JUMUIYA ya Viongozi wanawake kutoka vyama mbalimbali vya siasa wamelaani tabia ya baadhi ya wanasiasa nchini kutoa lugha za vitisho na hivyo kutishia suala la uvunjifu wa amani wakati huu wa kampeni za lala salama kuelekea uchaguzi mkuu.

Aidha wamewataka watanzania kutumia haki yao ya kikatiba kwa kujitokeza kupiga kura kwa amani na utulivu ili kuliacha taifa salama kwa kuwa suala hilo ni la mpito linalotokea kila baada ya miaka mitano.

Wakizungumza katika mkutano maalumu kwa ajili ya uhamasishaji wa makundi mbalimbali kushiriki katika uchaguzi huo, Mratibu wa umoja huo Saumu Rashid alisema kumekuwepo na lugha za vitisho  zinazotolewa na baadhi ya viongozi,  jambo alilodai kuwa linaweza kuhatarisha amani iliyopo nchini.

Alisema kimsingi kauli kama hizo zinazojitokeza katika majukwaa ya kisiasa zinaweza kuvunja umoja wa watanzania uliodumu tangu uhuru na hivyo akawaomba watanzania kuwaepuka watu wa aina hiyo.

"Mara nyingi zinapotokea vurugu sisi wakina mama pamoja na watoto ndiyo waathirika wakubwa, hivyo tunaomba watanzania na kuacha kushabikia kauli zozote zinazotolewa na viongozi hao ambao kwetu tunaona kuwa hawalitakii mema taifa letu" alisema Saumu.

Alisema wao kama wanawake kutoka vyama mbalimbali  vya siasa wanao wajibu mkubwa wa kuhakikisha amani ya taifa hili inalindwa wakati wote hata baada ya uchaguzi mkuu kumalizika kwa kuwa jukumu la kufanya hivyo ni wajibu wa kila mtanzania.

Kwa upande wake Mratibu wa wanawake Taifa kutoka Chama cha UMD Mwajuma Noti, alisema suala la kuitunza amani ni jukumu la kila mtanzania na kusisitiza kuwa itikadi za vyama zisiwafanye watanzania kubaguana na badala yake washirikiane kuilinda. 

Alilitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linakuwa macho na wavunjifu wote wa amani na kuwachukulia hatua pale wanapokwenda kinyume na utaratibu ili kuilinda amani ya taifa hili ambalo tangu kuasisiwa kwake limekuwa muasisi mkubwa wa amani. 

Aidha aliipongeza Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) usimamizi mzuri wa mchakato mzima wa uchaguzi tangu kuanza kwake hadi sasa unapoelekea ukingoni kwa watanzania kujiandaa kuitumia haki yao ya kikatiba kupiga kura jumatano ya wiki ijayo.

 Mratibu wa Jaumuiya ya Viongozi wa VYama vya Siasa Wanawake (TWCP/ULINGO) ,Bi Saumu Rashid akizungumza mbele ya Waandishi wa habari (hawapo pichani),leo jijini Dar Es Salaam, kuhusu  kulaani tabia ya baadhi ya wanasiasa nchini kutoa lugha za vitisho na hivyo kutishia suala la uvunjifu wa amani wakati huu wa kampeni za lala salama kuelekea uchaguzi mkuu.

 Mjumbe wa Jukwaa (TWCP/ULINGO) ambaye pia ni mwakilishi wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Bi Mgeni Ottow Naye akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari leo jijini Dar,akielezea umuhimu wa Wanawake katika Uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28,2020 nchini ,kuwa wanawake ndio wasimamizi wa jamii hivyo ni wajibu wao kukemea viashiria vyote vya uvunjifu wa amani nchini,Wanasiasa wanatakiwa kutambua kuwa mshindi yeyote wa Uchaguzi huo, atatokana na chaguo la wananchi hivyo wasijihusishe katika njama zozote zenye dhamira ya kuhatarisha amani ya nchi. 

Baadhi ya Viongozi wa Meza kuu wakihamasisha kuimba nyimbo za mshikamano,utulivu na amani  ukumbini humo 




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...