*Afichua siri sababu za kumteua Gambo kuwa Mkuu wa mkoa, kumpitisha kugombea ubunge ...
Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Arusha
MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.John Magufuli ameahidi kuendelea kuleta maendeleo zaidi katika Mkoa wa Arusha kwani anawapenda huku akitumia nafasi hiyo kueleza hatua ambazo wamepanga kuchukua katika kutatua kero za wananchi wa mkoa huo.
Pamoja na kueleza miradi mbalimbali ya maendeleo iliyogharimu mabilioni ya fedha katika Mkoa huo wa Arusha kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, Dk.Magufuli ameweka wazi mbunge sahihi kwa Jimbo la Arusha Mjini ni Mrisho Gambo anayetokana na CCM na amefichua siri ya kwanini aliamua kumteua kuwa mkuu wa mkoa huo.
Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Arusha leo akiwa katika mkutano wa kampeni zake za kuomba kura kwa Watanzania wakiwemo wa mkoa huo ili kumpa tea ridhaa ya kuongoza nchi, Dk.Magufuli ametumia nafasi hiyo kuelezea hatua kwa hatua mambo ambayo yamefanyika na yale yanayokwenda kufanyika miaka mitano ijayo.
"Nitakapochaguliwa nitakuwa mtumishi wa wana Arusha wote bila kuwabaga kwa dini na kabila zao, namuomba Mungu anisaidie kwenye hili.Nianze kwa kumshukuru sana Mungu kwa kutujaalia afya njema na uhai kwa kutuwezesha kuwa hai.Nawashukuru wana Arusha , nashukuru Chama changu kuandaa mkutano huu.
"Arusha wamechoka kuchagua watu wa porojo, mnataka mabadiliko ya kweli, mwaka 2015 nilipokuja kuomba kura, niliwaomba kwa heshima kubwa, lengo langu lilikuwa kuwatumikia Watanzania.Wakati nakuja kuomba kura nilikuja nikiwa tayari nimeshafanya serikalini kwa miaka 20, hivyo nilikuwa nina uzoefu na utumishi, naamini mlinichagua kwa kura nyingi.
"Kwa wabunge wengi walikuwa wanatoka upinzani, nilijua mmenipa msalaba.Nilizunguka kunadi Ilani nikiamini nataka kuwatumikia, lakini mlinipa shida, nilikuwa najiuliza nipate conection katika mji huu wa Arusha ambao ni wa utalii.Ilibidi nianze kutafuta viongozi ndani ya Serikali ambao watanisaididia kutatua matatizo ya hapa.
"Nilimteua Mrisho Gambo awe Mkuu wa Mkoa wa Arusha, siwezi kusema mbele ya viongozi wa dini, siwezi kusimama hapa mbele yenu , siwezi kusimama hapa nikazungumza uongo mbele ya viongozi wangu wastaafu.Gambo ndio alikuwa ananieleza matatizo ya hapa.
"Nikamwambia nenda kafanye kazi kama Mkuu wa Mkoa lakini kama Mbunge wa Arusha, huu ni mji wa watanzania, Arusha wakati ni wa utalii, Wazungu wanakaa hapa. Arusha ni mji wa watu wanaojishughulisha, wanapenda maendeleo, wanapenda kutatuliwa kero zao, ndio maana nikamleta Gambo,"amesema Dk.Magufuli.
Ameongeza wananchi hao ni mashahidi , hata alivyokuwa anakwenda kutekeleza mradi ya maendeleo alikuwa anapambana, yey anataka kutekeleza mradi huku wengine wanapinga."Nakushukuru sana kwa kazi nzuri ambayo umeifanya hapa Arusha. Gambo sikumfukuza Ukuu wa Mkoa, wala aliyekuwa DC wa hapa, wasingekuwa na nia ya kugombea.
