Na Mwandishi wetu, Mirerani

MAMLAKA ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara,
imeazimia kuhakikisha barabara ya lami ya kuelekea mtaa wa Kairo
inawekewa madaraja madogo ili maji yapate upenyo mkubwa wa kupita na
kuepusha mafuriko wakati wa mvua.

Mwenyekiti wa mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani Adam Kobelo ameyasema
hayo katika kikao cha mamlaka ya mji huo. Kobelo amesema shughuli hiyo itafanyika kwa wakati huu ambapo hakuna mvua ili madhara ya mafuriko yasitokee tena pindi mvua kubwa zikinyesha.

Amesema alishazungumza na wakala wa barabara nchini mkoani
Manyara kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa madaraja hayo madogo ya
kupitisha maji.

Amesema wataalamu wa TANROADS mkoani Manyara walipita kwenye barabara hiyo na kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa barabara
hiyo.

"Sisi kama viongozi tulisimama kwenye nafasi yetu na kufanikisha
kuonana na viongozi wa TANROADS ili barabara hiyo ifanyiwe ukarabati,"
amesema Kobelo.

Awali, Mwenyekiti wa mtaa wa Kairo, Gadi Msuya ameeleza kuwa, kipindi cha
mafuriko wananchi wengi nyumba zao zilibomoka kutokana na barabara
hiyo kushindwa kupitisha maji kwa wingi.

Msuya amesema endapo suala hilo litapatiwa ufumbuzi itakuwa nafuu kwa
wananchi kwani kipindi cha mvua kikifika maji yatakuwa na sehemu ya
kupitia tofauti na awali.

Mwenyekiti wa mtaa wa Tanesco, Justin Abraham amesema kero hiyo
itafikia kikomo endapo utekelezaji wake unafanyika kwani wananchi
wengi wameathirika na mafuriko kutokana na maji kukosa sehemu ya
kupitia.

"Wananchi wa Mireani hawatatuelewa kama barabara hiyo haitawekwa
madaraja madogo yatakayoruhusu maji kupita kwa wingi hasa kipindi cha
mafuriko," amesema.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...