Katibu Mkuu
wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk.Leonard Akwilapo,
ameipongeza Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii(CSSC),kwa mchango wake
katika sekta ya elimu nchini huku akiahidi serikali kufanyia kazi maoni
yanayotolewa ikiwamo kupunguza kwa mitihani ya majaribio.
Akifungua
leo Mkutano wa mwaka cha Wakuu wa Shule za Sekondari na Msingi za
makanisa, Dk.Akwilapo, amesema suala la mitihani ya majaribio lina utata
na kudai kuwa ni mingi na wakati mwingine inaipa Wizara wakati mgumu
kuiratibu.
“Kuna wengine wanadhani elimu inapatikana kwa kuuliza
wanafunzi maswali mara kwa mara, ili ng’ombe anenepe ni kuhakikisha
amekula na si kumpima uzito asubuhi, mchana na jioni, kitu kizuri ni
kuimarisha ufundishaji,”amesema.
Ameongeza kuwa “Kuna dhana
nyingine imeongezeka hadi kuweka kambi kufanyishwa mitihani kila siku
hadi jumamosi,kuna mambo tumekemea na si sahihi kwamba ili mwanafunzi
afaulu ni kupigwa mitihani, majaribio hatuyakatai bali kila mara
inamchosha mtoto.”
Aidha, amesema nia ya serikali ni kutoleta
mgongano na wanaendelea na majadiliano na kutaka kuimarisha ufundishaji
na si kupewa mitihani kila siku.
Pia amezitaka shule kuzingatia maelekezo ya serikali katika kumkaririsha mwanafunzi darasa kwa kuwa suala hilo linalalamikiwa.
“Tunatambua
mchango wenu mnaoutoa nchini katika sekta ya elimu, hata hivyo baadhi
ya shule zisizo za serikali kama nyingine zipo kwenu au hazipo, ambazo
zinaenda kinyume na maelekezo ya serikali, niwakumbushe myazingatie
kukaririsha wanafunzi bila kuzingatia taratibu ni tatizo tunalokutana
nalo sana,”amesema.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume hiyo,
Peter Maduki, amesema la mkutano huo ni kuweka mikakati ya utoaji huduma
bora ya elimu na kuangalia kero zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi.
“Pia
tutajadili namna ya kuboresha huduma ya TEHAMA itatusaidia sana katika
kuboresha elimu na kupunguza gharama ya utoaji wa elimu na kuwapunguzia
mzigo wazazi,”amesema.
Ameomba Wizara kuangalia namna ya
kupunguza mitihani ya majaribio ambayo imeonekana kuendelea kuibuka
mbali na inayopaswa kufanyika kitaifa.
“Kunaendelea kuibuka
mitihani ya majaribio mara ya kikata, kiwilaya hali inayosababisha
mwingiliano wa mitihani na hii hata inashusha ubora wa mitihani tunaomba
umakini zaidi uwepo katika kuendesha mitihani,”amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya
Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC) Bw.Peter Maduki,akielezea jinsi
wanavyotoa elimu katika shule zao wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa wakuu
wa shule za Sekondari na Msingi za Makanisa yaliyo chini ya Kanisa
Katoliki na Jumuiya ya Kikristo Tanzania ambayo yanaratibiwa na Tume ya
Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC) iliyofanyika leo Januari 25,2021
jijini Dodoma.
Sehemu ya washiriki wakifatilia Hotuba ya Mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa wakuu wa shule za sekondari na Msingi za Makanisa yaliyo chini ya Kanisa Katoliki na Jumuiya ya Kikristo Tanzania ambayo yanaratibiwa na Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...