"DC wa hapa alienda kugombea Babati vijijini, usingeweza kuwa na Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya halafu unataka kwenda kugombea,ndio maana wakuu wa mkoa wote, wakuu wa wilaya wote ambao walikuwa wanakwenda kugombea niliwatengua, Gambo aliniomba anataka kugombea Arusha , nikamwambia nenda na nimekubariki. "Kuna watu wana simama majukwaani wanasema simpendi, ningekuwa simpendi ningerudisha jina lake hapa kugombea ubunge?Kama mnataka maendeleo ya kweli nileteeni Gambo aelete maendeleo.
"Arusha imetengenezwa mahali ambapo hakuna mito, Arusha kupata maji ni shida, tulipopata fedha miradi 1443 nchi nzima , mradi wa kwanza mkubwa ni ule wa kutoa maji Ziwa Victoria hadi Tabora uligharimu Sh.trilioni moja,"amesema Dk.Magufuli.
Amefafanua mrdi wa pili ambao ni mkubwa wa maji katika nchini ni wa Sh.bilioni 520 ambao umefanyika Arusha na aliyemsumbua hadi mradi huo umetekelezwa ni Gambo.Hivyo atashangaa kama wana Arusha kama malipo yao kwa Gambo ni kumnyima kura."Hata barabara ya njia nne ambayo hakuna aliyetegemea kama itajengwa Arusha kwa watu walioninyima kura.Ningeweza hata hii barabara tukaipeleka sehemu nyingine.
"Tumetumia Sh.bilioni 164 katika ujenzi wa barabara hiyo pamona na By pass , na hivi sasa hata taa zinawaka barabarani, division, sasa inataa hadi za barabarani , niliyekuwa namtuma ni huyu Mkuu wa Mkoa wa ArushaNawaomba ndugu zangu wa Arusha maendeleo hayana Chama na ndio maana nimeleta hizo Sh.bilioni 520 kwa ajili ya maji na mradi umefikia asilimia 60.
"Nataka mkandarasi na wale ambao mtakuwa mmewachagua Gambo, ikifika Deemba mwaka huu maji yaanze kutoka Arusha, kwa hiyo kwa maneno yangu ya leo na mimi bado ni Rais kandarasi afanye kazi usiku na mchana akabidhi huo mradi,"amesema na kuongeza Arusha imechelewa kwasababu wanatakiwa kuwa na watu wenye uchungu na watu wa hapo.
Hata hivyo amesema kuna watu wameanza kutumia kampeni za ukabila katika jimbo hilo la Arusha, hivyo amewaomba wasiweke mambo ya ukabila kwani haujengi huku akifafanua nchi ya Tanzania kuna makabila 21 lakini Baba wa Taifa alifanya kazi ya kuyaunganisha na kubaki kuwa wamoja.
"Hapa uwanja tumekuja wengi hivi lakini hatukuuliza makabila, kama kabila yangekuwa muhimu maana yake hata Mungu angekuwa na Malaika wa makabila mengi,"amesema Dk.Magufuli.
Akizungumza zaidi na wanachi hao, amesema anataka Arusha iwe ndio Calfonia ya Tanzania na hilo halishindikani."Ndio maana nimekuwa nikisisitiza amani, nashukuru viongozi wa dini wanahimiza amani, palipo na amani ndiko kuna maendeleo.
"Tunataka kuongeza watalalii wafike milioni 5, halafu vijana wanaweka mawe na matairi barabarani, hivyo wana Arusha nileteeni Mbunge wa CCM pamoja na madiwani ili wafanye kazi ya kuleta maendeleo na kutatua kero za hapa,"amesema.
Akizungumzia mambo ambayo yamefanyika kwa kipindi cha miaka mitano katika mkoa wa Arusha, amesema mengi yamefanyika katika sekta za afya, elimu, maji, miundombinu ya barabara, usafiri wa anga.Katika afya ametaja baadhi yaliyofanyika ni kununua kwa X-Ray ya kisasa katika Hospitali ya Mkoa , ujenzi wa hospitali nne za wilaya.
