Na Said Mwishehe, Michuzi TV, Tanga

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya CCM, Dk.John Magufuli ametumia mkutano wake wa leo kuwalekeza wananchi wa Korogwe mkoani Tanga namna ya karatasi ya mfano ya mpiga kura inavyoonekana na kwa vipi wataweza kumpigia kura ashinde kwa kishindo.

Pia ameendelea kusisitiza umuhimu wa nchi kuendelea kuwa na amani, na kwamba nchi nyingi zimeingia katika mapigano kwasababu ya udini na ukabila, hivyo Watanzania wajiepushe na wagombea wanaotoa kauli za kuhatarisha amani ya nchi.

Akizungumza leo Oktoba 20, mwaka 2020 mbele ya wananchi hao ambao walijitokeza kwa wingi kumsikiliza akiomba ridhaa ya kuomba tena miaka mitano ya kuwatumikia katika kuwaletea maendeleo,Dk.Magufuli amesema zimebaki siku nane kufanyika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Amefafanua tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) imetoa mfano wa karatasi ya fomu ya kupigia kura na katika fomu hiyo inaonesha Chama Cha Mapinduzi ndio namba moja kwenye fomu na linaanza jina la Mgobea mwenza Samia Suluhu Hassan na linafuata jina la Dk.John Pombe Magufuli na mbele ya majina hayo kuna kiboksi cha kuweka alama ya tiki.

"Ukishachukua fomu hiyo utaona nimevaa miwani na kichwani nina kaupara, hivyo nenda katika kiboksi weka alama ya tiki, hakikisha hauvuki chini ya mstari na baada ya hapo chukua kura karatasi yako ya kura weka katika boksi.Usihangaike na wengine walipo katika fomu hiyo ya kupiga kura kwani hawatuhusu,"amesema.

Dk.Magufuli amesema siku ya kupiga kura itakuwa ni siku ya mapumziko kitaifa ili wananchi wakapige kura na kwamba baada ya kupiga kura warudi nyumbani kusubiri matokeo."Nawaomba watanzania wote wakiwemo wana Korogwe kuweka tiki kwa wagombea wa CCM kwenye karatasi ya kupiga kura".

Amesisitiza uchaguzi huo ndio wa kuamua kama wananchi wanataka maendeleo au wanataka blaa blaa, ni uchaguzi wa kuamua wanataka amani au wanataka kuandamana, ndio uchaguzi wa kuamua wanataka upendo au amani.Nawaomba wananchi mfahamu nchi yetu hivi sasa ni taifa kubwa, tumetoka nchi masikini na kuingia uchumi wa kati.

"Lazima mjitenge na propaganda chafu zenye lengo la kutugawa watanzania, ukiona wagombea wanatoa kauli za kuhamasisha uvunjifu wa amani maana yake wameshashindwa uchaguzi lakini wanasema wanakwenda barabarani.Wananchi wameamua watamchagua Magufuli halafu unawaambia wakaandamane,"amesema.

Pia amesema uchaguzi wa mwaka huu wapo wagombea urais 15 na wale ambao wanazungumzia chuki maana yake ni kuwa sio kwa maslahi ya taifa bali ni maslahi yao binafsi."Mufti wa Tanzania amesema hapa kuhusu udini, na mimi nataka kueleza ukweli mapigano mengi duniani yanatokana kutokana na udini na ukabila.

"Kuna vyama wana sera zao ambazo mmezisikia , wanataka kuwagawa watanzania kwa majimbo, tukienda kwenye muelekeo wa kugawana kwa majimbo tutakuwa tumepotea, hivyo nawaomba vijana ambao wengi wao hawataki kujifunza historia tulikotoka, kuna chama katika Ilani yao wanasema madini yote wataweka rehani,"amesema Dk.Magufuli.

Amewaomba wana Korogwe, Tanga na watanzania wote kutafakari na kuangalia Taifa letu limetoka wapi, na kwamba baba wa taifa alipatia Taifa hili uhuru bila kumwaga damu wakati mataifa mengine yamepata uhuru kwa kumwaga damu , ndio maana bendera zao zina rangi nyekundu na ya Tanzania haina.

Dk.Magufuli amesema Tanzania imepata uhuru kwa amani, na kwamba baba wa taifa aliongoza nchi na kisha akang'atukka kwa hiyari, na baadae wakaja viongozi wengine na sasa yuko yeye, maisha ya watanzania yameanza kuwa mazuri."Sisi tunaweza mnipe connection ,msinichanganyie, kwenye maziwa unaweka gongo, hainyweki, nileteeni wabunge hawa wa CCM".

Kuhusu Korogwe amesema wana bahati sana , kwani viongozi wengi ambao wapo katika Serikali yake wametoka katika Wilaya hiyo."Katibu Mkuu Kiongozi ametoka hapa, Mwenyekiti wa wazazi Tanzania nzima anatoka hapa, Sheikh Mkuu wa Tanzania anatoka hapa, Askofu wa Kanisa la Anglikana anatoka Korogwe, nasikia Katibu Mkuu Wizara ya Habari naye ni wa hapa".


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...