MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu Mahakama ya Mafisadi imewahukumu mfanyabiashara Ayubu Kiboko na mke wake Pilly Mohammed Kiboko kutumikia kifungo cha miaka 20 gerezani kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na dawa za kulevya

Hukumu hiyo imesomwa leo Desemba 18, 2020  na Jaji Lilian Mashaka baada ya washtakiwa kutiwa hatiani kwa makosa ya kusafirisha gramu 251.25 za dawa za kulevya  aina ya heroin.Pia Mahakama imeamuru vielelezo ambavyo ni dawa za kulevya viteketezwe, huku vielelezo vingine (Mali- Magari)  ya washtakiwa yarudishwe kwa mshtakiwa wa Kwanza na Wapili (Kiboko na Mkewe).

Akisoma hukumu hiyo Jaji Lilian amesema upande wa mashtaka wameweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa washtakiwa wametenda kosa hilo.

 "Ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha kesi kwa mshtakiwa wa kwanza na wa pili, hivyo Mahakama inawatia hatiani kwa makosa mnayoshitakiwa nayo", amesema Jaji Lilian.

Amesema, kwa maoni yake utetezi uliotolewa na  washtakiwa, wote wawili uliunga mkono ushahidi wa Upande wa Mashtaka kutokana na kujichanganya kwa maelezo yao ya ushahidi na unaonyesha kwamba wote walikuwa wanajua kwamba kulikuwa na Dawa za kulevya katika stand ya viatu.

Hata hivyo kabla ya kusomwa kwa adhabu Jaji Mashaka aliuliza upande wa mashtaka kama walikuwa na lolote la kusema, ndipo wakili wa Serikali Constantine Kakula akadai kuwa hawana kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya washtakiwa ila wameiomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwao na kwa wengine wenye nia ya kutenda makosa kama hayo

Katika utetezi wao, mshtakiwa wa kwanza, Kiboko, ameiomba mahakama asipewe adhabu kali kwani hahusiki na biashara hiyo ya dawa za Kulevya na hilo ndio shtaka lake la kwanza toka amezaliwa na wala halifahamu

Naye mshtakiwa wa Pili, (mkewe Kiboko) ameiomba Mahakama impunguzie adhabu kwani yeye ni mzazi ana watoto watatu ambao  wanamtegemea kwenda kuwalea.

"Mshitakiwa wa Kwanza na Wapili mna makosa kama mlivyoshtikiwa na mna hatia kwa kukutwa na dawa za kulevya aina ya Heroin.Nikizingatia mitigation na sheria za dawa za Kulevya na nikizingatia tangu mlipokamatwa May 23, 2018 na muda wote mlikuwa gerezani na tunafahamu Dawa za Kulevya zina athari, ninawahukumu kutumikia kifungo cha miaka 20 jela na kama hamjaridhika mna haki ya kukata rufaa," amesema Jaji Lilian

Kwa upande wa Wakili wa Utetezi, Nehemiah Nkoko alisema kuwa "Ni shufaa yetu kwamba washtakiwa wote ni wazazi na wana watoto na toka walipokamatwa hadi leo wanajiendesha wenyewe mmoja ana umri wa miaka 14.

Mahakama pia izingatie kuwa hawana rekodi yoyote ya makosa ya jinai na walikuwa wanafanya shughuli zilizokuwa halali na hakuna ushahidi uliotolewa kuonyesha kuwa kipato chao kilitokana na biashara ya dawa za Kulevya,"
Jumla ya mashahidi sita na vielelezo 16 vya upande wa mashtaka vilifikishwa mahakamani hapo kama sehemu ya ushahidi wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 29/2018, Kiboko na mkewe wanadaiwa, Mei 23, 2018 eneo la Tegeta Nyuki Masaiti wilaya ya Kinondoni,  walisafirisha dawa za kuÄşevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 251.25.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...