Na Muhidin Amri,
Tunduru
SERIKALI ya kijiji cha Makande kata ya Lukumbule wilayani Tunduru
kilichopo mpakani mwa Tanzania na nchi jirani ya Msumbuji,kimetoa ardhi
yenye ukubwa wa ekari 3,000 kwa ajili ya kuanzisha mradi mkubwa wa
kilimo cha zao la ufuta katika msimu wa 2021.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Silaju Said alisema, hapo awali eneo hilo
lilitengwa kwa ajili ya makazi ya jeshi la wananchi Tanzania, hata
hivyo serikali ya wilaya ikiongozwa na Mkuu wa wilaya Julius Mtatiro
wameona ni vizuri eneo hilo liwe sehemu ya mradi wa kilimo cha ufuta
kutokana na ardhi yake kuwa mzuri kwa kilimo.
Alisema, katika mradi huo makundi mbalimbali ikiwemo shule, muungano
wa vyama vya wakulima(Mviwata) yatapewa maeneo ambapo ameipongeza
serikali kwa uamuzi wake wa kuimarisha zao la ufuta ambalo ni la pili
kuwaingizia fedha nyingi wakulima wa wilaya ya Tunduru .
Alisema, wametoa eneo hilo kwa manufaa ya jamii na pia itasaidia wakazi
wa kijiji hicho na vijiji vya jirani kwenda kujifunza kilimo bora cha
ufuta pindi mradi utakapoanza na utafungua fursa kwa wakulima kupata
masoko na taasisi mbalimbali kwenda kuwekeza katika shamba hilo.
Baadhi ya wananchi wa Makande Adinan Kihosa na Tabia Ali wameshukuru
kupelekewa mradi wa kilimo cha ufuta kwani mbali kuwapatia kipato cha
uhakika,pia utasaidia kupata elimu ya kilimo cha kisasa ambacho
kitakwenda kumaliza suala la umaskini wa kipato katika familia zao.
Tabia Ali alisema, mbali ya mradi huo kuwa sehemu ya kujifunza kama
shamba darasa utakwenda kupunguza tatizo la vijana wengi kukaa vijiweni,
kwa sababu baadhi yao watapata shughuli mbalimbali za kuwaingizia
kipato.
Hata hivyo,ameiomba serikali kupitia Benki ya maendeleo ya kilimo ambayo
ndiyo itatoa fedha za mradi kuhakikisha inatoa fedha hizo mapema ili
wakulima na vikundi vitakavyoingizwa kenye mradi huo waweze kuwahi msimu
wa kilimo kwani tayari mvua za kwanza zimeshaanza kunyesha katika
maeneo mbalimbali ya wilaya ya Tunduru.
Kwa upande wake Afisa kilimo wa wilaya ya Tunduru Gallus Makwisa
alisema,mradi wa kilimo cha ufuta katika wilaya hiyo umelenga sana
vikundi vidogo vidogo ambavyo vitaungana pamoja na vitapata fedha kutoka
kwa chama kikuu cha ushirika TAMCU ambayo imebeba dhamana ya kusimamia
mradi huo.
Alisema, mradi wa kilimo cha ufuta umegawanyika katika meneo mawili
ambayo ni shamba la ushirika kijiji cha Pacha nne kata ya Namiungo
ambalo litachukua vyama vya msingi vya ushirika(Amcos) na pili ni shamba
la Makande ambalo litahusisha kwa vikundi maalum vilivyoonesha nia ya
kulima zao hilo.
Kwa mujibu wake, kwa kuanzia mradi huu utaanza kwa kilimo cha kutegemea
mvua ambapo hunyesha kuanzia katikati ya mwezi Novemba,hivyo hadi
kufikia mwishoni mwa mwezi Desemba inatakiwa mashamba yote yawe
yamelimwa ili mwishoni mwa mwezi Desemba kazi za kupanda zianze na
kukamilika katikati ya mwezi Januari kwa kuwa maeneo hayo yamezungukwa
na maji.
Alitaja mategemeo ya mradi ni kuleta tija kwa wana vikundi kujitegemea
kiuchumi kutokana na faida itakayopatikana kwenye mradi na kuacha
kutegemea chanzo kimoja cha mapato ambacho ni ushuru wa mazao,kuongezeka
uzalishaji wa ufuta,kutoa ajira kwa baadhi ya wana vikundi ambapo zaidi
ya watu 20,000 hususani vijana watapata ajira.
Alisema, kwa kuanzia chama kikuu cha Ushirika Tamcu ambacho ndiyo
wasimamizi wakuu wa mradi huo kimejipanga kuomba kwa makubaliano maalum
taasisi ya Magereza na vijana wa jeshi la akiba kufanya kazi katika
mashamba yote mawili.
Mwenyekiti wa kijiji cha Makande kata ya Lukumbule wilayani Tunduru Silaju Said aliyenyoosha mkono katikati akiwaonesha baadhi ya wataalam wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru Afisa kilimo anayeshughulikia mazao Gallus Makwisa wa kwanza kulia,afisa ushirika George Bisan wa pili kushoto na mjumbe wa chama kikuu cha ushirika Tamcu Ltd Zainabu Yassin.
Baadhi ya wananchi viongozi wa Serikali ya kijiji cha Makande na wataalam wa kilimo ba ushirika kutoka halmashauri ya wilaya Tunduru wakikagua eneo la shamba lililopangwa kutumika kwa ajili ya mradi wa kilimo cha ufuta katika msimu wa 2020/2021.
Picha na Muhidin Amri
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...