





CHUO Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam wakishirikiana na Kuehne Foundation wameeandaa mafunzo ya siku tatu kwa watu wenye Ulemavu wa wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.
Mafunzo hayo yamejumuisha watu wenye ulemavu wa Viungo, watu wenye Ualbino, watu wasioona pamoja na watu wenye uziwi wakiwa na mwalimu wa Lugha ya ishara ili wote wapate kile kilichokuwa kikifundishwa.
Mkuu wa Kampasi ya Dar es Saalam, Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Honest Ngowi akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo amesema kuwa lengo la ni kutoa mafunzo ya kiuongozi, rasilimali watu pamoja na namna ya kubuni miradi kwa viongozi wa shirikisho la watu wenye ulemavu (SHIVYAWATA) wa Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam ili waweze kujisimamia wenyewe katika shuguli zao.
Amesema kuwa mafunzo haya ni kulingana washiriki walivyoomba kupewa mafunzo na watoa mada wamejipanga, washiriki watapata kile wanachokihitaji kwani wao ndio waliopendekeza wanataka kujifunza nini na watoa maada wamejiandaa vyema kuwapa kile wanachokihitaji.
"Risala iliyotolewa hapa ni mpango mkakati wetu kati ya mambo mliyoyoyasema hapa ni mkakati wa kurudisha kwa jamii, tumepewa bure nasi tunatoa bure ikiwemo kutoa elimu kwa jamii, haya ni maeneo yetu ya kitaalamu, masuala ya kuandaa mpango mkakati, mpango mkakati wa fedha, mpango wa usimamizi wa fedha na usimamizi wa rasilimali watu, masuala ya ujasiriamali na masuala ya usimamizi wa biashara yote hayo ni maono yetu tutajitahidi kadili tunavyoweza tuweze kushirikishana." Amesema ngowi.
Amesema Chuo Kikuu Mzumbe ni kama vyuo vingine lakini Chuo hicho nilazima kurudisha kwa jamii kwani wanatoa mafunzo bila gharama yeyote kwa jamii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa shirikisho la watu wenye Ulemavu wilaya ya Ubungo (SHIVAWATA), Musa Geuza amesema kuwa shirikisho la watu wenye ulemavu halina Utaalamu wa kuongoza shirikisho ndio maana wakapata wazo la kuomba kwa Chuo Kikuu Mzumbe Kupata mafunzo ya utaalamu wa Kuongoza shirikisho hilo.
Hata Hivyo Geuza ameomba wasaidiwe kuwepo kwa mwongozo wa Fedha, rasilimali watu pamoja na uongozi ili waweze kusaidiwa katika uongozi wa kuongoza taasisi za walemavu.
"Baada ya haya mafunzo tunaomba mpange mipango ya kusaidia shirikisho la watu wenye Ulemavu Ubungo ili tuweze kujisimamia wenyewe katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika shirikisho letu."Amesema Geuza.
Hata hivyo Geuza amesema kuwa wanaomba kusaidiwa wataalaamu katika uandishi wa Miradi, tathmini ya mradi, Ufatiliaji wa mradi pamoja na Utekelezaji wa Miradi ili waweze kuwa na utaalamu ambao utaweza kuendeleza Shirikisho la SHIVYAWATA Ubungo.
Geuza amesema kuwa wao kama shirikisho la watu wenye Ulemavu Ubungo wamekuwa wakiendesha shughuli zao kienyeji, sasa wanataka kuanza kuendesha kiutalaam endapo watapata miongozo watakayo waandalia ili iwasaidie katika kuendesha shughuli zao zitakazo wasaidia kuwa sawa na taasisi nyingine.
Kwa Upande wake Mratibu wa Mafunzo, Dkt. Omary Swalehe amesema kuwa wataendelea kupokea maombi kwa vikundi mbalimbali wanaotaka kupata mafunzo.
Kwa Upande wake Katibu wa Shirikisho la watu wenye Ulemavu Wilaya ya Ubungo, Maria Ganji ameshukuru Uoongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuwapa mafunzo bila gharama yeyote .
Hata hivyo amesema kuwa amewaomba kuwa mafunzo hayo yasiwe mwisho yawe mwanzo kwani yatawasaidia katika Shirikisho lao kuweza kujiongoza wenyewe.
Mafunzo hayo kwa upande wa watu wenye Uziwi walikuwa na walimu wa ishara ambaye aliwawezesha kupata kile kilichokuwa kikitolewa na watoa mada huku akitafsiri maswali waliyokuwa wakiulizawashiriki wa mafunzo hayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...