Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof.Paramamgamba Kabudi akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo Pichani) Jijini Dar es Salaam,  kuhusu ujio wa Rais wa Jamhuri ya Malawi Dkt Lazarus Chakwera ambaye atakuwepo nchini kwa siku tatu.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubbakar Kunenge akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo Pichani) Jijini Dar es Salaam,  kuhusu ujio wa Rais wa Jamhuri ya Malawi Dkt Lazarus Chakwera ambaye atakuwepo nchini kwa siku tatu.

Na.Beatrice Sanga-Dar es Salaam

RAIS wa Jamhuri ya Malawi Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera anatarajia kutembelea nchini Tanzania ambapo atafanya ziara ya Kitaifa ya siku tatu, kuanzia tarehe 7 mpaka 9 Octoba, 2020, yenye lengo la kuimarisha uhusiano, ushirikiano na kuendelea kudumisha ujirani uliopo baina ya nchi hizi mbili.

Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera atapokelewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli katika uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere.

Dkt. Chakwera atatembelea bandari ya Dar es Salaam ili kujionea shughuli mbalimbali na uboreshaji wa miundombinu ya bandari hiyo lakini pia atatembelea kituo cha kuhifadhia mizigo cha Malawi (Malawi Cargo Center) ambacho kimekuwa alama muhimu ya ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi.

Dkt Chakwera akiwa na mwenyeji wake, Mhe. Rais John Pombe Magufuli wataweka jiwe la msingi katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Mbezi Mwisho ambapo hatua hiyo ni ishara ya ushirikiano na umoja katika uendelezaji wa miradi ya maendeleo.

Akizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari Mhe.  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi amesema uhusiano kati ya Tanzania na Malawi ni wa muda mrefu na unaendelea kuimarikasiku hadi siku ambapo Nchi hizi mbili zimeendelea kushirikiana katika nyanja za kisisasa, ulinzi na usalama, kiuchumi, kijamii na yale ya kikanda hususan ndani ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika ( SADC) na Umoja wa Afrika.

“ Nchi hizi mbili sio majirani tuu, lakini watu wanaoishi Tanzania na Malawi ni ndugu na ni watu wa jamii moja. Hivyo tutakuwa na ugeni mkubwa wa Rais wa Malawi kuanzia kesho” amesema Prof. Kabudi.

Aidha Prof.. Kabudi ameongeza kuwa nchi ya Malawi ni kati ya nchi zenye uwekezaji hapa nchini ambao umejikita katika sekta mbalimbali zikiwemo fedha,uzalishaji, usafirishaji, ujenzi, kilimo pamoja na mafuta.

Akizungumza katika mkutano huo mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge amewataka wananchi wa Jiji la Dar es Salaam wawe tayari kwa ajili ya ugeni huo mkubwa na wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kumpokea Rais huyo wa Malawi.

Hii inakuwa ni ziara rasmi ya kitaifa ya kwanza kwa Mhe. Rais Dkt Chakwera tangu aingie madarakani mwezi Juni, 2020. Kabla ya hapo, Dkt. Chakwera   alifanya ziara za kikazi za siku moja moja katika nchi za Zambia na Zimbabwe.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...