Na Mwandishi Wetu, Lindi
MGOMBEA Ubunge wa Mchinga kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM,)
Mwalimu Salma Kikwete, amesema safari ya upatikanaji wa maendeleo
katika jimbo hilo inaanza rasmi Oktoba 28, mwaka huu baada ya wapiga
kura kuwachagua wagombea wa chama hicho.
Akizungumza katika mikutano ya kampeni zake zilizofanyika kuanzia
Jumatano, juzi na jana kwenye vijiji vya Makumba, Muungano, Mchinga
Moja, Ruvu, Kitomanga na Kilangala ‘A’, Salma amesema
maendeleo yatapatikana kwa sababu jimbo hilo si masikini kwa kuwa lina
maeneo ya uzalishaji ikiwamo ardhi yenye rutuba, fukwe za bahari,
kilimo, utalii, uvuvi na mito inayotiririsha maji mwaka mzima ila
tatizo wananchi wa maeneo hayo wanashindwa kujipanga kutumia fursa
hizo.
“Mchinga sio masikini hata kidogo tatizo tunashindwa kutumia fursa
tulizopewa na Mungu, nimekuja kuleta mabadiliko ya maendeleo, sasa
vijana msiwe na mihemuko kwa sababu Oktoba 28, 2020 tunaianza rasmi
safari ya maendeleo kwa sababu jawabu la maendeleo mnalo nyinyi
wenyewe,” amesema Salma na kuongeza:
"Wanamchinga tunatakiwa kuchagua mafiga
matatu ambayo ni wagombea wote wa udiwani wa CCM, mbunge wa CCM na
Rais wa CCM kwa sababu kiongozi anaweza kutoka chama chochote lakini
kiongozi mzuri anatoka ndani ya CCM, chagueni mnyororo wa maendeleo
kwa faida ya Mchinga.
“Mkinielewa vizuri mtatoka katika biashara ya shilingi elfu tano,
mtapanda juu kwa sababu fursa zinapatikana, vijana wa bodaboda hapa
Nangaru tutawatengenezea mpango mzuri wakopeshwe pikipiki ndani ya
mwaka mmoja. Nani kama mama? Mimi ndio mama nataka niwabebe na sitaki
niwaache katika safari ya maendeleo. Nataka kondoo wangu
nitakaowachunga wawe hodari.” amesema.
Katika hatua nyingine, amesema moja ya kazi ya mbunge ni kusimamia
shughuli za maendeleo na akichaguliwa anakusudia kuliunganisha jimbo
hilo kwa kupigania ujenzi wa barabara zitakazopitika mwaka mzima
ikiwamo zinazopita kutoka katika maeneo ya Kibaoni, Matimba, Nangaru
na Milola.
Pia amesema maendeleo yataletwa katika jimbo hilo kwa kuboresha huduma
za jamii ikiwamo kusimamia huduma za afya kwa kusaidia ujenzi wa
zahanati na vituo vya afya pamoja na kujenga madarasa na maabara.
Amesema akichaguliwa kuwa mbunge amejipanga kuhakikisha atashirikiana
na watu mbalimbali kupata majawabu au ufumbuzi wa kutatua kero za
jimbo hilo.
“Tutashughulikia eneo la afya kwa sababu bila afya nzuri huwezi
kufanya shughuli yoyote ya maendeleo, nitazungumza na wahusika
serikalini watusaidie ujenzi wa zahanati, madarasa na maabara na
tutazisemea bungeni." ameeleza.
“Na yote haya sio kwamba nafanya propaganda kama wengine, ninayoahidi
nitayatekeleza mkinipa ridhaa ya uongozi wa miaka mitano, sifanyi au
sisemi bla bla, tunasema ukweli na yanawezekana, hayo yote niachieni
kwa sababu nataka kushughulikia kero za Mchinga kwa kuzipeleka kwa
wakubwa serikalini,” amesema Salma.
Kuhusu kilimo, amesema kwa Mchinga lazima kiwe cha kisasa baada ya
wakulima kuanza kutumia mbegu bora huku wafugaji nao wakitakiwa kufuga
kwa mbinu bora.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...