Waziri
Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda akipata maelezo kutoka kwa Meneja
Mahusiano Tawi la Oysterbay, Witness Kileo kuhusu uwezeshaji unaofanywa
na Benki yetu kwa Wanawake kupitia CRDB Malkia wakati wa Mkutano Mkuu wa
Pili na Madirisha uliofanyika jumamosi hii katika Kituo cha Mikutano
cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Waziri
Mkuu Mstaafu Mheshimiwa Mizengo Pinda amepongeza jitihada zinazofanywa
na Benki ya CRDB katika kuwawezesha wanawake wajasiriamali nchini
kupitia huduma ya CRDB Malkia. Mheshimiwa Pinda ametoa pongezi hizo
wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Pili wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake
la MADIRISHA uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha
Julius Nyerere (JNICC) ambapo Benki ya CRDB ilikuwa ni mdhamini mkuu.
“Nimefurahishwa
kusikia hapa tayari mmeshafanya uwezeshaji wa zaidi ya shilingi bilioni
600 kwa wanawake wajasiriamali kupitia CRDB Malkia. Uwezeshaji huu
unaleta chachu ya wanawake wengi zaidi kushiriki katika shughuli za
Maendeleo katika taifa letu. Hongereni sana,” alitoa pongezi Mheshimiwa
Pinda.
Waziri
Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Pili
na Madirisha uliofanyika jumamosi hii katika Kituo
cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa
Pinda aliipongeza Benki hiyo pia kwa ushiriki wake katika makangamano
na semina mbalimbali za uwezeshaji akisema kwa kufanya hivyo kunasaidia
kufikisha elimu ya ujasirimali na masuala ya fedha kwa wanawake zaidi.
Tafiti zinaonyesha ni asilimia 60 tu ya Wanawake ndio waliofikiwa na
huduma za kifedha huku wengi wao wakiwa nyuma katika shughuli za
ujasiriamali kutokana na kukosa elimu.
“Leo
hii mmetoa elimu nzuri sana juu ya fursa za uwezeshaji zinazotolewa na
Benki hii. Niwapongeze lakini niwasihi mfikishe elimu hii kwa wanawake
wengi zaidi mjini na vijijini,” aliongezea Mheshimiwa Pinda.
Akizungumzia
kuhusiana na huduma za uwezeshaji kwa Wanawake zinazotolewa na Benki ya
CRDB, Mheshimiwa Pinda alipongeza hatua ya Benki hiyo kupunguza riba ya
mikopo inayotolewa kwa wanawake wajasiriamali kutoka asilimia 24 hadi
asilimia 14.
“..
Kupungua huku kwa riba na masharti mengine yaambatanayo kunatoa fursa
kwa Wanawake wengi zaidi kunufaika na CRDB Malkia,” alisema Mheshimiwa
Pinda huku akiwahamasisha Wanawake wote kujitokeza kwa wingi
kuchangamkia fursa hizo zinazotolewa na Benki yao ya CRDB.
Akiwasilisha
mada katika mkutano huo, Meneja Uwezeshaji Wanawake Benki ya CRDB,
Rehema Shambwe alisema huduma ya CRDB Malkia imelenga katika kumtambua,
kumpa nafasi na kumuwezesha mwanamke wa Kitanzania kufikia malengo yake
kupitia mikopo ya biashara na ujasiriamali, kujiwekea akiba kwa akaunti
ya Malkia na mafunzo ya uendeshaji biashara.
“Mpaka
kufikia mwishoni mwa mwezi June mwaka huu, Benki yetu tayari ilikuwa
imekwisha toa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 600 kwa wanawake
zaidi ya elfu 55,” alisema Rehema huku akibainisha kuwa zaidi ya
wanawake 30,000 tayari wameshajiunga na akaunti ya Malkia.
Rehema
alisema pamoja na mafanikio ambayo Benki ya CRDB imeyapata katika
kumuwezesha mwanamke, bado idadi ndogo ya wanawake wamekuwa wakijitokeza
kupata huduma kutokana na changamoto ya riba, masharti magumu ya
dhamana na kukosa uelewa wa huduma za kifedha.
“Tukiwa
Benki ya kizalendo inayothamini mchango wa wanawake katika maendeleo ya
taifa letu, tukasema ni vyema tukatafuta suluhisho la changamoto hizi
ili kuweza kumsaidia mwanamke kufankisha malengo yake zaidi,”
alisisitiza Rehema.
CRDB
Malkia sasa hivi inawawezesha wanawake kupata mikopo kwa riba ndogo ya
asilimia 14 kulinganisha na asilimia 24 iliyokuwa ikitozwa mwanzo huku
masharti ya upatikanaji wa mikopo yakirahisishwa kwa kiasi kikubwa.
“Kupungua
kwa riba kuna maana wanawake sasa wanaweza kukopa zaidi na kwa gharama
nafuu kulinganisha na mwanzo hivyo kusaidia kufanikisha malengo yao kwa
uharaka zaidi,” alisema Rehema.
Rehema
alibainisha kuwa kupitia CRDB Malkia, Benki ya CRDB pia imeanzisha
huduma ya Malkia Rafiki katika mitandao wake wa matawi ambao watakuwa
wanawasidia wanawake kupata huduma stahili kwa uharaka na elimu juu ya
huduma hizo ili kuwawezesha kufikia lengo.
Naye
Muanzilishi na Mwenyekiti wa Jukwaa la MADIRISHA, Fatma Kange
aliishukuru Benki ya CRDB kwa udhamini iliyoutoa kufanikisha Mkutano
Mkuu huo ambao kwa mara ya kwanza umeweza kuhudhuriwa na wanawake zaidi
1,000.
“..
Wanawake sasa tumepata Benki kimbilio na sehemu ya kuelezea mahitaji
yetu. Tuishukuru Benki ya CRDB kwa kutushika mkono na kwa kutuheshimisha
Wanawake kupitia CRDB Malkia,” alisema Fatma Kange huku Akitoa rai kwa
Wanawake wote kuchangamkia fursa zinazotolewa na Benki hiyo.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...