Na Karama Kenyunko globu ya jamii
MAHAKAMA Kuu nchini, imeteketeza dawa za kulevya aina ya Heroine zenye uzito wa kilogramu 118.174, kilogramu 3.932 za cocaine na kilogramu 120 za bangi jijini Dar es Salaam kufuatia amri ya mahakama baada ya mashauri yake kumalizika.
Zoezi la uteketezwaji wa dawa hizo umefanyika leo Oktoba 12, 2020 katika kiwanda cha Twiga Cement kilichopo Wazo Tegeta, jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) Biswalo Mganga, Kamishna wa Ukaguzi na Sayansi Jinai wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Bertha Mamuya, mawakili wa kujitegemea na maofisa kutoka baraza la mazingira NEMC.
Akizungumza kabla ya zoezi la kuteketezwa kwa dawa hizo kuanza, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Edwin Kakolaki amesema vielelezo vyote vinavyopokelewa mahakamani na kutumika kama sehemu ya ushahidi na kupokelewa kama kielelezo pindi kesi zake zimeisha basi huteketezwa kwa amri ya mahakama
"Niwahakikishie Watanzania, vielelezo vinavyopokelewa mahakamani na kesi kumalizika vinateketezwa na zile tetesi za kwamba mashauri yake yakiisha huwa vinarudi mitaani sio za kweli, dawa hizi zinateketezwa kutokana na amri ya Mahakama baada ya kesi kufika mahakamani, kusikilizwa na kumalizika kisha kupokelewa kama kielelezo cha mahakama na baadae hutoa amri ya kuteketezwa", amesema Jaji Kakolaki.
Ameongeza kuwa, utaratibu wa zoezi zima la uteketezwaji wa dawa za kulevya lazima wawepo mashuhuda ili kushuhudia amri ya mahakama jambo ambalo kufanyika kwa uwazi ili watanzania wajue kesi inapoenda mahakamani na kumalizika lazima vielelezo viteketezwe kwa uwazi
Kwa upande wake DPP Mganga amesema dawa zinazoteketezwa leo ni kilogramu 118.174 za heroin, kilogramu 3.932 za cocaine na kilogramu 120 za bangi zilizotokana na kesi 15 zilizofikishwa mahakamani na kumalizika.
Amesema Oktoba, mwaka jana kilogramu 10.65 za cocaine na kilogramu 226.149 za heroin zillizotokana na kesi 17 ziliteketezwa ambapo katika kipindi cha miaka miwili, mwaka Jana na mwaka huu, jumla ya kilogramu 345.22 za heroin zimeteketezwa, kilogramu 14.5 za Cocaine na bangi kilogramu 120 zikihusisha kesi 32 kwa mkoa waaDar es Salaam pekee.
Aidha Mganga amesema, kesi iliyokuwa dawa za kulevya nyingi ni kesi ya uhujumu uchumi namba 14/2018 iliyowahusisha raia wa Iran 12 waliokutwa na kilo 111.02 ya dawa za kulevya aina ya Heroine ambayo imemalizila hivi karibuni na wawili wamehukumiwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.
Akielezea madhara yake Mganga amesema dawa za kulevya zina madhara makubwa kwa binadamu, zinachochea watu kufanya makosa na kushindwa kufanya shughuli halali, na ndio maana serikali inapambana ili nchi ibaki salama.
Naye Kamishna Bertha amesema uteketezaji wa dawa hizo ni wa utaalamu wa hali ya juu na hauna madhara kwa mtu.
Kamishna wa ukaguzi na Sayansi jinai wa Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na dawa za kulevya Bertha Mamuya akizungumza wakati wa zoezi hilo
Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini, Biswalo Mganga, Jaji wa Mahakama Kuu Edwin Kakolaki na Kamishna wa Ukaguzi na Sayansi Jinai wa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya, Bertha Mamuya, mawakili wa Serikali, mawakili wa kujitegemea, na Maofisa kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wakisoma namba za kesi zilizokwishamalizika na kukagua dawa za kulevya kabla ya kuanza kuzichoma.
Wafanyakazi wa kiwanda cha simenti cha Twiga kilichopo Tegeta jijini Dar es Salaam wakiteketeza dawa za kulevya.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...