SULEIMAN MSUYA, TUNDURU

USIMAMIZI Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ), katika Msitu wa Chihuruka Kijiji cha Sautimoja, Kata ya Namakambale Tarafa ya Nakapanya wilayani Tunduru mkoani Ruvuma umerejesha mfumo wa elimu kijijini hapo kuwa kama wa wakati wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Itakumbukwa wakati wa uongozi wa Hayati Nyerere elimu ilikuwa bure kwa asilimia 100 kuanzia elimu ya msingi jambo ambalo linatekelezwa Sautimoja kupitia USMJ chini ya ufadhili wa Shirika la Mpingo na Maendeleo (MCDI) na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori Duniani (WWF)

Akitoa taarifa ya namna kijiji kinanufaika na USMJ mbele ya waandishi wa habari waliopo katika ziara ya siku saba iliyoratibiwa na Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC), Mtendaji wa kijiji hicho Philemon Dastan amesema mafanikio ni mengi ila hili la elimu ni kubwa zaidi.

Dastan amesema msitu wa kijiji umefanikiwa kuingiza zaidi ya shilingi 118.5 kwa kuuza magogo, mbao na mianzi.

Amesema Msitu wa Chihuruka wenye ukimbwa hekta 21,969 umetengwa kwa ushirikiano kati ya Halmashauri ya Tunduru, MCDI na WWF mwaka 2014.

"Sisi msitu umeturejesha enzi za Mwalimu Nyerere katika elimu kwani tumuweza kuwanunulia wanafunzi kalamu, madaftari, chaki na kujenga darasa hali ambayo ilitokea wakati wa uongozi wa Nyerere.

Kupitia mfumo huo wa kuwapatia mahitaji muhimu wanafunzi ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 80 hadi 92 hivyo USMJ unapewa kipaumbele Sautimoja," amesema.

Mtendaji amesema motisha hiyo imesaidia mahudhurio kuongezeka jambo ambalo linasababisha dhana ya elimu bure kivitendo.

Aidha amesema shilingi milioni 118 zilizopatikana zimezesha kununua pikipiki mbili, kujenga ofisi ya kijiji kwa shilingi milioni 26, kununua thamani za ofisi, kufatua tofali za nyumba ya mtendaji, kununua vifaa vya doria na kulipa bima ya afya kwa wajumbe 17 wa kamati ya maliasili.

Aidha, amesema katika kuhakikisha wanavijiji wanazidi kunufaika na USMJ wanatarajia kukata bima  kaya zote 250.

"Kila kaya moja itagharimu kiasi cha shilingi 30,000 ambapo itawezesha watu sita kupata kadi za bima ya afya kwa wanakijiji 513,"amesema.

"Kama tunavyojua kwamba ugonjwa ni jambo la dharura hivyo kwa wananchi kupata kadi za CHF watakuwa na uhakika wa matibabu nyakati zote tumeona mafanikio kwa kaya zile wanazotoka wajumbe wa kamati ya maliasili na sasa tunaelekea kwa kijiji chote,"amesema.

Aidha amesema kijiji kina zaidi ya shilingi milioni 28 ambazo  zitatumika kujenga zahanati ya kijiji.

"Kadi tumepata lakini kazi kubwa  iliyopo ni kuhakikisha tunajenga zahanati yetu hapa kijijini ili kupunguza adha ya kwenda wilaya nyingine ya Nanyumbu kufuata huduma afya,"amesema.

Aidha, Dastan amesema pamoja na mafanikio waliyopata kuna changamoto ya mifugo kuingia msituni, kukosa soko la uhakika wa mazoa ya misitu kama mbao hivyo wameomba wafanyabishara kuja Sautimoja kununua mbao nzuri.

"Changamoto ya soko tunaendelea kuipigania ni imani yangu ujio wenu utatangaza fursa hii muhimu kuwa tuna mbao nzuri zinachanwa na mashine ya kisiasa," amesema.

