MKUU wa Mkoa wa Ruvuma
Christina Mndeme amewaagiza maafisa Tarafa na viongozi wote ngazi ya Wilaya
kusimamia utunzaji wa vyanzo vya maji ili viwe endelevu.
Mndeme ametoa agizo
hilo wakati anafungua mkutano wa wadau wa sekta ya maji mkoani Ruvuma
kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Mndeme pia ameagiza
wote wanaofanya shughuli za kiuchumi kwenye vyanzo vya maji kuondolewa na
kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ya mazingira ya mwaka 2004 ya sheria ya
RUWASA ya mwaka 2019.
Maagizo mengine
yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa katika kikao hicho ni Halmashauri zote na
sekretarieti ya Mkoa kuwajibika kikamilifu katika kutekeleza na kusimamia
majukumu yote yaliyoorodheshwa kwenye sheria namba tano ya huduma ya maji ya
mwaka 2019.
“Mameneja wa RUWASA
Wilaya kwa kushirikiana na Halmashauri zote zihakikishe kwamba miradi iliyopo
na mingine itakayojengwa inaunda vyombo huru vya watumiaji maji kwa sheria
namba tano ya mwaka 2019 kabla au ifikapo Mei 31,2021’’,alisisitiza Mndeme.
Mndeme pia ameagiza
katika kikao cha Baraza la madiwani cha kila robo katika Halmashauri zote iwepo
mada ya kudumu ambapo Mameneja wa RUWASA katika wilaya husika watatoa taarifa
kuhusu hali ya upatikanaji na usajili wa vyombo vya watumiaji maji.
Mkuu wa Mkoa pia
ameagiza RUWASA Wilaya na Mkoa zishirikiane na Mamlaka ya Majisafi na Usafi
wa mazingira SOUWASA sanjari na ofisi za mabonde ya maji katika kutafuta vyanzo
vya maji na kuandaa mipango ya utunzaji wa vyanzo vya maji.
“Naagiza fedha
zitokanazo na mauzo ya maji zikaguliwe na mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ili
kujiridhisha namna fedha hizo zilivyotumika,endeleeni kuwachukulia hatua
wanaoharibu kwa makusudi miundombinu ya maji na vyanzo vya maji’’,alisema
Mndeme.
Kwa upande wake Meneja
wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) Mkoa wa Ruvuma
Mhandisi Rebman Ganshonga ameyataja majukumu ya RUWASA kuwa ni kuandaa mipango
ya kusanifu miradi,kujenga na kusimamia uendeshaji wake.
Majukumu mengine ni
kuendeleza vyanzo vya maji kwa kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi,kuchimba
visima na kujenga mabwawa sanjari na kufanya matengenezo makubwa ya miundombinu
ya maji.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...