Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania, Waziri Kindamba kuhusu mtambo wa zamani wa kupiga simu kwenye chumba cha makumbusho cha Shirika hilo wakati wa ziara yake ya kutembelea Shirika hilo, Dar es Salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania, Waziri Kindamba akiambatana na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (katikati) na Naibu Waziri wake, Mhandisi Kundo A. Mathew (wa kwanza kulia) wakati wa ziara yake ya kutembelea Shirika hilo, Dar es salaam.
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo A. Mathew akisisitiza jambo kwa wafanyakazi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (hawapo pichani) wakati wa ziara ya Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Faustine Ndugulile (anayesikiliza) alipotembelea Shirika hilo, Dar es Salaam.


Kampuni za simu, wanaohujumu miundombinu waonywa 

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile ameamua kuwatolea uvuvi mashirika na taasisi zote ambazo zinadaiwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL)ambapo amesema hadi ifikapo Januari 31, mwaka 2021 wawe wamelipa madeni na iwapo hawatalipa wakatiwe huduma mara moja.

Aidha ametoa onyo kwa watu wote ambao wamekuwa wakihujumu miundombinu ya TTCL kwa kuiba miundombinu yake na kwamba watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria ikiwemo ya kushtakiwa kwa uhujumu uchumi huku akitoa salamu kwa kampuni za simu ambazo zimekuwa zikifanya mbinu chafu kuidhoofisha TTCL.

Amesema hayo leo Desemba 30,2020 baada ya kufanya ziara ya kutembelea shirika hilo ambapo alipata fursa ya kuzungumza na viongozi pamoja na wafanyakazi ambapo ametumia nafasi hiyo kuweka mikakati ya kuboresha huduma  ya mawasiliano ya sauti na data kwa taasisi za Serikali, sekta binafsi na wananchi ili kukuza uchumi na kuchangia pato la taifa.

Akizungunzia kuhusu madeni, Dkt. Ndugulile amesema kwamba zaidi ya taasisi 20 za Serikali zinadaiwa na TTCL huku akiweka wazi kutokana na madeni hayo shirika linadai Sh.bilioni 30, hivyo lazima zilipwe na watakaokaidi baada ya siku ambazo amezotoa wakatiwe huduma.

" Natoa muda hadi Januari 31 mwaka 2021 wadaiwa wote wanaodaiwa na TTCL lazima wawe wamelipwa, wale ambao watakaidi wakatiwe huduma .Haya ni maagizo na nataka yatekelezwe.Shirika hili linatoa huduma kwa mashirika na taasisi mbalimbali za umma na binafsi, lazima madeni hayo yalipwe,"amesema Dk.Ndugulile.

Aidha amesema anazo taarifa kuna baadhi ya kampuni za simu ambazo majina yake tayari anayo yamekuwa yakifanya mbinu chafu kwa lengo la kulikwamisha shirika hilo katika kutoa huduma ambapo ameyataka kuacha tabia hiyo mara moja."Kuna kampuni za simu zimekuwa zikifanya mbinu chafu kuikwamisha TTCL na kubwa ni kukwepa ushindani.Ninayo majina ya kampuni hizo, waache tabia hiyo,tutachukua hatua."

Wakati huo huo amesema amepata taarifa kuna tabia ya wizi wa miundombinu ya TTCL inayofanywa na baadhi ya watu.Amefafanua wapo watu wanaoiba nyaya za shaba za TTCL na kuuza kama chuma chakavu, hivyo amewataka kuacha mara moja kwani watahusishwa na uhujumu uchumi.

 Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba ametumia nafasi hiyo kueleza wamefurahishwa na ziara ya Waziri Ndugulile na wamepokea maagizo na maelekezo yote ambayo wamepewa kwa lengo la kuboresha utoaji huduma .

" Waziri amepata nafasi ya kuzungumza nasi, amezungumza mambo mengi ya msingi na yenye muelekeo wa kujenga, amehimiza watumishi kufanya kazi kwa bidii, nami nieleze tutafanya kazi kwa spidi kubwa tena ya kukimbia na wale ambao wanaona hawataweza kwenda na kasi hiyo ni vema wakaondoka mapema," amesema Kindamba na kuongeza ameshaambiwa na Dk.Ndugulile wakimbie hivyo kama kuna mwenye nyonga ambazo hazina uwezo wa kukimbia wakae kando.

Kuhusu wadaiwa sugu,amesema Waziri Ndugulile ameshatoa maelekezo na jukumi lao ni kuandika barua kwa wanaodaiwa walipe madeni ndani ya muda uliotolewa na wakishindwa yeye atakachokifanya ni kukata huduma." Na naomba niseme kazi yangu itakuwa ni Ka ... Ta.Baada ya hapo sitaki wanaodaiwa wanipigie simu."


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...