MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.John Magufuli amefichua siri ya umuhimu wa Jiji la Dar es Salaam ambalo idadi ya watu kwa sasa imefikia milioni sita.
Dk.Magufuli ametoa siri hiyo leo mbele ya maelfu ya wananchi wa Jiji la Dar es Salaam ambao wamejitokeza kwenye mkutano wake wa kampeni za kuomba ridhaa kwa Watanzania ili achaguliwe tena kuongoza nchi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza umuhimu wa Jiji hilo katika kuleta maendeleo ya nchi.
Akifafanua kuwa Jiji la Dar es Salaam ni muhimu sana hapa nchini kwani ndilo Jiji lenye idadi kubwa ya watu kuliko maeneo yote nchini Tanzania."Kwa sasa Dar es Salaam kuna watu milioni sita na ifikapo mwaka 2030 litakuwa na watu milioni 10 na hivyo kulifanya kuwa miongoni mwa majiji manne barani Afrika".
Ameongeza mbali ya kuwa na idadi kubwa ya watu , Jiji la Dar es Salaam ni lango kuu la biashara hapa nchini kwani linatoa mchango mkubwa katika kuchangia pato la Taifa na maendeleo kwa ujumla na limekuwa likiongoza kwa uchangiaji mapato na hasa mapato ya kodi kwa asilimia 90.
Dk.Magufuli ametumia nafasi hiyo kutoa takwimu za mapato tangu mwaka 2015 hadi mwaka 2020 ambapo mwa mwaka 2015/2016 Dar es Salaam ilichangia mapato ya Sh. 11.9 sawa n asilimia 89.9, mwaka 2016/2017 ilichangia Sh.trilioni 12.6 sawa na asilimia 88.6 na mwaka 2017/2018 ilichangia Sh.trilioni 13.6 sawa na asilimia 89.
Amesema mwaka 2018/2019 Jiji la Dar es Salaam lilichangia mapato ya Sh.trilioni 13.9 sawa na silimia 88.7 na mwaka 2019/2020 limechangia Sh.trilioni 16.6 ambayo ni sawa na asilimia 89. 7."Kwa kipindi cha miaka mitano Jiji la Dar es Salaam limeendelea kuongoza katika pato la Taifa
"Ndugu zangu wana Dar es Salaam ndugu zangu wana Dar hili ni lango kuu la uchukuzi na lango lausafirishaji, sio hapa tu nchini bali na nchi nyingine zinatuzunguka, nchi yetu inapakana na nchi nane kati ya hizo nchi sita hazina bandari.Kwa kuzingatia hayo yote nilipokuja kuomba kura niliahidi mambo mengi lakini nitataja manne"amesema Dk.Magufuli wakati anazungumzia umuhimu wa Jiji hilo.
Amefafanua mwaka 2015 wakati anaomba ridha aliahidi kuimarisha ulinzi na usalama, kuimarisha miundombonu mbalimbali, kuboresha huduma za jamii ikiwemo afya, elimu maji na umeme pamoja na ahadi ya nne ilikuwa ni kuboresha mazingira ya biashara kwa ajili ya wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na Watanzania wote.
"Nashukuru kwa miaka mitano tumeweza kutekeleza ahadi hizo kwa vitendo, wagombea udiwani na wabunge wamekuwa wakieleza mambo ambayo yametekelezwa.Wakati tunaingia Dar es Salaam kulikuwa na vitendo vya ujambazi wa kutumia silaha.
"Waliokuwa wanakwenda benki hawakuwa na uhakika wa fedha zao kufika salama, hali hiyo imedhibitiwa na sio Dar es Salaam tu bali hata maeneo ya nje ya Jiji hilo yakiwemo ya Kibiti na Mkuranga ambako waliokuwa wanafanya vitendo hivyo Dar wanakwenda kujificha huko,"amesema.
Kuhusu ahadi ya miundombinu, Dk.Magufuli amesema wagombea ubunge wameeleza mambo mengi yamefanyika, barabara za lami zimejengwa katika mitaa ya Dar es Salaam na ukijumlisha barabara za lami ni zaidi ya kilometa 200 zimejengwa ambapo kiasi cha Sh.bilioni 660 zimetumika.
Pia amesema barabara nyingine bado zinaendelea kujengwa na fedha tayari zipo kufanikisha ujenzi huo huku akiamua kumjibu mmoja ya wagombea urais ambaye amekuwa akieleza barabara ya kutoka Kimara hadi Kibaha ni pana sana."Kwanza sio kweli kule Hoston nchini Marekani kuna barabara ina njia 26 lakini hata kama kwa mfano ingekuwa ni barabara yetu ni pana hakuna ubaya.
"Sio lazima ili kitu kizuri basi kiwepo Ulaya tu, mbona Mungu aliamua kutupa mtu wa kwanza hapa Tanzania, hakushangaa kitu, mbona tunao mlima mrefu hapa kwetu lakini wala hakushangaa, mbona madini ya Tanzanite yapo Tanzania tu na hata mti mrefu kuliko yote duniani uko hapa hapa kwetu,"amesema Dk.Magufuli.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...