Na Geofrey Kazaula
WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera umeendelea kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kwa kujenga barabara na vivuko katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

Mratibu wa TARURA Mkoa wa Kagera Mhandisi Avith Theodory alisema kuwa ujenzi wa Barabara ya Omukigando – Omukalinzi yenye urefu wa Km 6.5 imesaidia kutatua kero ya muda mrefu iliyokuwa inawakabili wananchi wa Kyerwa ambao walikuwa wanatumia mtumbwi kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine.

“Tunamshukuru Mtendaji Mkuu wa TARURA kwa kutoa maelekezo ya kutengeneza Barabara ya Omukalinzi - Omukigando ambayo imekuwa mkombozi kwa wananchi wa eneo hili kwani barabara hii imeweza kurahisisha huduma za kijamii kupatikana kwa urahisi”, alisema Mhandisi Avith Theodory.

Naye, Jamali Shabani Mkazi wa Kijiji cha Kagenyi alisema kuwa, ujenzi wa barabara hiyo ambayo ni njia ya mkato kutoka Nkwenda kwenda Nyakatuntu umeleta unafuu mkubwa sana kwa wananchi wa eneo hilo kwani wanasafirisha mazao yao kwa urahisi ikiwemo kahawa, ndizi, mahindi na maharage.

“Kipindi cha nyuma tulikuwa tunapata shida sana ya usafiri kutoka Nkwenda kwenda Nyakantuntu, tulikuwa tunazunguka umbali mrefu lakini uwepo wa barabara hii umeturahisishia kusafirisha mazao yetu na kufanya biashara zetu kufanyika sehemu kubwa, tunawashukuru sana TARURA pamoja na Serikali”, alisema Jamali Shabani.

Mbali na ujenzi wa barabara hiyo pia TARURA katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa imekamilisha ujenzi wa miradi ya Ahadi za Mhe Rais kwa kutekeleza ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa Km 2.5 katika Mji wa Nkwenda.

Wakala wa Barabara za Vjijini na Mijini (TARURA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera unahudumia Mtandao wa Barabara zenye urefu wa Km 900 na jitihada zinaendelea za uboreshaji wa huduma za usafiri na usafirishaji ili kuinua uchumi wa wananchi wa Wilaya hiyo.

Muonekano wa Barabara ya Omukigando–Omukalinzi kabla ya kujengwa na TARURA iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera ambapo wananchi walikuwa wanazunguka umbali mrefu kufika maeneo mbalimbali ikiwemo Nyakatuntu, Nkwenda na Omukalinzi.

Muonekano wa Barabara ya Omukigando-Omukalinzi yenye urefu wa Km 6.5 ikiwa imekamilika na kuanza kutumika katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...