Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi( CCM) Dk.John Magufuli amehitimisha kwa kishindo kampeni zake katika Jiji la Dar es Salaam huku akitumia nafasi hiyo kutaja mambo matano muhimu yaliyoyachwa na muasisi wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Nyerere ambayo ameahidi kuyasimamia na kuyaendeleza kwa nguvu zake zote.
Akihutubia leo Oktoba 14 mwaka 2020 mbele ya maelfu ya wananchi wa majimbo ya Kinondoni, Kawe na maeneo mengine ya Jiji la Dar es Salaam, Dk.Magufuli amewashukuru wananchi kwa mapokezi makubwa ambayo wamemuonesha tangu alipoingia hadi anahitimisha kampeni na kwamba amebaki na deni ambalo atalipa kwa kuleta maendeleo.
"Nawashukuru wana Kawe, wana Kinondoni na Dar es Salaam kwa ujumla kwa mapokezi mazuri.Namaliza nikijua Dar ni babalao wa mambo yote,"amesema Dk.Magufuli mbele ya wananchi hao waliojitokeza kwa wingi kumsikiliza.
Hata hivyo amesema leo Oktoba 14 ambayo ni siku ya kumbukizi ya Mwalimu Nyerere ambayo huadhimishwa kwa kuzimwa Mwenge wa Uhuru lakini kutokana na janga la Corona mwaka huu hakukua na mbio za mwenge kwani haukukimbizwa.
"Nitamzungumzia Mwalimu Nyerere, Nata hivyo tunapaswa kumshukuru Mungu kwa Nyerere kuzaliwa Tanzania,alikuwa kiongozi mahiri shupavu,mwenye maono ya kweli kwa maslahi ya wananchi wake, alibeba maono ya Bara la Afrika ,alikuwa mwafika wa kweli,mtetesi wa wanyonge,alikuwa na mvuto ndani na nje ya nchi yetu.Mwalimu Nyerere alikuwa mkombozi Taifa letu pamoja na mataifa mengine kwani hadi anafariki alikuwa msuluhishi wa mgogoro katika nchi ya Burundi,"amesema.
Dk.Magufuli ametumia nafasi hiyo kutaja mambo matano ambayo atahakikisha anayasimamia kwa nguvu zake ambayo yalianzishwa na muasisi wa Taifa hili Mwalimu Nyerere.
Amesema jambo la kwaza ni Uhuru wa nchi ambapo amefafanua kwamba Baba wa Taifa aliongoza harakati za mapambano ya ukombozi na harakati zake zilianzia jijini Dar es Salaam kwa kushirkiana na wazee wengine.
"Mwaka 1961 baada ya kupata Uhuru, mwalimu Nyerere katika moja ya nukuu zake alisema kwamba uhuru tulioupata uwe wa kweli kwa kila mwananchi, walikubaliana kuwa na uhuru wa kweli sio uhuru wa bendera. Katika kudhihirisha maneno yake alikuwa tayari kuvunja uhusiano na mataifa ambyo yaliingilia uhuru wetu.
"Na viongozi wote ambao wamefuata badala yake wamesimama imara kulinda uhuru wa taifa letu.
Hata ilipoibuka Corona tulisimama imara kulinda uhuru wa watu wetu,"amesema Dk.Magufuli.
Jambo la pili ambalo ni amani na utulivu ambayo ni tunu kubwa ambayo tumeachiwa na baba wa Taifa."Baba wa Taifa ,alipigania amani ndani na njeya nchi yetu, baba wa taifa alipenda amani na utulivu.Kuna wagombea urais wako kwenye kampeni wanahubiri uvunjifu wa amani watu hao waogopwe kwani amani ikiharibika watakaoteketea ni watanzania na hasa wanawake na watoto.
Wakati jambo la tatu ni Umoja na mshikamano wa taifa hili ambapo Dk.Magufuli amefafanua Baba wa Taifa aliunganisha Taifa hili licha ya kuwa na makabila zaidi ya 121i , jambo hilo sio dogo ni kubwa sana,kuna nchi wana lugha mbili au tatu lakini wameshindwa kuuungana na kuwa taifa moja.
