R-LABS Tanzania (Reconstruction Labs) ni shirika linalowajengea uwezo vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu ya maarifa ya kujitegemea kwa kuwafundisha stadi muhimu za maisha.

Tangu lilipoanzishwa mwaka 2013, shirika limejikita kuwafundisha vijana stadi muhimu kama vile ushonaji nguo, upambaji wa kumbi za sherehe na mikutano, ususi wa nywele, uselemara pamoja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Yusuph Ssesanga ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika hilo amesema wao wamejikita zaidi katika kuibua ubunifu katika ngazi ya chini kabisa na lengo lao ni kusaidia vijana kuweza kupata mtazamo wa kujiajiri wenyewe.

Akizungumza kuhusiana Ufadhili waliopata toka Serikalini kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Mkurugenzi wa miradi toka R-LABS Naomi Rousse alisema ”walipokea ruzuku ya shilingi Milioni 45 ambayo imewasaidia katika kukamilisha baadhi ya mambo ukiwemo mgahawa wa “Youth Cafe”ambao utatoa huduma ya chakula kwa wananchi mbalimbali waliopo mjini Iringa, hivyo kuiingizia taasisi fedha za kujiendesha huku ikitoa mafunzo kwa vijana watakaojiunga katika ukumbi uliopo ndani ya mghahawa huu.”

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi mkuu wa COSTECH na Meneja wa mfuko wa MTUSATE Bw.Ntufye Mwakigonja, amesema tayari wameviwezesha vituo vya ubunifu 15 vinavyopatikana mikoa tofautitofauti na miongoni mwao ni R_Labs-Iringa huku wakiwa na lengo la kuhakikisha kila Taasisi ya ubunifu inafika katika viwango vya juu katika kuwawezesha vijana kujiajili lakini zaidi sana kuleta mapinduzi katika teknolojia yatakayo saidia shughuli za kiuchumi na kuchangia katika pato la Taifa.
Mwakilishi wa Mkurugenzi mkuu wa COSTECH na Meneja wa mfuko wa MTUSATE Bw.Ntufye Mwakigonja akihutubia wahitimu na wageni waliofika katika maonesho ya wahitimu wa mafunzo ya shirika la R_labs Iringa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mh. Richard Kasesela ameipongeza Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na shilika la maendeleo la ya watu nchini Uingereza (HDIF) kwa kuona umuhimu wa kufadhili kituo hicho ambacho kinarudisha matumaini mapya kwa vijana na kutimiza ndoto zao, hayo ameyasema alipo tembelea maonesho ya bidhaa za wahitimu wa mafunzo yanayotolewa na kituo cha R-Labs ambayo yalifanyika katika viwanja vya ‘Iringa garden’ mjini Iringa

Pia Mkuu wa Wilaya alitumia nafasi hiyo kumwagiza afisa biashara wa manispaa ya Iringa Bw.Majaliwa Kasim kuhakikisha wanatoa nafasi kwa vijana wa R-Labs kila mwezi kuonesha na kuuza bidhaa zao

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mh. Richard Kasesela akiongozana na mwakilishi wa Mkurugenzi mkuu wa COSTECH na Meneja wa mfuko wa MTUSATE Bw.Ntufye Mwakigonja katika maonyesho ya bidhaa za wahitimu wa mafunzo ya R_Labs

Kutokana na mafunzo wanayoyapata R-Labs, takribani vijana 700 kwa sasa wanaweza kujiajiri kwa kuanzisha miradi inayotoa fursa ya ajira kwa vijana wenzao pia.

Sherehe hizo zimeambatana na ugawaji tuzo kwa vijana wanufaika wa mafunzo yanayotolewa na kituo cha R-Labs ambao wameweza kuanzisha kampuni zao na kuajiri vijana wengine.

haya yakiendelea kutolewa kwa taasisi mbalimbali nchini yataongeza ari ya ujasiriamali miongoni mwa vijana, lakini zaidi sana yatasaidia kupunguza wimbi la ujauzito katika umri mdogo na pia vijana wanaotumia madawa ya kulevya, pombe na bangi kupungua kwa kuwa yatatoa nafasi nzuri ya kuzitumia rasilimali zilizopo nchini katika kujiongezea kipato.

Kituo cha R-Labs kimerudisha matumaini kwa vijana waliokata tamaa ya maisha baada ya kushindwa kuendelea na masomo yao kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za ujauzito masomoni, kukosa karo ya shule au kufanya vibaya kwenye mitihani yao ya mwisho.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...