Na Mwandishi wetu, Babati
WAGANGA
wawili wa kienyeji Luhanga Mabeshi na Hamis Gambona wamehukumiwa kwenda
jela miaka miwili na Mahakama ya Hakimu mkazi wa Babati kwa kosa la
kuomba rushwa ya shilingi 500,000 na kupokea shilingi 200,000 kutoka kwa
mganga wa jadi.
Hata
hivyo, mshtakiwa wa kwanza Mabeshi hakuwepo mahakamani hapo baada ya
kuruka dhamana ila anaendelea kutafutwa huku mshtakiwa wa pili Gambona
akipelekwa gereza la mkoa wa Manyara, Mrara ili akatumikie adhabu hiyo.
Hakimu
mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Babati Simon Kebello ametoa adhabu
hiyo jana kwenye kesi hiyo namba CC 2019 baada ya kuridhishwa na
ushahidi usiotia shaka uliotolewa na mwendesha mashtaka wa TAKUKURU
Evelyine Onditi.
Awali,
washtakiwa hao walifikishwa mahakamani kwa kosa la kuomba na kupokea
rushwa kwa mganga wa jadi wakidai kuwa wao ni wapelelezi kutoka umoja wa
waganga za jadi na tiba asili Tanzania (Uwawata).
Wakadai
kuwa kwa vyeo vyao wanakagua waganga wanaopiga ramli chonganishi hivyo
naye anahusika katika hilo awape rushwa ya shilingi 500,000 ili
wasimchukulie hatua kwa kosa hilo.
Amesema
kwa sababu mganga huyo hakuwa anajihusisha na ramli chonganishi alitoa
taarifa TAKUKURU na kisha kukamatwa kwa washtakiwa hao waliopokea rushwa
ya shilingi 200,000 na wakafikishwa mahakamani na kuhukumiwa baada ya
kutiwa hatiani.
Mkuu wa
TAKUKURU Mkoani Manyara Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa
habari mjini Babati ametoa rai kwa wananchi kutoa taarifa kwao pindi
wakimuona Mabeshi ili afikishwe gerezani akatumikie adhabu yake.
Makungu amesema Mabeshi hupendelea kutembelea maeneo ya Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha na Mkoa wa Shinyanga.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...