Na Mary Gwera, Mahakama
JAJI Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma ameutaka Uongozi wa Chuo cha
Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto kuongeza wigo wa mafunzo kwa Watumishi wa
Mahakama kwenye eneo la Teknolojia hususani utoaji haki mtandao ‘e-judiciary,
e-justice.’
Akifungua
rasmi semina elekezi kwa Wajumbe wapya wa Baraza la saba (7) la Uongozi wa chuo
hicho, mapema Oktoba 07 katika Ukumbi wa Shule ya Sheria jijini Dar es Salaam, Jaji Mkuu amesema kuwa kwa kufanya hivyo, Chuo kitaisaidia Mahakama kutekeleza
azma yake ya kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia yanayoenda kwa kasi na
kufanya matumizi ya TEHAMA kuwa ni ya lazima na si hiyari.
“Karne
ya 21 imelazimisha mabadiliko mengi na makubwa yanayogusa nafasi ya Mahakama
katika utoaji haki, hususani ulazima wa matumizi ya TEHAMA kama nyenzo wezeshi
katika utoaji wa haki,” amesema Jaji Mkuu.
Jaji Prof. Juma ameongeza kuwa Mahakama ina utayari mkubwa juu ya matumizi ya
TEHAMA katika utoaji wa huduma zake, hivyo ni muhimu watumishi wake wakawa na
utayari na ujuzi wa matumizi lengo likiwa ni kuwafikishia wananchi huduma ya
utoaji haki kwa haraka zaidi.
Aidha, Jaji Mkuu amewaeleza Wajumbe hao kuwa ana imani kuwa Baraza la Uongozi wa
chuo hicho litaendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama ya Tanzania hususani
katika eneo la mafunzo ambayo ndio chachu ya mafanikio.
Kwa
upande mwingine, Jaji Mkuu amekipongeza chuo hicho kwa kuendesha mafunzo
kwa Maafisa mbalimbali wa Mahakama kuhusu namna bora ya kuendesha mashauri ya
uchaguzi. Ametaja Maafisa waliopatiwa mafunzo ambao ni pamoja na Majaji wa
Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Wasajili na Warajisi
kutoka Zanzibar, Mahakimu na wengineo.
Pia Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Uongozi wa Chuo, Mhe. Jaji
Dkt. Paul Kihwelo amesema kuwa lengo kuu la kuandaliwa kwa semina hiyo
kuwasaidia wajumbe wapya wa Baraza kukifahamu kwa kina chuo.
“Mafunzo
haya yameandaliwa ili kutoa nafasi kwa wajumbe wapya kuelewa kwa undani
uhusiano uliopo kati ya Mahakama ya Tanzania na Chuo, na matarajio ya
Mahakama kwa chuo pamoja na kuliwezesha Baraza kusimamia Menejimenti ya chuo
kwa umahiri na ufanisi mkubwa,” ameeleza Jaji Dkt. Kihwelo.
Katika
semina hiyo, Washiriki wamewezeshwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo majukumu
na wajibu wao, Mabaraza na Bodi za Taasisi za Umma kusimamia Menejimenti,
Sheria za fedha za umma yam waka 2001, Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011
pamoja na marekebisho ya kanuni zake.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...