungu.
Amesema
Takukuru mkoani Manyara inakemea kwa nguvu zote watumishi wachache wa
Wizara ya Afya wanaokiuka maadili ya taaluma yao na kujihusisha na
vitendo vya rushwa na wataendelea kuchukua hatua kali za kisheria kwa
watumishi wa aina hiyo.
"Ni
rai yetu kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa bila woga kwa kuwa sheria
ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007 ina vifungu
vinavyowalinda wanaotoa taarifa kwa nia njema," amesema Makungu.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...