Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
IDADI kubwa ya Vijana wanaoishi maeneo mbalimbali kutoka Kata ya Mzimuni Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam wanatarajia kupata ajira mara tu baada ya uchaguzi Mkuu wa 2020 kumalizika na hiyo ni kufuatia ahadi iliyotolewa na mgombea wa kiti cha udiwani katika Kata hiyo.
Hayo yamesemwa na mgombea nafasi ya Udiwani kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mzimuni Manfred Lyoto wakati akizungumza katika kamnpeni zake katika Kata ya Mzimuni jijini jijini humo.
Amesema kuwa, suala la ajira kwa vijana wa Kata ya Mzimuni tayari lina mbadala wake na hiyo ni kutokana na matarajio kupitia makampuni mbalimbali yakiwemo ya kichina ambayo ameyashawishi ili yatoe ajira kwa vijana hao.
Amesema mbali na changamoto ya vijana kutokuwa na ajira lakini pia zipo changamoto mbalimbali ambazo wanamzimuni wamekuwa wakikumbana nazo na kuahidi kuwa ikiwa atapewa ridhaa ya kuongoza atahakikisha anazishughurikia kwa haraka.
"Lakini pia ninatambua kuwepo kwa changamoto nyingine kubwa ya baadhi ya barabara zetu kutopitika nipende kuahidi kwamba hili nalo nitalishughurikia pamoja na nyingine nyingi;"amesema Lyoto.
Aidha amewaomba wananchi kutokosea na kuchagua mtu wa chama kingine mbali na CCM na kusema kuwa iwapo watafanya hivyo basi wataendelea kulalamika kwa kutotatuliwa matatizo wanayokumbana nayo kwenye Kata hiyo.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...