Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
SHIRIKA linalojishughulisha na kuzuia ajali Barabarani nchini (AMEND) limeendelea na jitihada zake za uboreshaji wa Miundombinu ya Barabara kwa kuboresha kivuko kwa Wanafunzi wa Shule ya Msingi Wailes iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika uzinduzi wa Kivuko hicho, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Victor Ayo amewapongeza AMEND kwa jitihada hizo za uboreshaji wa Miundombinu hiyo hususan kwa Shule za Msingi kwa Watoto wenye Mahitaji maalum.
Kamanda Ayo amesema ubunifu huo ni mkubwa baada ya kuona kivuko cha awali hakijakidhi vigezo, amesema Jeshi la Polisi litaendelea kuunga mkono jitihada za AMEND kuhakikisha Wanafunzi na Watu wenye mahitaji maalum kuwa na amani wanapovuka barabara.
Ametoa wito kwa madereva kutii sheria wanapofika katika Vivuko hivyo (Zebra Crossing) ili kuwapa nafasi Wanafunzi na Watu wenye mahitaji maalum kuvuka kwa amani pale wanapohitaji kuvuka katika maeneo hayo ya vivuko.
Pia Meneja Miradi kutoka AMEND, Simon Kalolo amesema wameshirikiana na Serikali upande wa TARURA, Ofisi ya Mkurugenzi na Jeshi la Polisi kuhakikisha Wanafunzi hao wa Wailes na Watu wenye mahitaji maalum wanapata kivuko hicho sambamba na kutoa elimu kwa Madereva kuwajibika ipasavyo kufuata sheria wanapofika katika vivuko husika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Usalama Barabarani Taifa, Kwa watu wenye Ulemavu, Ditram Kabatele amewapongeza AMEND kwa juhudi zao na kuwataka zoezi hilo kufanyika nchi nzima, amesema watawapa ushirikiano popote pale watakapohitaji. Amesema Vivuko hivyo vimepunguza idadi ya ajali kwa Wanafunzi na Watu wenye mahitaji maalum.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Wailes, Mwl. Jaribu Bakari amesema ujenzi wa Kivuko hicho utasaidia kwa kiasi kikubwa kwa Wanafunzi wa Shule hiyo kwa kuondoa adha ya kuvuka pale wanapoingia au kutoka maeneo ya Shule.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...