MRADI wa Mwanamke Imara wenye lengo la kutetea na kulinda haki za wasichana na wanawake dhidi ya ukatili umezinduliwa leo jijini Dodoma ukihusisha Mikoa mitatu, Wilaya sita na vijiji 30 kwenye mikoa hiyo mitatu huku ukilenga kumkomboa pia mwanamke kiuchumi.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), Tike Mwambipile amesema mradi huo utahusisha Mkoa wa Mbeya na Wilaya zake za Mbarali na Rungwe, Mkoa wa  Kilimanjaro na Wilaya zake za Moshi na Rombo pamoja na Mkoa wa Njombe na Wilaya zake za Makete na Ludewa.

Tike amesema lengo kubwa la mradi huo ni kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na utafanywa katika maeneo makuu manne   ambayo ni kuangalia namna ambavyo mwanamke atapata haki kwa wakati, kumiliki mali kwa maana ya mirathi, kupinga ukatili wa kijinsia pamoja na kuwainua wanawake katika kupata nafasi za kiuongozi.

Amesema licha mradi huo kufanyika katika mikoa michache wanaamini bado italeta matokeo chanya nchi nzima katika kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa wanawake unaongezeka, kuongeza ulinzi dhidi ya ukatili wa kijinsia hasa katika kuzuia ukeketaji lakini pia kuviinua kiuchumi vikundi vya wasichana na wanawake.

" Kila Mkoa katika hiyo mitatu tutafanya kwenye Wilaya zake mbili na katika hizo Wilaya tutafanya katika kata tano kwahiyo ni mradi mkubwa ambao tunaamini utatufanya tumuone mwanamke wa kitanzania anaweza kuwa jasiri na kuwa imara.

Wengi wanaamini mkoa wa Mara ndio kuna ukatili sana lakini nataka niwahakikishie hii mikoa mitatu ukatili dhidi ya mwanamke umekithiri kwa kiwango kikubwa, mfano Mbeya mwanamke ndio analima lakini wakati wa mavuno mwanaume ndio ananufaika, Kilimanjaro huko bado kuna changamoto kubwa ya ukeketaji hivyo ni jukumu letu kufanya kazi pamoja kuondoa changamoto hizo," Amesema Tike.

Kwa upande wake Meneja wa  Mradi huo kutoka Tawla, Mary Richard amesema mradi huo umegharimu kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni Minne na unafanyika kwa ushirikiano wa asasi na mashirika mengine ikiwemo USAID, Tanlap, Kwieco na Wildaf huku akisema mchakato huo umefuata Sera zote za Nchi na za wadau wanaofanya nao kazi.

Kwa upande wake mmoja wa washiriki waliohudhuria uzinduzi huo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Michael Semindu ameipongeza Tawla kwa kuandaa mradi huo ambao amesema utakua msaada mkubwa katika Wilaya yake ambayo ni mnufaikaji wa mradi huo.

" Ni ukweli Wilaya yetu ya Mbarali una changamoto ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake, sisi kama serikali kuna jitihada mbalimbali tumekua tukichukua lakini kupitia mradi huu kwa ushirikiano na wenzetu hawa tunaenda kupiga hatua kubwa katika kukabiliana na changamoto hii," Amesema DAS Semindu.

Mkurugenzi Mtendaji wa TAWLA, Tike Mwambipile akizungumza na wandishi wa habari baada ya mradi wa Mwanamke Imara kuzinduliwa jijini Dodoma leo
Katibu Tawala Wilaya ya Mbarali ambaye ni mmoja wa washiriki ambao Wilaya zao zimeguswa na mradi huo akizungumzia mradi huo namna utakavyokua na msaada kwao.
Mratibu wa Mradi wa Mwanamke Imara kutoka Taasisi ya Tanlap, Mcherehi Machumbana akizungumzia ushiriki wa Tanlap katika mradi huo
Washiriki waliohudhuria uzinduzi wa Mradi wa Mwanamke Imara wakimsikiliza mmoja wa watoa mada wa Mradi huo, Mary Richard ambaye ni Meneja mradi huo kutoka TAWLA.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...