MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeamuru wafuasi watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukamatwa baada ya kushindwa kufika mahakamani bila kutoa taarifa yoyote.
Washitakiwa wanaotakiwa kukamatwa ni pamoja na; Edgar Adelini, Reginald Massawe na Pendo Raphael.
Uamuzi huo umetolewa leo Januari 19 2021 na Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi wakati kesi inayowakabili ya kukaidi amri ya jeshi la magereza iliyowataka kutuwanyika katika eneo la gereza dhidi yao pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na aliyekuwa Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na wengine 21 ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Mbali na shtaka hilo, shtaka hilo, washtakiwa pia wanakabiliwa na mashtaka ya kufanya mkusanyiko usio halali, kuharibu mali, kutoa lugha ya kuudhi na kufanya shambulio kwa askari magereza.
Mapema, wakili wa Serikali Esther Martin alidai kuwa, kesi hiyo ilipelekwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa lakini washtakiwa wanne kati ya 27 hawakuwepo hivyo akaomba mahakama itoe hati ya kukamatwa washtakiwa hao na wadhamini wafike mahakamani kutoa maelezo ya kwanini washtakiwa hawakutokea mahakamani.
Hakimu Shaidi alipotaka kujua sababu ya kutokufika kwao mdhamini wa mshtakiwa Yihana Kaunya alijitokeza na kueleza kuwa mshtakiwa huyo alishindwa kusafiri kutoka Bunda anakoishi kwa sababu anasumbuliwa na vidonda vya tumbo.
Hata hivyo, hakimu Shaidi amewasisitiza wadhamini kuhakikisha washtakiwa wote wanafika mahakamani na baadaye akatoa amri ya kukamatwa washtakiwa watatu ambao hawakutoa taarifa na kuwataka wadhamini kufika mahamamani kutoa maelezo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 15, 2021 itakapokuja kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...