"Ukienda Mbeya utakuta Wachaga wapo na hawabaguliwi, ukienda Mwanza utakutana Wangoni wapo, ukienda Lindi na Mtwara nako utakutana na watu wa makabila mengine wakiendelea na shughuli zao.
"Na ndio maana hata wakuu wa mikoa ambao wapo katika mikoa mbalimbali ya nchi yetu sio wa makabila ya mikoa hiyo hata Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam sio Mzaramu,Mkuu wa mkoa wa Morogoro sio Mluguru wala Mkagulu. Hili ndio Taifa ambalo tumeachiwa na Baba wa Taifa letu,"amesema Dk.Magufuli na kuongeza Uchaguzi Mkuu mwaka huu unatoa fursa kwa Watanzania kuchagua umoja au kugawa watu kwa misingi ya ukanda na ukabila.
Jambo la nne ambalo Dk.Magufuli amesema ataendelea kulisimamia kwa nguvu zake zote ni tunu ya Muungano kwani muungano ni muhimu na kwamba Tanzania ndio nchi ambayo muungano wake haukotokana na ukoloni bali umetokana na mataifa mawili huru."Tanganyika na Zanzibar waliungana na kuunda Tanzania, Uchaguzi utatoa fursa kuchagua viongozi wa kuendeleza muungano au kuuvunja muungano.Ukiwa Bara utakuta Wapemba na ukiwa Zanzibar utawakuta wa watu kutoka Tanzania Bara.
"Zanzibar wanafikia watu milioni milioni 1.5 na huku bara wanakaribia watu milioni 60.Ni dhambi kubwa ya kuvunja muungano na haitashia hapo tutaendeelea kubaguana, hivyo nikachaguliwa nitaulinda Muungano kwa nguvu zote kwa kushirikiana na Dk.Hussein Mwinyi ambaye naamini na sina wasiwasi atakuwa Rais wa Zanzibar.
"Hata nchi za Ulaya ziungana,ndio maana kuna Umoja wa nchi za Ulaya, kuna Jumuiya ya Afrika Mashariki, tunajumuiya ya SADC, Muungano ni kitu muhimu, muungano wa kwanza ni Adam na Eva na inawezekana bila kuungana kwao tusingekuwa hapa,"amesema.
Wakati jambo la tano ambalo Baba wa Taifa alisimamia ni Kujitegemea kiuchumi, hivyo hatuna budi kutumia rasilimali zilizopo katika kuleta maendeleo." Baba wa Taifa katika dhana hiyo ya kujitegemea kiuchumi aliamua kuanzisha mashirika ya umma, alianzisha mashamba,"amesema.
Ametaja baadhi ya mashirika yaliyoanzishwa na Baba wa Taifa ni Shirika la Ndege la ATCL, Shirika la Reli Tanzania( TRC), Shirika la Madini la Taifa( STAMICO)Shirika la Nyumba la Taifa( NHC)pamoja na mashirika mengine mengi.
"Kwa kuzingatia hayo Serikali ya Awamu ya Tano imejitahidi kusimamia misingi ya baba wa taifa ya kujitegemea,ndio maana nilisimamia kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu, na katika kipindi cha miaka mitano nchi yetu haijawahi kuingia kwenye njaa, miradi mbalimbali ya kitaifa imefanyika,
"Baba wa Taifa alihimiza watu kulipa kodi na tumesimamia hilo, tumeziba mianya ya kupotea fedha za umma na hivyo kusababisha mapato kuongezeka.Fedha ambazo tumezikusanya zimetuwezesha kutekeleza miradi ya kimkakati ya maendeleo, tunajenga bwawa la Umeme la Nyerere.
"Tunajenga reli ya kisasa, tumejenga shule,tumejenga viwanja vya ndege, tumejenga hospitali za rufaa,kanda,mikoa, tumenunua vifaa tiba,tumeajiri watumishi wa afya,tumenunua ndege mpya 11, tumenunua meli na mambo mengine mengi ya maendeleo yamefanyika,"amesema Dk.Magufuli.
Ameweka wazi yamefanyika hayo yote kutokana na tunu ambazo zimeachwa na Baba wa Taifa na hivyo amesisitiza wananchi wasifanye makosa katikaa uchaguzi mwaka huu na kwamba Taifa hilo kwa sasa linakwenda mbele.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...