Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akisisitiza jambo
wakati wa kikao kazi cha kujadili hali ya utoaji huduma za afya nchini
ambacho kimewakutanisha Wakurugenzi wa Wizara pamoja na Taasisi zake
kilichofanyika kwenye ukumbi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini
Dodoma. 
Waziri wa Afya Dkt. Dorothy
Gwajima akiongea na viongozi wa wizara na taasisi zake kwenye kikao
kilichofanyika kwenye ukumbi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini
Dodoma(Picha zote na Wizara ya Afya) 
Wakurugenzi wa wizara ya afya
pamoja na taasisi zake wakiwa kwenye kikao kazi cha pamoja cha kujadili
hali ya utoaji huduma za afya nchini.Kikao hicho kimeongozwa na Waziri
wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima na Naibu wake Dkt.Godwin Mollel 
Baadhi ya Wakurugenzi wa Wizara
kutoka Taasisi za Wizara ya Afya wakifuatilia kwa makini neno kutoka
kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Dorothy Gwajima (hayupo kwenye picha) wakati wa kikao kazi cha kujadili
maendeleo ya Sekta ya Afya, kilichofanyika kwenye ukumbi wa hospitali ya
Benjamin Mkapa jijini Dodoma
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Godwin
Mollel akieleza jambo wakati wa kikao kazi cha kujadili hali ya utoaji
huduma za afya nchini ambacho kimewakutanisha Wakurugenzi wa Wizara
pamoja na Taasisi zake kilichofanyika kwenye ukumbi wa hospitali ya
Benjamin Mkapa jijini Dodoma.
***********************************
Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma.
Serikali kupitia Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto inatarajia kuanzisha mfumo
wa Tehama kufuatilia mnyororo mzima wa utoaji wa dawa kwenye vituo vya
kutolea huduma za afya vya umma vyote nchini.
Hayo yamesemwa leo na Dkt.
Dorothy Gwajima, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na
Watoto wakati wa kikao kazi cha kujadili hali ya utoaji huduma za afya
nchini ambacho kimewakutanisha Wakurugenzi wa Wizara pamoja na Taasisi
zake kilichofanyika kwenye ukumbi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini
Dodoma.
Dkt. Gwajima amesema kuwa, mfumo
huo utasaidia kufuatilia utoaji wa dawa unaofanywa na watoa huduma za
afya kwenye vituo vya umma , kwani Serikali haitaji upotevu wa dawa
kwenye vituo vyake.
“Tunataka mfumo huu uunganishe
vituo vyote pamoja na hospitali zote hadi za Taifa kwani huu ni
ulimwengu wa Tehama,hivyo kama kiongozi anatakiwa kuona kila kitu pale
alipo ili kuweza kurahisisha kutatua matatizo ya wananchi wetu na hivyo
tutadhibiti upotevu wa dawa kwani imekua ni changamoto kubwa na sio
kwamba dawa hamna”.Alisema Dkt. Gwajima.
Hata hivyo, Dkt. Gwajima
aliwakumbusha watoa huduma kutoa dawa kwa kufuata muongozo wa utoaji wa
dawa kwa kuandika jina la dawa na sio jina la kampuni kwani kwa kufanya
hivyo inasababisha kukosekana kwa dawa ilhali dawa zipo kwenye stoo.
Kwa upande mwingine, Dkt.
Gwajima, ameagiza kufufuliwa na kukanza vikao mara moja kwa kamati za
dawa kuanzia ngazi ya Taifa hadi Zahanati, ili kuweza kujadili dawa
zote zinazotumika kwenye vituo vyao jambo ambalo litasaidia kugundua
upotevu wa dawa kwenye vituo vya umma.
Naye, Naibu Waziri Dkt. Godwin
Mollel amesema kikao kazi hicho kitasaidia kujua changamoto na
kuzijadili kwa pamoja ili kuweza kuwasaidia wananchi kupata matibabu
bora na huduma zingine kwenye taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo kwa
urahisi.
Amesema kwa kipindi cha miaka
mitano iliyopita uwajibikaji na uadilifu umefanyika na hivyo nchi
kufanya mapinduzi makubwa kwa kutumia mapato ya ndani, Serikali inayo
uwezo wa kununua dawa,vifaa na vifaa tiba na kutoa matibabu kwa
wananchi kwa gharama nafuu na hivyo itawaondolea wananchi mzigo mkubwa
wa matibabu nchini.
Dkt. Mollel amewataka watumishi
kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu ili kuondoa matatizo yalipo, kwani
asilimia 75 ya matatizo hayo yanaweza kutatuliwa na wenyewe bila
kutegemea mtu mwingine, hivyo kuwataka kuongeza kasi ya utendaji kazi na
kutumia mapato vizuri ili kuweza kuboresha huduma za afya nchini na
kuiongezea mapato Serikali na kusiwepo upungufu wa dawa kwa kuweza
vipaumbele maeneo muhimu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...