Na Munir Shemweta, WANMM LINDI
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
ameiagiza ofisi ya Ardhi mkoa wa Lindi kuhakikisha inatoa elimu kwa
wananchi wa mkoa huo ili waone umuhimu, faida na thamani ya kumiliki
ardhi kutokana na mkoa huo kuwa nyuma katika umilikishaji ardhi.
Dkt
Mabula alitoa agizo hilo tarehe 5 Januari 2021 mkoani Lindi wakati
akigawa hati za ardhi kwa wananchi wa kata za Mnazi Mmoja na Mingoyo
katika halmashauri ya Manispaa ya Lindi akiwa katika ziara ya kukagua
utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya
serikali kupitia kodi ya pango la ardhi mkoani humo.
Dkt Mabula
alisema, mkoa wa Lindi uko nyuma kwa wananchi wake kujitokeza
kumilikishwa maeneo ya ardhi wànayomiliki na kumbukumbu za mkoa
zinaonesha kuna jumla ya hati 7025 zilizotolewa kwa wamiliki wa ardhi
na kusisitiza kuwa idadi hiyo ni ndogo kwa kuwa wananchi wengi
hawajaamka na kuona thamani ya kumilikishwa.
"Ofisi ya Ardhi Mkoa
mkatoe elimu kwa wananchi umuhimu na faida za kuwa na umiliki wa ardhi,
maana hapa shida haiko katika kumilikishwa kwa hati za miaka 99 pekee
bali hata zile za kimila hivyo lazima mkatoe elimu hata kwa wale
wananchi walio vijijini ili wamilikishwe na kupatiwa hati watakayoitumia
kwa faida ya maendeleo" alisema Dkt Mabula.
Aliitaka Ofisi ya
Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Lindi kujipanga vizuri na kwenda
kwenye maeneo ya kata za mkoa huo kuwaelimisha wananchi faida za kuwa na
hati ya ardhi kwa kuwa tangu kuanzishwa ofisi hiyo miezi sita iliyopita
ni hati 367 pekee ndizo zilizotolewa idadi aliyoieleza kuwa ni ndogo
ukilinganisha na mikoa mingine.
Aliwaeleza wakazi wa kata za
Mnazi Mmoja na Mingoyo katika Manispaa ya Lindi kuwa, mkoa huo una
maeneo mengi mazuri ya uwekezaji na iwapo watazembea kumilikishwa kuna
hatari wakayauza kwa bei ya chini kwa kwa kisingizio cha kutopimwa au
kuhaulishwa.
"Mkizembea kumilikishwa maeneo yenu sasa na
kupatiwa hati, mtu akitaka kuwekeza mtampa kwa bei ya chini kwa
kisingizio cha kutopimwa na mwingine atalichukua na baadaye ataliuza kwa
bei kubwa kwa kuwa ulimuuzia likiwa halijapimwa" alisema Naibu Waziri
Dkt Mabula.
Aliwataka wananchi wa mkoa wa Lindi kujitokeza kupima
maeneo yao na kuchukua hati na kusisitiza kuwa hata kama maeneo hayo
hawayahitaji wanaweza kuyapima ili kuongeza thamani na baadaye
watakapotaka kuyauza wauze na kupata fedha za kutosha.
Aidha,
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwataka
Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakikisha wanasimamia ipasavyo
makusanyo ya kodi ya pango la ardhi kwa kuwa mapato ya kodi hiyo ndiyo
yanayotumika katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Kwa
mujibu wa Dkt Mabula, idara ya ardhi ikisimamiwa vizuri na Wakurugenzi
wa Halmashauri wakiiwezesha kwa kuipatia vitendea kazi na bajeti ya
kutosha basi inaweza kuingiza mapato mengi kuliko sekta nyingine yoyote
kwa kuwa ardhi ndiyo kila kitu.
Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa
wa Lindi Said Kijiji alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula kuwa
pamoja na jitihada zinazofanywa na ofisi yake kuhakikisha maeneo mengi
ya mkoa huo yanapimwa lakini mwamko wa wananchi ni mdogo.
Alisema,
ofisi yake ilishatembelea halmashauri za mkoa huo na kuonana na
wakurugenzi kwa lengo la kuendesha zoezi la kupima na kumilikisha
maeneo ambapo alisema mafanikio makubwa yalikuwa katika halmashauri ya
Mtama.
Kwa upande wao wananchi wa Kata ya Mingoyo Manispaa ya
Lindi Zakaria Michael Mwanga na Hadija Rashid Magaya waliokabidhiwa Hati
ya pamoja walikuwa na haya ya kusema.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi (Katikati), Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Rehema Madenge (Kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga wakiwa katika picha na wamiliki wa Hati ya Pamoja Zakaria Michael Mwanga na mke wake Hadija Rashid Makaya baada ya kukabidhiwa hati akiwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi pamoja na kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali mkoani Lindi tarehe 5 Januari 2021.

Sehemu
ya wananchi wa Kata za Mnazi Mmoja na Mingoyo katika Mkoa wa Lindi
wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt
Angeline Mabula (hayuko pichani) alipokwenda kugawa hati akiwa katika
ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha
ukusanyaji kodi ya pango la ardhi katika mkoa wa Lindi tarehe 5 Januari
2021.
Watendaji wa sekta ya ardhi na viongozi wengine wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (Hayuko pichani) wakati wa ziara yake katika mikoa wa Lindi kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi tarehe 5 Januari 2021.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...