Amesema hospitali hizo zimejengwa Arusha Jiji, Karatu, Longido na Ngorongoro na kwamba miaka mitano ijayo wataendelea kujenga hospitali, vituo vya afya na zahanati.Amesema wamepanga kujenga jengo la huduma ya uchunguzi daraja la kwanza katika mkoa huu wa Arusha, kuajiri watumishi huku akisisitiza mkakati uliopo ni kutoa bima ya afya kwa watanzania wote milioni 60
"Sh.bilioni 25.9 zimetumika katika kuboresha miundombinu ya elimu ikiwemo ya uboreshaji wa shule kongwe.Tumepanga kuendelea kutoa elimubila malipo na tutaendelea kuboresha miundombinu ya elimu na kujenga shule.Kuhusu miradi ya maji kwa Arusha tumetekeleza miradi 96 iliyogharimu Sh,bilioni 161.6.
Hata hivyo ameeleza katika kuendelea kutatua kero ya maji Arusha mbali ya kuwepo kwa mradi wa maji wa Sh.bilioni 520 , kuna mkakati mwingine wa kuendelea kuwa na mradi mwingine wa maji ambao huo utakwenda kumaliza kabisa changamoto ya maji katika maeneo mbalimbali ambayo yamekuwa yakikosa huduma hiyo.
Akizungumzia umeme, amesema kwa Arusha wamepeleka umeme katika vijiji 257, vimebaki vijiji 136,hivyo amewahakikishia katika kipindi cha miaka mitano watapeleka umeme katika vijiji vyote vilivyobakia.Kwa upande wa barabara amesema Jiji la Arusha kilometa 37 zimetengenezwa kwa lami.Ujenzi huo ni sehemu ya mpango wa kuboresha majiji 10 nchini liwekimo Jiji la Arusha.
"Kuna mtu mmoja hapa Arusha anasema hizo barabara katengeneza yeye, ndio tatizo la watu kutosema ukweli, tumeanza barabara ya kilometa 20 kutoka Usa –Kijenge, tumefufua usafiri wa reli ya kutoka Dar , Tanga, Moshi Arusha, usafiri huo ulikufa kwa zaidi ya miaka 30.
"Tuliamua watu wa Arusha hawawezi kukaa kwenye mateso, reli hii ambayo tumeifufua inakwenda kupunguza gharama za kubea mizigo yenu kwenye miaka mitano ijayo tumepanga kuendelea kuboresha miundombinu ya usafiri.Pia tumepanga kujenga jengo la abiria uwanja wa ndege Arusha, tutanunua vichwa vya treni 30, mabehewa 800, tutanunua ndege tano na moja itakuwa ya mizigo.
"Tumepanga kupunguza bei ya mafuta na usafiri kwa wananchi wa Kilimanjaro, Arusha na Manyara, tumeanza upanuzi wa bandari ya Tanga ili mafuta yawe yanashushwa hapo na kuletwa katika mikoa hiyo, tumepanga kukuza sekta uchumi, kilimo,"amesema.
Amefafanua katika miaka mitano viwanda 4,870 vimejengwa,anaamini katika kipindi kingine cha miaka mitano viwanda vingi vitajengwa, hivyo amewaombwa Wataznania wenye uwezo wa kufungua viwanda wafungue kwani huu ndio wakati wa kutafuta fedha.
Ametumia nafasi hiyo kuwahakikisha wananchi wa Mkoa wa Arusha kwamba kipindi cha miaka mitano ijayo Serikli itashughulikia kero ambazo zimekuwa zikiwakabili kwa muda mrefu huku akielezea mchakato wa ujenzi wa stendi mpya ambapo tayari eneo limepatikana na fedha zipo. Amesisitiza walivyojipanga kuboresha maslahi ya wafanyakazi nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...