
Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
KATIKA kuadhimisha siku ya Kimataifa ya unawaji mikono Duniani, Shirika la Kimataifa la WaterAid Tanzania, limetoa msaada wa mashine mbili za kunawia mikono katika shule za Chanzige A na B zilizopo Kisarawe, mkoani Pwani zenye thamani ya shilingi milioni 19.
Pia Shirika hilo limetoa msaada wa lita 5000 za sabuni ya maji kwa ajili ya shule hizo huku wananchi wakisisitizwa kuwa suala la unawaji mikono ni muhimu na inapaswa kuwa tabia endelevu.
Mashine hizo zimetolewa leo Oktoba 15,2020 wakati wa maadhimisho ya siku ya unawaji mikono duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule vya Chanzige A na B zilizopo Kisarawe Mkoani Pwani.
Akizungumza, wakati wa sherehe za uzindua wa matumizi ya mashine hizo Katibu Tawala Wilaya ya kisarawe Mwanana Msumi, amesema msaada huo ni muhimu katika kukabiliana na magonjwa yatokanayo na uchafu na kwamba vifaa hivyo vitachangia uhamasishaji wa kunawa mikono kuanzia shuleni hadi nyumbani.
Akizungumzia kauli mbiu ya mwaka huu, ambayo ni 'Usafi wa Mikono kwa Kila Mtu ni Msingi wa Afya Bora'. amesema, kufanyika kwa maadhimisho na elimu iliyotolewa itasaidia jamii kujua umuhimu wa kunawa mikono katika kujikinga na magonjwa mbalimbali.
Aidha, ameishukuru WaterAid kwa msaada huo na kuongeza kuwa, unawaji mikono ni sehemu muhimu katika kukabiliana na magonjwa na ya milipuko.
"Niwaombe wazazi elimu ya namna bora ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni iliyotolewa tukaitumie ipasavyo, ni wajibu wetu kuhakikisha majumbani kwetu tunakuwa na maeneo ya kunawia mikono na sabuni, hii itatusaidia kuepukana na magonjwa ya mlipuko" amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la WaterAid nchini Anna Mzinga amesema msaada huo wametoa ukiwa ni uwekezaji wa kusaidia watoto kutambua umuhimu wa kunawa mikono na usafi kwa kutumia maji ili kuepukana na maradhi mbali mbali yakiwemo magonjwa ya mlipuko.
"Elimu ya kunawa ni muhimu sana katika kukabili maradhi ya kuambukiza kwani hata ugonjwa wa Corona tuliweza kupambana nalo kupitia unawaji wa mikono kwa kutumia maji tiririka na sabuni.
''Kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto siku hii tunaiadhimisha tukiwa tunasema, ukinawa mikono utaweza kulinda Taifa."amsema.
Pia, Kaimu Afisa Elimu Msingi Saleh Segumba ameishukuru WaterAid kwa msaada huo huku akieleza kuwa utawasaidia wanafunzi na jamii nzima kukabiliana na maradhi yatokanayo na uchafu.
Morongo Eliya, mwanafunzi wa darasa sita Nzige A amesema msaada huo ni mkubwa kwani wanafunzi wengi wamekuwa wakishirikiana vyakula mbalimbali bila kuzingatia unawaji mikono.
Siku ya unawaji mikono duniani ilianzishwa kwa lengo la kuongeza ufahamu kwa jamii kutambua umuhimu wa kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.
Katika hatua nyingine balozi wa shirika hilo na kampeni ya Nyumba ni Choo, Mrisho Mpoto, amekabidhi vyoo aina ya Sato 20 shuleni hapo na kuahidi kuwa vyoo hvingine 30 vitapelekwa baadae.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...