Hadija Athuman Katibu wa Kamati ya Maliasili amesema awali mradi ulikuwa na changamoto ila kupatikana kwa mashine ya kuchakata mbao wameanza kunufaika.

Amesema USMJ imechochea usawa wa kijinsia jambo ambalo awali halikuwepo huku akiwasisitiza wakina mama kushiriki katika uhifadhi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Sautimoja, Said Juma amesema miaka sita ya mradi umerahisisha utendaji wenye kufuata misingi ya utawala bora.

"MCDI na WWF wamechochea uwazi, uwajibikaji na utawala bora na kijiji kimepata mafanikio makubwa ya maendeleo. Lakini pia ajira zimepatikana kwa kijiji chote kushiriki kwenye USMJ," amesema.

Juma amesema mafanikio ambayo yamepatikana kupitia miradi ya USMJ imeweza kuunganisha familia na sio kutenganisha.

Naye Shakila Bushiri amesema kuwa kimsingi wametambua umuhimu wa kutunza misitu kwa maslahi ya maendeleo ya  kikazi cha sasa na kijacho.

"Uhifadhi umetukomboa sisi wanawake wa Kijiji cha Sautimoja maana fedha zote zinazopatikana zinafanya shughuli za maendeleo  kwa mtu mmoja mmoja na Kijiji kwa ujumla," amesema.

Samson Remmy Kaimu Ofisa Misitu wilaya ya Tunduru amesema serikali ipo pamoja na vijiji vinavyotekeleza miradi ya USMJ kwa kuwa ina manufaa kwa wananchi, vijiji na nchi kwa ujumla.

Remmy amesema wanaomba wadau wote wa misitu kuendelea kuibua miradi chanya na wao watawaunga mkono  na kwamba watawapa ushirikiano.

Kaimu ofisa misitu huyo amesema hali ya uharibifu wa misitu katika vijiji visivyo na USMJ ni kubwa tofauti na ile vyenye USMJ na kuwataka wanavijiji kuhifadhi.

"Naomba Serikali kuungana na wadau wote wenye miradi ya USMJ kama FORVAC, MDCI, WWF, MJUMITA, TFCG na wengine huku akisisitiza elimu itolewe zaidi.
 
Marcel Mutunda ambaye ni Mratibu wa FORVAC) mkoa wa Ruvuma amesema program hiyo wamekuja nayo kuhakikisha misitu inakuwa salama lakini wananchi nao wanufaike kiuchumi, kijamii na maendeleo.

Mutunda amesema mradi huo ambao upo chini  ya Wizara ya Maliasili na Utalii, kupitia Idara ya Misitu na Nyuki kwa ufadhili wa serikali ya Finland umekuwa ni chachu ya maendeleo kwa jamii na hata kuwafanya wananchi kutambua thamani ya misitu.

Msimamizi na Mtaalam wa Misitu  FORVAC Alex Njahan amesema wamedhamiria kutoa elimu kwa kina ili thamani ya mazao ya misitu nchini ionekane kuanzia ngazi ya chini hadi juu.

Njahani amesema program hiyo inatekelezwa kwenye wilaya 12 za Songea, Mbinga, Nyasa, Namtumbo, Tunduru, Liwale, Ruangwa, Nachingwea, Handeni, Lindi, Mpwapwa na Kiteto.

Mratibu wa FORVAC Kitaifa, Emmanuel Msoffe amewataka waandishi wa habari nchini kutumia kalamu zao vizuri kuelezea kwa kina faida za USMJ ili wafanya maamuzi wapate uelewa.

Msoffe amesema dhana ya USMJ bado haijaeleweka kwa kina hasa kwa wafanya maamuzi hivyo ushahidi utakaonekana kupitia kalamu zao utawabadilisha.

"Mnapaswa kutumia nafasi yenu kuiambia jamii kuwa misitu sio kuhifadhi pekee bali inapaswa kutumika kuchochea mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na maendeleo kwa wanavijiji," amesema.

 

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...