Jane Edward Michuzi TV,Arusha.
Zaidi ya vikundi 38 Wilayani Longido Mkoani Arusha, vimepatiwa mikopo ya zaidi ya shilingi milioni 150 kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido Jumaa Muhina amesema kuwa ,vikundi ambavyo vimepatiwa mikopo vimekidhi matakwa ya Halmashauri katika utoaji wa mikopo hiyo.
Ameongeza kuwa ,awali kiwango cha utoaji wa mikopo hiyo ulikuwa si wa kuridhisha lakini uwepo wa Serikali ya Awamu ya tano chini ya Rais Dr Joseph Magufuli ,halmashauri hiyo imekuwa ikipata fedha za miradi mbalimbali ikiwemo mikopo hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Longido ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika zoezi hilo la utoaji mikopo kwa wananchi hao Frank Mwaisumbe, amesema kuwa mikopo hiyo italeta chachu ya maendeleo katika Wilaya hiyo kama wanufaika wa mikopo hiyo wataitumia vizuri katika biashara pamoja na kuzalisha mifugo na kuleta tija.
Aidha amesema Serikali ya Wilaya hiyo imelenga kunufaisha Wanalongido katika kuleta maendeleo sanjari na kujikwamua kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja kwa kuzingatia wilaya hiyo imezungukwa na jamii ya kifugaji na wanawake ndiyo wahusika wakubwa wa kutunza familia zao.
Naye Bi Grace Mghasi ambaye ni afisa maendeleo ya Jamii amesema wanatarajia kutoa mikopo takribani Milioni 200 kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021zikitokana na bajeti ya Halmashauri hiyo.
Kwa upande wa wanufaika wa mikopo hiyo,Nalepo Laizer walisema kuwa mkopo huo utakuwa msaada mkubwa sana kwao kwani wataweza kuanzisha biashara mbalimbali na kuweza kuboresha shughuli na hatimaye kujikwamua kiuchumi.
Bi Grace Mghase akionyesha mfano wa hundi ya Milioni 150 iliyokabidhiwa kwa vikundi 38(Picha na Jane Edward, Arusha)
Mkurugenzi wa halmashauri ya Longido akizungumza na mmoja wa wanufaika wa Mikopo inayotolewa na halmashauri ya Longido (Picha na Jane Edward, Arusha)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...